Sababu anguko makundi ya Bongofleva

What you need to know:

Hata waandaaji wa tuzo za TMA hawajaona sababu ya kuweka kipengele cha kundi bora la Bongofleva, kwani hakuna makundi mengi.

Kadiri miaka inavyosonga, ndivyo na idadi ya makundi ya muziki wa kizazi kipya inavyozidi kupungua, masilahi duni na mabadiliko ya kimfumo vinatajwa kuchangia hilo.

Kipindi cha nyuma Bongofleva ilibebwa na kutangazwa na makundi kama HBC, Gangwe Mobb, East Coast, TMK Wanaume, Nako 2 Nako Soldiers, Kikosi cha Mizinga, Watengwa, Tip Top Connection, Wateule, Chemba Squad, Park Lane, Daz Nundaz.

Hata hivyo, mambo yamebadilika, mathalani ni msimu wa pili huu zinaenda kufanyika tuzo za muziki Tanzania (TMA) bila kuwa na kipengele cha 'Kikundi Bora cha Mwaka Bongofleva' wakati kabla ya kusimama tuzo hizo mwaka 2015 kilikuwepo. Makundi yalishinda tuzo za TMA.
Miongoni mwa hayo ni; Jambo Squad (2013), Weusi (2014) na Yamoto Band (2015), lakini sasa fursa hiyo haipo tena kwa makundi ya Bongofleva.

Wakizungumza na gazeti hili, wasanii kutoka makundi ya Mabantu, Nako 2 Nako, Yamoto Band na Kikosi cha Mizinga wamekuwa na maoni tofauti kuhusu uchache wa makundi katika Bongofleva sasa, wengi wao wanataja suala la masilahi ndio mzizi wa tatizo.

Kundi la Mabantu limesema hata sasa makundi kwenye Bongofleva yapo ila yanayopata nafasi ya kusikika ni machache, miongoni mwa hayo ni wao, huku wakisema hamasa inahitajika ili makundi yenye nguvu yawe mengi kama hapo awali.

“Hatuwezi kusema makundi ni machache, yapo mengi ila yaliyopata nafasi ya kusikika au yanayosikika ni machache, kama tunataka kuwa na makundi mengi inabidi hamasa iwepo kama hicho kipengele cha Kundi Bora katika tuzo.

“Kama tunahitaji makundi katika hii tasnia tuna kila sababu ya kuzidi kuyapa nafasi makundi ambayo yanafanya vizuri sasa hivi, ili kutengeneza kizazi kingine kama tulivyokuwa tunashuhudia kwa kaka zetu, TMK, East Coast, Kikosi cha Mizinga na makundi mengine,” anasisitiza mkuu wa kundi la Mabantu.

Anasema si kweli kuwa uchache wa makundi ndio umeifanya TMA kutokuwa na kipengele cha kundi bora, kwani makundi yapo, wakiwamo wao, Navy Kenzo n.k na yanafanya vizuri, huku akikumbushia tuzo za mwaka jana, Prodyuza Kenny alikuwa peke yake katika kipengele cha Prodyuza bora wa singeli.

Naye Lord Eyes aliyetamba na kundi la Nako 2 Nako Soldiers na sasa Weusi, anasema tasnia ya burudani Bongo yenyewe ndio hasa imesababisha makundi mengi kusambaratika kutokana na malipo kiduchu wakati watenda kazi ni wengi. "Ni tasnia yenyewe imeshindwa kuhudumia makundi ndio maana yanapungua, imeshindwa kuwalipa, kuwalea na kuwabeba kwa sababu wanataka walipe fedha ya mtu mmoja kwa kundi zima, inakuwa tabu ndio maana makundi yanashindwa kudumu," anasema Lord Eyes.

Hata hivyo, Lord Eyes anasema wasanii kutofahamiana vizuri napo kumechangia makundi mengi kusambaratika, huku akieleza kuwa kundi la Weusi limedumu kwa sababu wanafahamiana kitambo na wamekuwa familia moja. "Kama mmekutana juu kwa juu tu mkaanzisha kundi inakuwa ni rahisi kuvunjika, ila kama mnajua kama familia ndio mnaweza kudumu kama ilivyo kwa Weusi ambao ni chapa tano zipo pamoja.

Kila mmoja anaweza kusimama mwenyewe lakini kwa nini tupo pamoja? Urafiki wetu umefika hadi kwenye familia," anasema Lord Eyes.

Ikumbukwe awali Lord Eyes alikuwa na kundi la Hood Squard Hardcore Unit, akiwa na wenzake JCB na Spark Dogg, baadaye akaungana na G Nako na Bou Nako kutokea Crinic Mob, ndipo wakaunda kundi la Nako 2 Nako, baadaye tena yeye na G Nako wakajiunga na Weusi.
Kwa upande wake Beka Flavour aliyekuwa kundi la Yamoto Band na Aslay, Mbosso na Enock Bella, anasema wasanii wanashindwa kudumu kwenye makundi kutokana masilahi tu. Wengi hujiengua na kufanya kama solo ukizingatia muziki sasa umekuwa ni kama biashara nyingine. "Hata kundi lifanye vizuri kiasi gani halafu promota akataka shoo ya kundi akaambiwa tupo wanne basi tulipe Sh20 milioni kwa shoo moja ili tugawane walau Sh5 milioni kila mmoja inakuwa ngumu, lakini msanii mmoja anayefanya vizuri anaweza kulipwa Sh10 milioni peke yake," anasema Beka Flavour.

Kuhusu kukosekana kwa kipengele cha Kundi Bora kwenye tuzo za TMA, Beka anasema uchache wa makundi yenye ushindani katika Bongofleva inaweza kuwa sababu, hivyo kama kipengele hicho kingewekwa ushindani wa kweli usingekuwepo.

"Hawawezi kuweka kipengele hicho wakati makundi yenyewe hayafiki hata manne, kwa hiyo hapo ushindani unakuwa haupo, nyuma kidogo makundi yalikuwepo mengi na yenye nguvu, sasa hivi kila mtu anafanya muziki solo," anasema Beka Flavour.

Akilizungumzia hilo, Kalapina kutoka kundi la Kikosi cha Mizinga anasema ubinafsi ndio hasa umeua makundi mengi, baadhi ya wasanii walijiona wao ni bora au wana uwezo kuliko wengine, hivyo wanastahili kupata zaidi ya wenzao.
"Sababu kubwa ni ubinafsi, sanaa hailipi kama inavyotakiwa, sasa watu wanaona kinachopatikana kinakuwa kidogo, mtu anaona asimame mwenyewe.

"Zamani watu walikuwa wanafanya kwa mapenzi zaidi, wanapenda muziki wanajikuta kwenye makundi, ikipatikana riziki wanagawana, lakini sasa mambo ya biashara yamekuja, umeingia ubepari kila mtu anaangalia masilahi, hiyo ndio ilileta matatizo," anasema. Hata hivyo, Kalapina anasema kuna makundi yalipokea wasanii waliokuwa wanataka kuwa maarufu tu kisha waendelee na mipango yao mingine. Kalapina anasema kundi lao la Kikosi cha Mizinga hadi leo lipo, ndio kundi pekee Bongo ambalo halijavunjika, tofauti yao ni kwamba baadhi ya wasanii wapo nje ya nchi.

Ndiyo kuna baadhi ya wasanii wapo nje ya nchi, lakini kundi lipo na huwa tunakutana na kufanya kazi, mara ya mwisho mwaka 2017 tulifanya tamasha la kuadhimisha miaka 13 ya Kikosi cha Mizinga,” alisema Kalapina.