Yanga, Simba kuzoa mamilioni FIFA
Muktasari:
- Malipo hayo yatahusu mchezaji aliyetumika kwa kucheza mchezo husika au kuwemo katika orodha ya wachezaji wa akiba.
Dar es Salaam. Yanga, Simba na Azam FC kila moja ina uhakika wa kupata zaidi ya Sh300 milioni kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani ukiwa ni mgao unaohusiana na Kombe la Dunia 2026 linaloanza keshokutwa Alhamisi huko Canada, Mexico na Marekani.
Mamilioni ambayo Simba, Yanga na Azam zitavuna kutoka FIFA ni kutokana na kutumika kwa wachezaji wao katika mechi za kuwania kufuzu mashindano hayo.
Imeripotiwa kwamba FIFA imepanga kulipa klabu za soka kiasi cha Dola 2,360 (Sh6.2 milioni) ikiwa ni fidia ya kila mechi moja ambayo mchezaji mmoja ameitumikia timu yake ya taifa katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Malipo hayo yatahusu mchezaji aliyetumika kwa kucheza mchezo husika au kuwemo katika orodha ya wachezaji wa akiba.
Kiujumla, Yanga inaonekana itavuna kiasi kikubwa cha fedha kutoka FIFA kwani idadi kubwa ya wachezaji wake ilishiriki mechi nyingi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu wakiwa na timu tofauti za taifa.
Timu hiyo itavuna zaidi ya Dola 141,600 (Sh372 milioni), Simba itapata zaidi ya Dola 129,800 (Sh341 milioni) na Azam itapata zaidi ya Dola 118,000 (Sh310 milioni) kutoka gawio hilo la FIFA.
Klabu nyingine za Tanzania ambazo zitanufaika na mgao huo wa FIFA kwa kutoa wachezaji ambao wamezitumikia timu za Taifa katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 ni Singida Black Stars, Dodoma Jiji, Coastal Union, JKT Tanzania na TRA United.
Mchezaji ambaye ataiingizia Yanga kiasi kikuba cha fedha ni beki Ibrahim Hamad 'Bacca' ambaye yeye amecheza idadi ya mechi saba za kuwania kufuzu mashindano hayo.
Kwa upande wa Azam FC, mchezaji ambaye atachangia kuwapa kiasi kikubwa cha fedha ni Feisal Salum ambaye ameitumikia timu ya Taifa ya Tanzania katika mechi saba kama ilivyo kwa Bacca.
Simba wao watapata kiasi kikubwa cha fedha kupitia kwa kipa Moussa Camara ambaye amecheza mechi sita za kuwania kufuzu Fainali hizo za Kombe la Dunia.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Azam FC, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi' amesema kuwa habari hizo ni njema kwao.
"Klabu zimekuwa zikipigania hii haki kwa muda mrefu kwa sababu ndio zinawalea hao wachezaji. Wakiumia klabu zinaingia gharama ya kuwahudumia na hazipati fidia na pia haziwezi kuwatumia kwa hiyo hasara inakuwa mara mbili.
"Hizi kiukweli ni habari njema kiukwelli na niwapongeze FIFA," alisema Zakazi.