Umejiuliza sababu ya kumpeleka mtoto shule?
Muktasari:
- Je, wewe ukiwa mzazi umewahi kuketi kwa utulivu na kujiuliza, nini hasa nataka mtoto wangu apate kwa kumpeleka shule?
Dar wa Salaam. Kila asubuhi, wazazi kote nchini tunahangaika kuhakikisha watoto wetu wanaenda shule.
Wapo wanaoamka alfajiri kuwawahisha watito katika vituo vya daladala au mabasi ya shule, wengine huendesha magari yao binafsi, achana na wale wengi wanaotembea wenyewe kwa miguu kuelekea masomoni.
Lakini swali moja la msingi linabaki: Umejiuliza kwa nini unamwamsha mtoto kila siku ili aende shule?
Kwa wengi, majibu yanaweza kuonekana rahisi: "Ni jambo la kawaida," "Wote wanafanya hivyo," au "Ni jukumu la mzazi."
Lakini ukiangalia kwa undani zaidi, utaona kwamba swali hili lina uzito mkubwa unaogusa msingi wa malezi, maadili na mustakabali wa mtoto.
Je, wewe ukiwa mzazi umewahi kuketi kwa utulivu na kujiuliza, nini hasa nataka mtoto wangu apate kwa kumpeleka shule?
Kuna sababu nyingi ambazo zimejengeka katika jamii kuhusu elimu. Miongoni mwa sababu hizo ni utamaduni wa kijamii.Katika jamii nyingi, hasa zile zilizoendelea au zinazopiga hatua kimaendeleo, ni kawaida kuona kwamba mtoto anapaswa kwenda shule mara tu anapofikisha umri wa kutosha. Ni kama desturi, jambo ambalo halihitaji kuulizwa sana. Mzazi anahisi kuwa asipompeleka mtoto shule, atadharaulika, atalaumiwa, au ataonekana mzazi asiyewajibika.
Hii ni nguvu ya jamii na utamaduni unaoathiri uamuzi wa mzazi bila hata kujua kwa undani lengo halisi la elimu hiyo.
Sababu ya pili ni msukumo wa serikali.
Serikali nyingi zimeweka sheria zinazoelekeza kwamba kila mtoto ana haki ya msingi ya kupata elimu. Kwa hiyo, baadhi ya wazazi wanawapeleka watoto shule ili kuepuka matatizo ya kisheria au kuonekana kukiuka wajibu wao wa malezi kwa mujibu wa sheria. Lakini je, ni busara kuridhika tu kwamba unampeleka mtoto shule kwa sababu unapaswa kufanya hivyo, bila kujiuliza madhumuni halisi?
Ya tatu, kufuata wengine na shindani. Wapo wazazi hupeleka watoto shule kwa hoja: “wenzangu wanasomesha.” Ni kama mashindano ya kimya kimya: nani atasomesha mtoto wake shule bora zaidi, nani mtoto wake atapata alama nzuri zaidi, nani atahudhuria shule ya kifahari.
Katika hali hii, elimu inageuka kuwa mbio za mitindo au hadhi ya kijamii badala ya kuwa msingi wa maendeleo ya mtoto binafsi.
Unataka nini kwa mwanao?
Hili ndilo swali kuu ambalo mzazi anayejitambua lazima alijiulize. Elimu si tu tiketi ya kupita kwenye maisha ya kawaida; ni nyenzo ya kumjenga mtu anayefikiri, anayechambua mambo, na anayechukua hatua zenye maana katika maisha yake na kwa jamii.
Kama lengo lako ni kwamba mtoto wako apate maarifa ya kawaida tu kama kusoma, kuandika, kuhesabu, basi hiyo ni hatua ya kwanza tu. Lakini elimu ya kweli haipaswi kuishia hapo.
Mtoto anatakiwa pia ajifunze maisha, maadili, fikra huru, na uwezo wa kuamua kwa busara. Dunia ya leo inahitaji zaidi ya uelewa wa kitabu.
Wazazi wengi huamini kwamba kusomesha mtoto ni njia ya kumwezesha kupata kazi nzuri baadaye. Ni kweli kwamba elimu inaweza kufungua milango ya ajira, lakini je, hiyo pekee ndiyo sababu ya msingi?
Katika ulimwengu wa leo ambapo ajira zimepungua na masharti yake yamekuwa magumu, si vyema kuwekeza kwenye elimu kwa matarajio ya ajira tu. Mtoto anahitaji ujuzi, ubunifu, na uwezo wa kutengeneza nafasi yake mwenyewe hata kama ajira rasmi haipo.
Elimu bora inapaswa kumfundisha mtoto kuwa mbunifu, mjasiriamali, na mwenye uwezo wa kujitegemea.
Badala ya kumwandaa kuwa mwajiriwa tu, mpe elimu itakayomfanya aweze kuwa mwajiri, mbunifu au mchangiaji mkubwa wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kujiajiri ni uwezo wa kuona fursa, kuibua mawazo mapya, na kuyatekeleza kwa vitendo.
Mzazi anayetambua haya huwa na nafasi nzuri zaidi ya kumchagulia mtoto njia sahihi ya elimu. Haimaanishi kwamba mzazi ndiye wa kuamua kila kitu, lakini anapaswa kuwa mshauri mkuu wa mtoto katika safari ya elimu.
Kila mtoto ana kipaji au mwelekeo wa kipekee. Wengine ni wachoraji wazuri, wengine ni wapishi, wengine ni wapenda sayansi au hisabati.
Usimlazimishe mtoto kusoma kitu anachokichukia kwa sababu tu ndicho “kina soko.” Badala yake, msaidie afahamu nguvu zake na jinsi ya kuzitumia vyema.
Mzazi anapaswa kujua mtoto wake anasoma nini, kwa nini anasoma, na analenga kuwa nani. Usiwe mzazi wa kusaini ripoti tu kila mwisho wa muhula. Shiriki katika kuchagua mwelekeo wa elimu, ikiwemo shule, kozi, na hata masomo ya ziada yanayoweza kusaidia kukuza vipaji vya mtoto.
Kumpeleka mtoto shule si jambo la kimazoea au la kufuata mkumbo. Ni uamuzi mzito unaopaswa kufanyika kwa uelewa na malengo madhubuti.
Mzazi anayejitambua haachi tu mtoto wake akisukumwa na mfumo wa elimu au jamii; anahakikisha kwamba kila hatua ya elimu inampeleka mtoto karibu na malengo yake ya maisha.
Kwa hiyo, kabla ya kumvalisha mtoto sare na kumpa begi la shule, jiulize:
Ninataka nini hasa kwa mtoto wangu? Na elimu hii tunayompa, itamfikisha kweli huko?
Hayo ni maswali ya mzazi anayewajibika, anayejali na anayetaka mustakabali bora kwa mtoto wake na kwa jamii kwa ujumla.