Tusiache kuwalea hata kama wako vyuoni
Muktasari:
- Furaha ya kuona jina la mtoto kwenye orodha ya waliochaguliwa imekuwa kubwa kiasi cha kufunika maswali muhimu kuhusu ustawi wao wanapofika katika mazingira mapya ya chuo.
Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikishuhudia ongezeko la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu vya umma na binafsi wakiwa na umri mdogo sana.
Hali hii imekuwa ikitafsiriwa kama ishara ya mafanikio makubwa ya kielimu, na familia nyingi zimekuwa zikijivunia watoto wao wanapofaulu mitihani ya kidato cha nne au sita mapema na kupata nafasi za kujiunga na vyuo vikuu. Furaha ya kuona jina la mtoto kwenye orodha ya waliochaguliwa imekuwa kubwa kiasi cha kufunika maswali muhimu kuhusu ustawi wao wanapofika katika mazingira mapya ya chuo.
Tunaposherehekea mafanikio haya ya kitaaluma, mara chache tunasimama kujiuliza swali la msingi, nani anawasimamia watoto hawa wanapofika chuoni. Wazazi wengi huamini kwamba mafanikio ya kitaaluma ni ishara tosha ya ukomavu wa mtoto, na hivyo kumwachia uhuru wa kujisimamia katika mazingira ambayo kimsingi yanahitaji uzoefu wa maisha na uwezo wa kufanya uamuzi mgumu.
Ukweli ni kwamba, mafanikio darasani hayalingani moja kwa moja na ukomavu wa kisaikolojia na kijamii. Hapa ndipo pengo kubwa linaanza kujitokeza, pengo ambalo linaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa maisha ya vijana hawa.
Ukweli wa maisha ya chuoni
Kisheria, mtoto nchini Tanzania ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18.Hata hivyo, mazingira ya vyuo vikuu hayafuati dhana ya 'In loco parentis' yaani malezi kwa niaba ya mzazi.
Hii ina maana kwamba mwanafunzi wa miaka 17 anapofika chuoni, anachukuliwa kama mtu mzima anayewajibika kikamilifu kwa uamuzi wake, sawa kabisa na mwanafunzi wa miaka 25. Hali hii inaacha pengo kubwa kati ya ulinzi wa kisheria na uhalisia wa maisha ya chuoni.
Fikiria hali halisi ya kijana ambaye kisheria hawezi kusaini mkataba, hawezi kupata hati ya kusafiria bila idhini ya mzazi, lakini anatarajiwa kuishi na kujisimamia kikamilifu katika mabweni au makazi binafsi karibu na chuo.
Katika vyuo, vijana hawa hukutana na mazingira mapya yenye uhuru mkubwa, shinikizo la marafiki, majaribu ya maisha ya chuoni na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja.
Wengi wa wanafunzi hawa hutoka katika shule za bweni, ambazo ni miongoni mwa mazingira yenye udhibiti mkubwa zaidi.
Kwa miaka kadhaa, wameishi chini ya uangalizi wa karibu wa walimu, walezi na sheria kali zinazodhibiti kila nyanja ya maisha yao.
Kisha ghafla, wanajikuta katika mazingira yenye uhuru mkubwa usio na mipaka ya wazi. Mabadiliko haya ya ghafla ni mshtuko mkubwa wa kisaikolojia.
Mwanafunzi ambaye hajawahi kujisimamia anatarajiwa ghafla kuweza kufanya uamuzi sahihi katika mazingira magumu, jambo ambalo si rahisi hata kwa watu wazima.
Changamoto za kiijamii na kisaikolojia
Jamii yetu inaelewa wazi kwamba watoto bado wako katika hatua ya ukuaji wa kimaendeleo, ndiyo maana kuna sheria zinazowalinda dhidi ya uamuzi mkubwa kama kuingia mikataba, ndoa au matumizi ya pombe.
Hata hivyo, tunapowapeleka vyuoni mapema, tunawatarajia kufanya uamuzi ya kiwango cha juu katika mazingira yenye changamoto nyingi bila ulinzi wa karibu. Hili ni tatizo kubwa la ulinzi wa mtoto ambalo halijapewa uzito unaostahili.
Maisha ya chuoni yana changamoto nyingi, kuanzia shinikizo la marafiki, uhusiano wa kimapenzi, matumizi ya pombe na dawa za kulevya, hadi changamoto za afya ya akili.
Kwa mwanafunzi mdogo ambaye bado hajakomaa kifikra na kihisia, changamoto hizi zinaweza kuwa nzito sana.
Ndiyo maana katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko la mjadala kuhusu afya ya akili miongoni mwa vijana, na inawezekana kabisa kwamba sehemu ya tatizo hili inachangiwa na kuingia mapema katika mazingira ya watu wazima bila maandalizi ya kutosha.
Tatizo lingine ni kwamba mfumo wetu wa elimu umejikita zaidi katika mafanikio ya kitaaluma na kusahau kwamba kuna maisha baada ya darasa. Tunawafundisha watoto jinsi ya kufaulu mitihani lakini hatuwafundishi jinsi ya kuishi maisha. Akili ya darasani si sawa na ukomavu wa maisha. Tunaweza kuwa na mwanafunzi mwenye alama za juu sana lakini asiye na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kila siku za maisha ya kujitegemea.
Wazazi wengi wameanza kuchukulia mafanikio ya mtoto kuhitimu chuo kama kipimo cha mafanikio yao katika malezi. Hali hii imegeuza malezi kuwa mbio za kufikia joho la kuhitimu badala ya safari ya kumlea binadamu kamili.
Tunasahau kwamba tunalea watu, si vyeti. Kuwa na shahada mapema hakumaanishi kuwa mtu amejiandaa kwa maisha.
Hitaji la mabadiliko ya mtazamo na maandalizi ya maisha
Ni muhimu sasa kama jamii kuanza kufikiria upya namna tunavyowaandaa watoto wetu kwa maisha. Elimu haipaswi kuishia darasani bali inapaswa kujumuisha maendeleo ya kihisia, kijamii na kimaadili.
Badala ya kukimbilia kuwapeleka watoto vyuoni mapema, tunaweza kuanza kufikiria mbinu mbadala kama programu za mpito au hata mapumziko ya muda mfupi yanayolenga kuwajengea ujuzi wa maisha halisi.
Programu hizi zinaweza kujumuisha mafunzo ya akili hisia, ujasiriamali, mawasiliano na uwezo wa kufanya uamuzi.
Haya ni mambo yasiyopimwa kwenye mitihani lakini yana mchango mkubwa katika mafanikio ya maisha ya mtu. Tunapaswa kujiuliza kama kweli tunawaandaa watoto wetu kwa maisha au tunawasukuma tu kufikia mafanikio ya kitaaluma bila msingi wa maisha.
Swali la msingi linabaki, je tunafanya hivi kwa sababu ya umasikini au ni kwa sababu hatujaelewa thamani ya utoto na hatua za ukuaji wa binadamu.
Utoto ni kipindi muhimu sana cha kujifunza, si tu masomo bali pia maisha. Kukikimbilia kipindi hiki kunaweza kuwa na gharama kubwa baadaye.
Lengo la malezi halipaswi kuwa kuzalisha wahitimu kwa haraka iwezekanavyo, bali ni kulea watu wazima waliokomaa, wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto na walio tayari kwa dunia halisi. Kuchelewa kidogo lakini kuwa tayari ni bora kuliko kuwahi kufika lakini bila maandalizi.