Dah! ulikuwa mwaka wa mapenzi kuliko sanaa

Muktasari:

  • Irene Uwoya haonyeshi kama staa wa filamu. Haeleweki anafanya biashara gani zaidi ya kutuua insta kwa pamba flani amazing za kutugombanisha na kina Eva wetu majumbani. Na hawa ndio mastaa wa kike ambao wakitolea macho sanaa wanaweza kurudi kwenye ubora wao. Wana mashabiki wengi.

Katika baa moja maarufu mitaa ya Kurasini, nipo na mrembo. Ninaposema mrembo nielewe, sijawahi kusifia kiumbe wa kike kindezindezi tu. Wema Sepetu? Labda lugha yake ya Kiingereza ndio inaweza kupata heshima ya kukaa kwenye mwili wa kiumbe huyu.

Ni wale warembo ukiwa nao unatumia pesa bila kikomo na ikiisha hujutii, unachofanya kesho unakopa tena pesa nyingi ili tu ukatumie naye. Shetani hakuwa bwege kumuita Eva kisirisiri na kumrubuni ili aje kumrubuni msela wetu Adam.

Huyu Eva niliyekuwa naye. Angetumiwa na shetani kunirubuni siyo tu ningekula lile tunda la mti wa katikati. Bali ningekula na mti mpaka mizizi yake ili afurahi. 'Siwezagi' kujivunga mbele ya viumbe uzao wa Eva. Nikipenda nachukia mpaka pesa. Sizitaki kwenye akaunti yangu nazitoa zikakae kwake milele.

Watu walikuwa wakicheza na kufurahi utadhani wote matajiri. Sikuwa na furaha. Lakini nikalazimisha niwe nayo kinguvu. Nikaagiza kinywaji kinachohifadhiwa ndani ya chupa yenye ustaarabu wa kipimbi sana. Eti haiwezi kukaa kitako mezani mpaka ilazwe. Mwisho wa siku ni wewe mnywaji unaishia kulala ukikizidisha.

Ghafla nikasikia shangwe kubwa la wazee kwa vijana. Wahudumu nao wakihudumia huku wakitingisha viungo vinavyotikisika kwenye miili yao. Kisa 'Dijei' kapiga ule wimbo uliofungiwa. Mpaka nikajiuliza kama ndio hivi ni nani sasa ambaye Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wanadai anaharibika kimaadili kwa huu wimbo? Maana walioufurahia nikiwatazama naona wameshaharibika kimaadili kuliko maneno ya wimbo wenyewe. Sikujali nikaendelea na kinywaji huku macho yangu yakiendelea utalii wa ndani kwenye mwili wa kiumbe pendwa kando yangu. Naye mwili aliutikisa kufuatisha mapigo ya wimbo ule.

Sikuwahi kuusikiliza wimbo ule kwa umakini. Siku hiyo niliusikiliza vyema maana ulirudiwa zaidi ya mara tatu. Nikagundua kuwa kosa la Mbosso, Billnas na Whozu ni matukio ya video ya wimbo tu. Lakini mashairi yake ndio lugha iliyotumika hata pale baa.

Tuachane na wasanii maana mwaka huu wameutumia kwa mapenzi zaidi ya vipaji vyao. Dunia inaenda kasi sana mara hii Farid Kubanda anapita kwenye mikato ya 'Amapiano' kuliko Marioo. Kweli 'hipapu' imeenda na upepo wa kisurisuri. Kifupi Imetengwa.

Mwaka huu Mondi alitutangazia ni wa bandika bandua. Yaani maisha yake 'aliyadediketi' kwenye korido za studio na 'lokesheni' za video zake. Lakini ukweli ni kwamba Mondi mwaka mzima amekuwa 'bize' na mapenzi kuliko studio.

Familia na pisi zake 'zilitekova' kwa mwana. Kuanzia Natasha, Zuchu mpaka bi mkubwa wa 'Sauzi'. Ahadi ya kutoa ngoma kila mwezi ilitoweka, ingawa kakusanya tuzo kubwa kadhaa na kupiga mashoo flan hivi amazing. Kitu ambacho kwake ni kawaida.

Hata hivyo licha ya kutoa nyimbo kadhaa. Lakini Mondi kafanikiwa kukimbiza kwenye ngoma ambazo ameshirikishwa na wanamuzki wenzake. Kama vile goma la Jux pamoja na lile dude la Ggwaragwara. Yeye kama yeye ngoma zake hazijatembea kwa 'levo' ya ukubwa wake.

Harmonize amekuwa na mwaka mtamu kisanii. Lakini naye ubongo wake ulitumika zaidi kuwaza mapenzi.

Huu ni mwaka ambao mastaa hawa waliwekeza zaidi kwenye hisia za mapenzi kwa asilimia 70 na iliyobaki wakaiweka  kwenye sanaa.

Tukio kubwa zaidi kwa mwaka unaoisha kwenye familia ya sanaa ni ujio wa mikopo kwa wasanii. Zaidi ya hilo hakuna tofauti. Wanamuziki na waigizaji wamefanya yaleyale  kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo.

Irene Uwoya haonyeshi kama staa wa filamu. Haeleweki anafanya biashara gani zaidi ya kutuua insta kwa pamba flani amazing za kutugombanisha na kina Eva wetu majumbani. Na hawa ndio mastaa wa kike ambao wakitolea macho sanaa wanaweza kurudi kwenye ubora wao. Wana mashabiki wengi.

Basata kama kawaida wazee wamekula pozi pale Ilala wanasikilizia tu. Bwege gani atoe wimbo wa kibwege wamfungie kibwege. Hawana mipango, mikakati wala mizuka ya kuendeleza sanaa.

Wamekuwa kama mgambo wa 'site' ambao wanavizia watu wafanye kosa wamkamate. Mbali ya kufungia nyimbo na wanamuziki, Basata wamekuwa watu wa kutoa au kufuta vibali vya maonyesho au shughuli za sanaa.

Basata ni mzazi na mlezi wa sanaa zote. Ni jukumu lake kulea, kuendeleza, kukuza, kulinda na kuokoa sanaa inapobidi ili kufanya iendelee kuwepo. Lakini pale Ilala wamejikita kwenye eneo moja tu la kufungia nyimbo au wanamuziiki. Hata wajumbe wao ni wanamuziki na waigizaji tu. Sanaa nyingine ipo kapuni.

Wasanii wanawaza siasa muda mwingi. Siasa imekuwa sanaa na sanaa imekuwa siasa. Mwaka unaisha kwa mwaka ujao huenda tukapoteza kila kitu kwenye sanaa kwa sababu sanaa inatelekezwa na wanasanaa wenyewe wakiishi kwa matukio zaidi ya vipaji.