Unesco: Elimu ya juu injini ya mabadiliko duniani
Muktasari:
- Katika ripoti hiyo, Unesco inaonya kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi kwa wakati mmoja, zikiwemo ukosefu wa usawa wa kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, vita, pamoja na athari za teknolojia mpya kama Akili Unde.
Paris. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limetoa ripoti mpya inayotaka mageuzi makubwa ya elimu ya juu duniani, likisisitiza kuwa sekta hiyo inapaswa kuwa kiini cha mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Ripoti hiyo iliyotolewa Machi 12, 2026, inaeleza kuwa elimu ya juu inapaswa kuongoza katika “kuelekeza mabadiliko, kuzalisha ustawi na kuhakikisha dunia inakuwa yenye amani, haki na endelevu.”
Ripoti hiyo iitwayo: ‘Kubadilisha Elimu ya Juu: Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuunda Dira na Hatua, inatokana na maazimio ya mkutano wa dunia wa elimu ya juu uliofanyika Barcelona mwaka 2022.
Katika ripoti hiyo, Unesco inaonya kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi kwa wakati mmoja, zikiwemo ukosefu wa usawa wa kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, vita, pamoja na athari za teknolojia mpya kama Akili Unde.
Aidha, imeelezwa kuwa kuna dalili za kupungua kwa imani ya jamii katika elimu ya juu, jambo linalohitaji hatua za haraka kurejesha hadhi ya vyuo vikuu.
Kanuni mpya za mageuzi
Ripoti hiyo imeweka kanuni saba zitakazoongoza mageuzi ya elimu ya juu, zikiwemo kulinda uhuru wa kitaaluma, kukuza ubunifu na fikra huru, pamoja na kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa elimu.
Kanuni nyingine ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuweka kipaumbele katika uendelevu wa mazingira na kuboresha uelewa wa ubora wa elimu.
Kwa mujibu wa Unesco, kanuni hizo zitasaidia kujenga mfumo wa elimu unaoweza kukidhi mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.
Takwimu zilizotolewa zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2024 kulikuwa na wanafunzi milioni 269 wa elimu ya juu duniani, huku milioni saba wakisoma nje ya nchi zao katika taasisi zaidi ya 24,000.
Ripoti inaeleza kuwa mifumo ya elimu ya juu inapaswa kubadilika ili kuwa jumuishi zaidi na kuruhusu wanafunzi kujifunza katika maisha yao yote badala ya kuishia katika hatua fulani ya umri.
Aidha, vyuo vikuu vinatakiwa kuacha mtazamo wa kumlenga mwanafunzi wa umri mdogo pekee na badala yake kufungua milango kwa watu wa rika zote.
Unesco pia inapendekeza kuanzishwa kwa mbinu mpya za kujifunza, ikiwemo elimu ya vitendo, mafunzo kazini na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mbinu hizo zitasaidia kuwajengea wanafunzi ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maisha ya kila siku.
Ubora wa elimu changamoto
Katika uzinduzi wa ripoti hiyo, wadau mbalimbali walieleza wasiwasi kuhusu kushuka kwa viwango vya uadilifu katika elimu, hususan ongezeko la udanganyifu katika mitihani na vyeti bandia.
Mwakilishi wa Kenya katika shirika hilo, Peter Ngure, alisema vitendo hivyo vinadhoofisha imani ya jamii katika mfumo wa elimu na kushusha thamani ya vyeti halali.
Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora na kuhakikisha nidhamu katika taasisi za elimu.
‘’Ninazungumza hasa nikiwa naangazia bara ninakotoka, Afrika. Waafrika waliopo hapa kwa kiasi kikubwa watakubaliana nami kwamba udanganyifu katika mitihani unadhoofisha uadilifu wa utafiti. Vyeti vya kitaaluma vilivyoghushiwa na kuenea kwa vyeti bandia vinapunguza imani ya umma, vinadhalilisha mafanikio halali na kudhoofisha taasisi zetu,’’ alisema.
Aliongeza: “Pindi uadilifu unapoporomoka, msingi mzima wa maarifa nao hubomoka. Hivyo basi, tunapaswa kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora, kuboresha usimamizi wa mitihani kwa kutumia majukwaa salama ya kidijitali, kuweka adhabu kali kwa udanganyifu wa kitaaluma na kuhamasisha utamaduni wa uaminifu.’’
Uhuru wa kitaaluma hatarini
Ripoti hiyo pia imeonya kuwa uhuru wa kitaaluma unakabiliwa na vitisho katika baadhi ya maeneo duniani, kutokana na shinikizo la kisiasa na kiuchumi.
Imeelezwa kuwa uhuru huo ni msingi wa utafiti na ubunifu, hivyo unapaswa kulindwa ili vyuo vikuu viweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Harald Nybølet, Naibu mwakilishi wa kudumu wa Norway katika shirika hilo, alisema: “Norway inapenda kusema maneno machache kuhusu hilo. Uhuru wa kitaaluma uko hatarini. Tunaona serikali zikiingilia kile kinachopaswa kufundishwa na kufanyiwa utafiti. Tunaona mifumo ya ufadhili ikiathiri kimyakimya maswali gani yanaonekana kuwa ya muhimu kuulizwa, na tunaona watafiti wakilipa gharama binafsi kwa kufuatilia matokeo yasiyowafurahisha baadhi ya watu.’’
Aliongeza: ‘’Hili si jambo la kufikirika tu. chuo kikuu ambacho hakiwezi kufuata ushahidi kinakoma kuwa chuo kikuu kwa maana halisi. Tunapaswa sote kujikumbusha kuchukulia kwa uzito mapendekezo ya Unesco ya mwaka 1997 kuhusu hadhi ya wafanyakazi wa kufundisha elimu ya juu, kama dhamira halisi, si utaratibu wa kawaida tu.’’
Teknolojia na nafasi ya Akili Unde
Kuhusu matumizi ya teknolojia, ripoti imeeleza kuwa akili unde inaweza kusaidia kuboresha elimu lakini isitumiwe kuchukua nafasi ya uwezo wa binadamu wa kufikiri na kufanya uamuzi.
Wataalamu wamesisitiza kuwa teknolojia inapaswa kuwa nyenzo ya kusaidia, si mbadala wa ubunifu na fikra za binadamu.
Elimu ya maisha yote ipewe kipaumbele
Ripoti hiyo imeweka mkazo mkubwa katika dhana ya kujifunza maisha yote, ikieleza kuwa elimu haipaswi kuishia darasani bali iwe mchakato endelevu.
Mfumo wa elimu unapaswa kuwa na unyumbufu ili kuwapa watu nafasi ya kujifunza kulingana na mahitaji yao na mazingira wanayoishi.
Kwa ujumla, Unesco imeweka wazi kuwa elimu ya juu lazima ibadilike ili iendane na mahitaji ya dunia ya sasa. Mageuzi hayo yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo serikali, taasisi za elimu, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.
Ripoti hiyo inasisitiza kuwa bila mabadiliko hayo, elimu ya juu inaweza kushindwa kutimiza wajibu wake wa kuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa jamii.