Siku ya kwanza darasani kwa mwalimu asiyeona

Mwalimu Michael Kayumbo akiwa katika majukumu yake. Picha na Rehema Matowo

Kama unaamini ulemavu ni kushindwa maisha, unakosea kwa kiwango kikubwa.

Michael Kayumbo (34) mzaliwa wa kijiji cha Mwanhalanga mkoani Shinyanga, ni kielelezo tosha cha namna watu wenye ulemavu wanavyoweza kufanya makubwa kwao wenyewe na kutoa mchango kwa Taifa.

Licha ya milima aliyopanda na mabonde aliyoteremka kama mlemavu wa macho asiyeona, hakukata tamaa. Uvumilivu na subira vimemfikisha katika ndoto yake na ya wazazi wake ya kuja kuwa mwalimu.

Leo ni mmoja wa walimu katika Shule ya Msingi Chato iliyopo wilayani Chato akifundisha somo la uraia kwa wanafunzi ambao tofauti na yeye, wao wanaona.


Alivyopata ulemavu

Mwalimu Kayumbo alizaliwa akiwa mzima, lakini akiwa na miaka mitano alipata tatizo la kuwashwa macho na wazazi wake hawakuwa na uelewa wa masuala ya hospitali, hivyo walimtibu kienyeji kwa kumpeleka kwa waganga wa kienyeji.

“Wazazi wangu waliniambia walitumia dawa nyingi za waganga wa kienyeji, lakini kadri muda ulivyoenda hali ilizidi kuwa mbaya na waligundua sioni pale waliponiwekea chakula badala ya kupokea na kula nilianza kupapasa kukitafuta”anasimulia alivyoanza kupata ulemavu.

Anasema kijijini kwao hakukua na hospitali, hivyo wazazi wake walifunga safari hadi mjini kutafuta huduma. Walipomuona daktari na kufanyiwa vipimo, majibu yalionyesha asingeweza kuona tena, na hiyo ilitokana na kuchelewa kumpeleka hospitali.


Kupata elimu

Kayumbo anayetembea kwa msaada wa fimbo maalumu, anasema kutokana na hali yake, wazazi walisita kumpeleka shule hivyo alikaa nyumbani.

Hata hivyo, kijijini kwao kulikuwa na mwalimu aliyekuwa anafundisha Shinyanga Mjini na mara kwa mara alikua akiwaandikia wazazi wake barua, akiwaeleza ipo shule inayofundisha watoto wenye ulemavu wa macho.

“Haikua rahisi wazazi wangu kukubali mimi kwenda kusoma mjini kwa kuwa nilikua mtoto wa pekee. Waliona watanipoteza, hivyo walipinga lakini yule mwalimu hakukata tamaa,’’ anaeleza.

 April 2000 akiwa na miaka 12 wazazi wake waliridhia akasome na kumpeleka shule ya Msingi Buhangija alikokutana na wanafunzi wengine wenye hali kama yake lakini changamoto kubwa wakati huo ilikuwa kutojua lugha zaidi ya Kisukuma.

Anasema iliwalazimu walimu waanze kumfundisha Kiswahili pamoja na maandishi ya nukta nundu wanayotumia walemavu wa macho ili aweze kwenda sambamba na wenzake.

 Baada ya kuhitimu elimu ya msingi alichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Shinyanga alikosoma hadi kumaliza kidato cha nne, na hapo akaamua kujiunga na chuo cha ualimu.

“Nilituma maombi vyuo tofauti sikufanikiwa licha ya kuwa na sifa za kitaaluma ilinilazimu nikae nyumbani mwaka mzima ndipo 2012 nilipata chuo cha Singachini kilichopo Moshi,’’ anasema.


Ahudhuria mafunzo ya jeshi

Utakuwa unashangaa kama mimi nilivyopata mshangaom mimi baada ya kusikia alihudhuria mafunzo ya jeshi. Ilikuaje?

Kayumbo anasema baada ya kumaliza chuo ilikuwa lazima kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi na yeye alipangiwa kambi ya jeshi Ruvu, alikoungana na wahitimu wengine wengi wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

“Sisi wenye ulemavu tulishiriki zaidi mbinu za ya kijeshi darasani na wakati wa mazoezi tulikaa pembeni tukiwasubiri wenzetu ambao sio wenye ulemavu wakimaliza ndio tunaondoka wote,”anasema.


Siku ya kwanza darasani

Anasema siku ya kwanza darasani haikuwa rahisi kwani wanafunzi walikua hawatulii darasani, hivyo ilimlazimu kutoa elimu ya jamii juu ya watu wenye ulemavu na hili liliwezekana kwa ushirikiano wa walimu wenzake.

“Wanafunzi walikua hawanisikilizi, wananiangalia machoni na kushangaa. Ilinilazimu kuingia na mwalimu mwingine kuwatuliza. Niliwaelimisha juu ya hali yangu ilibidi nianze kuwapa elimu ya kuwa mimi ni mwenye ulemavu wa macho lakini sina tofauti na walimu wengine, ‘’ anasema na kuongeza:

Baadaye walinielewa na wamekuwa wasaidizi wazuri ninapokua darasani na hata nje ya darasa.”

Mwalimu Kayumbo anasema huandaa somo na kuwafundisha wanafunzi akizungumza, huku akisoma maandishi ya nukta nundu na wanafunzi huandika na wakati wa maswali, huyaandaa na kuwapa walimu wenzake majibu ili wamsaidie kusahihisha.

“Kwenye ufundishaji wangu kikubwa ni ushirikiano wa walimu wenzangu. Ninapotaka kazi iandikwe ubaoni, nazungumza mwalimu mwingine ananisaidia kuandika, lakini mara nyingi darasa langu nazungumza na wao wanaandika”anasema.

Kuhusu mitihani anaeleza:“Ikiwa ni mtihani huwa natunga maswali na majibu kwa kuandika kwa maandishi yangu halafu nawasomea walimu wao wanayaandika kwa maandishi ya kawaida na kuwapa wanafunzi, na baada ya mtihani wananisaidia kusahihisha wananipa mrejesho wa somo langu kama wanafunzi wanaelewa au la. Namshukuru Mungu somo langu wanafanya vizuri sana.”


Walimu wenzake

Mwalimu Peleka Dawa anaefundisha watoto wenye ulemavu wa kusikia shuleni hapo anasema Kayumbo ni mwalimu anayependwa na wanafunzi.

“Wanafunzi wanamuelewa hata mitihani ya darasa la saba masomo yake ndio yanafanya vizuri zaidi kwenye mitihani. Wangekuwa hawamuelewi wangefeli somo lake”anasema .

Mwalimu mwingine, Mariam Kihongo anasema wakati wa mtihani somo la mwalimu Kayumbo husahihishwa na jopo la walimu wote kwa kila mwalimu kupewa swali moja na wamekuwa wakifanya kwa upendo.

 Mwalimu mkuu, Wilfred Machugu anasema shule hiyo yenye wanafunzi 2,057, walimu watatu wana ulemavu akiwemo Kayumbo.

Anasema kulingana na uelemavu wake vipo vitu anavyohitaji ikiwemo vitabu vya nukta nundu, lakini shule imeshindwa kumpatia na hadi sasa ana vitabu vya darasa la sita pekee hivyo kushindwa kufundisha madarasa mengine.


Wanafunzi nao?

Dickson Nzigo, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, anasema haoni tofauti ya mwalimu Kayumbo na walimu wengine katika ufundishaji kwani licha ya yeye kutokuandika ubaoni, somo lake wanafunzi wanalielewa na kulifurahia kutokana na mbinu yake ya kupenda kujadiliana zaidi awapo darasani.

Naye Rehema Boniphace mwanafunzi wa darasa la sita, anasema mwalimu huyo anafundisha kirafiki na wanafunzi wamemzoea, hivyo kutoogopa kuuliza swali au kujadiliana naye jambo.


Malengo yake

Mwalimu Kayembo anasema lengo kubwa kwa sasa ni kuongeza kiwango cha elimu. Lakini pia anatamani kuwaona watu wenye ulemavu wa macho wakipata elimu.

Anasema shule zinapaswa kuwa na mifumo ya kuwasaidia wanafunzi wanaofanya vibaya kitaaluma, ili wasaidiwe kuwa wabunifu badala ya kuwa ombaomba wanapomaliza.