Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania inajipanga kutumia teknolojia ya GMO katika kilimo

Mahindi yaliyozalishwa kwa teknolojia ya GMO.

Muktasari:

Ni teknolojia ambayo inaweza kumsaidia mkulima kukabiliana na magonjwa na wadudu wa haribiufu wa mazao, kuwa na mimea inayovumilia ukame, kuvuna mazao mengi katika eno dogo na hata kuongeza viinilishe vyakula kama vile protini, vitamini, madini na mafuta.

Ni teknolojia inayotarajia kuleta mapinduzi ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ambao wanalima bila tija. Hiyo inaitwa ni teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO).

Ni teknolojia ambayo inaweza kumsaidia mkulima kukabiliana na magonjwa na wadudu wa haribiufu wa mazao, kuwa na mimea inayovumilia ukame, kuvuna mazao mengi katika eno dogo na hata kuongeza viinilishe vyakula kama vile protini, vitamini, madini na mafuta.

Baada ya mijadala ya muda mrefu kuhusu kilimo cha mazao yanayozalishwa kwa teknolojia ya bayoanuwai (bayoteknolojia), hatimaye serikali imeridhia kuendelea taaluma hiyo na kuingia katika ngazi ya kisasa zaidi ya uhandisi jeni.

Hata hivyo, ni teknolojia ambayo imepata upinzani kwenye maeneo mengi duniani kwa hisia kuwa inaweza kusababisha madhara kwa binadamu na mazingira.

Pamoja na hali hiyo, wanasayansi wamefanya tafiti mbalimbali na wamekuja na majibu kuwa mazao yaliyozalishwa kwa teknolojia ya GMO hayana madhara kwa binadamu wala viumbe.

Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula, Godfrey Zambi anasema kutokana na utandawazi unaoendelea duniani Tanzania haiwezi kukwepa maendeleo ya bioteknolojia katika uendelezaji wa sekta ya kilimo.

“Serikali ina nia ya dhati ya kubadili kilimo cha Mtanzania kiwe cha kisasa na chenye tija. Hii inawezekana tu pale tunapowawezesha wakulima wetu kupata fursa ya kutumia teknolojia mbalimbali,” anasema na kuongeza: “wengine wanafaidi, sisi tunasubiri nini?”

Anasema Serikali imeshaweka misingi ya kuendeleza bioteknolojia nchini pia imeweka mikakati ya kuhakikisha kunakuwapo matumizi salama ya teknolojia hii ya uhandisi jeni.

Teknolojia ya uhandisi jeni

Mtafiti wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo na Chakula, Emmarold Mneney anaelezea kuhusu uhandisi jeni na kusema ni teknolojia ambayo hubadilisha mmea au mnyama kwa kwa njia ya teknolojia ya kuchanganya jenetiki yaani DNA (chembe hai) za mmea au mnyama mmoja na mwingine tofauti, ili kuupa mmea huo mpya au mnyama huyo mpya tabia zisizo za asili.

Uzuri wa teknolojia ya GMO ni kwamba inaweza kumsaidia mkulima kuvuna mazao mengi katika eneo dogo, kutotumia au kutumia kidogo dawa za kuulia wadudu na mazao kumea vyema kwenye maeneo yenye mvua kidogo.

Kwa mfano, mimea inayoota baharini, kwenye chumvi au katika miamba hufanyiwa utafiti wa kimaabara na hivyo jeni zake huchukuliwa na kuwekwa katika mimea mingine.

“Teknolojia hii hutafuta sifa iliyo katika mmea mmoja na kuipandikiza katika mmea mwingine ili kuhamisha sifa hizo,” anasema Dk Mneney.

Dk Mneney anasema nia na madhumuni ya kutumia teknolojia ya uhandisi jeni ni kupambana na changamoto za magonjwa, ukame na mabadiliko ya tabianchi.

Anasema teknolojia hii huweza kupambana na magonjwa mbalimbali ya mazao kama ugonjwa wa batobato unaoshambulia mihogo na ule unaoshambulia migomba.

“Sababu kubwa ya kutumia teknolojia hii ni kulinda usalama wa chakula kwani mkulima huwa na uhakika wa kupata mazao mengi na pia mazao yenye afya,” anasema

Ripoti ya mwaka 2014 ya hali ya biashara ya mazao yaliyozalishwa kwa kutumia teknolojia ya bioteknolojia inaeleza kuwa hadi sasa wakulima milioni 18 duniani wanatumia teknolojia hii.

Kadhalika, nchi 28 duniani zinatumia teknolojia hii na nchi 20 kati ya hizo ni zile zinazoendelea na wakulima milioni 16 kati yao ni wenye kipato cha chini.

Katika ripoti hiyo, mazao ya GMO yaliyoingia sokoni mpaka sasa ni soya, pamba, canola na mahindi huku nchi za Afrika ambazo tayari zimeanza kuvuna mazao ya GMO ni Afrika Kusini, Burkina Faso, Misri na Sudan.

Tangu kuvumbuliwa rasmi kwa teknolojia hiyo mwaka 1996 mpaka sasa kuna hekta 3.3 milioni za mazao ya GMO.

Manufaa ya GMO

Dk Mneney anasema GMO tofauti na yanavyodhaniwa na wengi lakini yana faida kuliko hasara ambapo anaeleza kuwa humpa mkulima ongezeko la mavuno kwa asilimia 22. Hupunguza wadudu waharibifu kwa asilimia 37 na kuongeza kipato kwa asilimia 68.

“Tusiipige vita teknolojia hii kwani haina madhara zaidi ya faida, ndiyo maana hata serikali ilipeleka wataalamu wake katika nchi zilizokubali uhandisi jeni ili wakajifunze na kuona manufaa yake,” anasema.

Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Kilimo na Chakula, Dk Fideli Myanki anasema ripoti ya hali ya biashara ya mazao ya GMO inaonyesha ongezeko la wakulima wadogo wanaolima kwa kutumia teknolojia hiyo na kueleza kuwa hiyo ni fursa kwa wadau kuandaa sera ya kilimo.

Kaimu Mkurugenzi wa Maarifa wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, (Costech) Dk Nicholas Nyange anasema tume hiyo inashirikiana na wadau wa ndani na nje kuhakikisha utafiti unafanyika ili kuiwezesha teknolojia hii kuwa bora kwa Watanzania.

“Taarifa hii ni changamoto kwetu kwani inatuhamasisha kutumia teknolojia hii ili kupeleka mazao ya GMO sokoni na kuyafanyia utafiti,” anasema.

Changamoto za GMO

Katika kufafanua umuhimu na changamoto za kilimo cha mazao ya GMO, Zambi anasema bado kuna wasiwasi miongoni mwa wanajamii kuhusu athari zinazoweza kupatikana kutokana na teknolojia hii licha ya kuwapo kwa miongozo na mfumo wa usimamizi wa matumizi salama ya teknolojia hiyo.

“Lakini pamoja na hayo, Tanzania haiwezi kukwepa maendeleo ya bioteknolojia katika uendelezaji wa sekta mbalimbali hususani kilimo,” anasema.

Hata hivyo, Zambi anasema serikali imeweka mikakati katika kushughulikia masuala ya matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa.

Kwa mfano serikali imeandaa sera ya Taifa ya Bioteknolojia ya mwaka 2010 yenye lengo la kujenga uwezo wa kutumia teknolojia hiyo kwa kuzngantia faida kwa kilimo, wanyama, viwanda, mazingira na binadamu.

Zambi alitaka wananchi wapewe elimu ya kutosha kuelewa msimamo wa serikali kuhusu mazao ya GMO hasa kwa kuangalia sera, sheria , mfumo na kanuni zilizowekwa za bioteknolojia.

Nchi mbalimbali zimekuwa zikitamani kuona wananchi wake wanazalisha chakula cha kutosha, pengine kuwa na ziada kwa ajili ya kuuza, lakini zimekuwa na hofu ya kujiingiza kichwa kichwa kwa kuwa ni teknolojia mpya.

GMO ina madhara?

Wataalamu mbalimbali wamekuwa wakisema kuwa mazao yanayopatikana kwa teknolojia hii hayana madhara, baada ya kufanya tafiti mbalimbali.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu na wanaharakati wamekuwa wakibashiri kuwa huenda mazao ya namna hiyo yakasababisha athari za kimwili na mazingira. Pamoja na kauli hizo hakuna hata mmoja ambaye amekuja na uthibitisho wa kisayansi.

Umoja wa Ulaya (AU) umetoa ripoti yao inayojumuisha miradi ya utafiti zaidi ya 130 yenye lengo la kutathmini madhara ya uhandisi jeni.

Ripoti hiyo ilijiridhisha kuwa mazao ya chakula yaliyolimwa kwa teknolojia ya uhandisi jeni hayana madhara ukilinganisha na mazao ya kawaida.

Utafiti wa EU, uliotumia zaidi ya Euro 200 milioni ulifanywa kwa miaka 25 na kuwashirikisha wadau zaidi ya 500 duniani.

Hii ndiyo kusema pamoja na Tanzania kutaka kujiridhisha kwa kufanya utafiti wa matumizi ya teknolojia hiyo, kuna tafiti nyingi zinazoshawishi kuwa ni salama katika kuinua uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara nchini.