Alikuwa ‘Shamba Boy’ sasa anamiliki studio ya muziki

Bruno Kayenzi
Muktasari:
- Ukibahatika kukutana naye hutaamini kuwa kijana huyu aliwahi kuishi kama mnyama na mtu aliyeogopwa katika jamii kutokana na maisha ya uhuni na uvutaji bangi aliyoyatumikia kwa muda mrefu.
- Ukitaja waimbaji wa nyimbo za injili ambao wameonekana kufanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni huwezi kuacha kumtaja Bruno Kayenzi anayefahamika kwa jina maarufu la Mr Potelea Mbali, jina ambalo limetokana na wimbo wake unaopendwa zaidi.
Maisha ni safari ndefu ambayo hakuna ajuaye kesho itakuwaje. Kauli hii inatoa funzo kutomdharau mtu yeyote unayekutana naye katika maisha yako.
Ukibahatika kukutana naye hutaamini kuwa kijana huyu aliwahi kuishi kama mnyama na mtu aliyeogopwa katika jamii kutokana na maisha ya uhuni na uvutaji bangi aliyoyatumikia kwa muda mrefu.
Ukitaja waimbaji wa nyimbo za injili ambao wameonekana kufanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni huwezi kuacha kumtaja Bruno Kayenzi anayefahamika kwa jina maarufu la Mr Potelea Mbali, jina ambalo limetokana na wimbo wake unaopendwa zaidi.
Bruno alifanya mahojiano na mwandishi wa makala hii na kuelezea maisha yake.
Mwandishi: Kwa nini uliamua kuimba nyimbo za injili na siyo aina nyingine kama Bongo Fleva?
Bruno: Nimewahi kuimba aina hiyo niliamua kuachana na mambo ya ulimwengu huu na kuamua kuyatoa maisha yangu kumtumikia Mungu. Kabla ya kuimba muziki wa injili hakukuwa na watu wanaonifahamu kama nilivyo kwa sasa. Nikisimama jukwaa lolote nafanya vizuri na watu wanabarikiwa sana kupitia nyimbo zangu.
Mwandishi: Uliingiaje kwenye muziki?
Bruno: Nilifika jijini Dar es Salaam na kuanza kufanya kazi ya kutunza bustani (Shamba Boy) mwaka 2006 na nikafanya kazi hiyo kwa miezi miwili kabla ya kuacha na kujihusiha na biashara ndogo ndogo kutembeza bidhaa (machinga). Baadaye nilijiunga na kundi la sanaa la Nanjilinji na kuigiza filamu kadhaa ikiwa ni pamoja na Mapito na Nani Mtetezi.
Mwandishi: Kabla ya kuwa mwimbaji wa nyimbo za injili na kuamua kuokoka maisha yako yalikuaje?
Bruno: Nimepitia maisha ya ajabu zamani kwani nilipoondoka sehemu nilipofikia nikitokea nyumbani kwetu Iringa, nilijiunga na makundi ya vijana ambao taratibu nilianza kuvuta bangi na ulevi.
Mwandishi: Kuna tofauti gani unazoziona kwa Bruno huyu wa sasa na yule wa zamani?
Bruno: Ukiacha kuwa kwa sasa namiliki studio yangu ya Ebenezer Record, nina furaha kwa kuwa maisha yangu yamejaa amani.
Mwandishi: Unazungumziaje mapokeo ya kazi zako kwa jamii na je una albamu ngapi?
Bruno: Hadi sasa nimefanikiwa kutengeneza albamu mbili, ya kwanza inaitwa Kwa Yesu Kuna Raha, ambayo ina nyimbo nane. Albamu yangu ya sasa inaitwa Potelea Mbali ambayo ina nyimbo 10 na natarajia kukamilisha video kabla ya kumalizika kwa mwaka huu, hata hivyo audio yake inafanya vizuri.
Mwandishi: Siku hizi Kumekuwa na ujanja mwingi kwa baadhi waimbaji wa muziki wa Injili huku wengi wao wakionekana kupenda fedha kuliko kumtumikia Mungu hii ikoje?
Bruno: Waimbaji walio wengi wamegeuza Injili kama kichaka cha kujifichia na wengi wao hawafanyi kazi ya Mungu ila wanafanya kazi na Mungu. Mimi najitambua kuwa nimeitwa kumtumikia Mungu na siyo vinginevyo.
Hata hivyo, jamii haina sababu kuwatupia waimbaji lawama nyingi kwa kuhisi kuwa wanapenda fedha kwani aina yetu ya muziki inahitaji fedha nyingi kufanya vizuri katika maandalizi na uandaaji wa kazi zetu ili kuleta ladha nzuri.
Mwandishi: Tofauti na zamani siku hizi kumekuwa na mchango mkubwa kati ya waimbaji wenye majina na katika kuwasaidia chipukizi waweze kutimiza ndoto zao, hili unalionaje?
Bruno: Siamini kama hayo mambo yapo ingawa inawezekana, lakini mtu kumsaidia chipukizi ni uamuzi wake hasa kama ana muda wa kufanya hivyo na hata hivyo. Tatizo chipukizi wamekuwa na nia ya kuimba na wasanii wakubwa siyo kwa lengo la kumuimbia Mungu bali kujipatia umaarufu na majina jambo ambalo kihuduma siyo zuri.Mimi kumekuwa na baadhi ya wasanii walio na majina makubwa wamekuwa na msaada sana kwangu na wamenipa mchango mkubwa kufika hapa kama Upendo Nkone, Martha Baraka, Emmanuel Mgaya (Masanja mkandamizaji) na wengine wengi.
Mwandishi: Unauzungumziaje mchango wa tasnia hii ya uimbaji nyimbo za injili katika kutoa ajira nchini?
Bruno: Ni jambo zuri kwa kuwa vipaji vinatoka kwa Mungu kwa maana hiyo ni ajira halali isipokuwa tu hutakiwi kutoka nje ya maagizo yake.
Pia inatakiwa waimbaji wa nyimbo za injili kuhakikisha wanaishi maisha matakatifu na ya kumpendeza Mungu. Wasiishi tofauti na wanachokiimba ili watu waige maisha yao na kumrudia Muumba wao kupitia wao na nyimbo zao.