Chanzo, tiba msongo wa mawazo kazini - 1
Huu ni msongo wa mawazo kwa watu walio kazini. Kwa kawaida, husababishwa na mazingira ya kazi, uzito wa kazi na uwezo wa mtu kuimudu kazi.
Mambo haya yote huunda mazingira yanayoweza kumweka mwajiriwa kwenye hatari ya kupata msongo wa mawazo.
Mambo mengine yanayochangia msongo wa mawazo kwa wafanyakazi ni nafasi ya mwajiriwa katika ofisi, uhusiano kati ya waajiriwa na muundo wa kiutendaji wa ofisi.
Msongo ukiwa juu sana au chini sana, unaweza kusababisha matatizo mbalimbali, ikiwemo magonjwa na udhaifu wa mwilin pia kiwango cha chini unaweza kutokea pale mwajiriwa anapohisi kuwa kazi yake haina thamani au umuhimu, hivyo anaweza kufukuzwa kazi na nafasi yake kujazwa na mtu mwingine wakati wowote.
Msongo wa mawazo wa kiwango cha juu unatokana na majukumu mengi ya kuchosha na wakati mwingine usimamizi mkali kuhakikisha hakuna makosa yanayotokea.
Katika hali zote mbili, mfanyakazi anakuwa katika mazingira ya kupata msongo wa mawazo unaoweza kumsababishia magonjwa na udhaifu.
Vyanzo vya msongo wa mawazo vinaweza kugawanywa katika makundi mawili: vyanzo vya ndani na vyanzo vya nje. Vyanzo vya ndani hutokana na mambo yanayohusiana na tabia ya mtu, kama vile uwezo wa mtu kushughulikia majukumu mazito, kujiamini, na wasiwasi juu ya kazi.
Vyanzo vya nje ni mambo yanayotokea nje ya eneo la kazi, kama matatizo ya kifamilia, changamoto za kiuchumi, na mazingira ya maisha kwa ujumla. Vyanzo hivi vyote vinaweza kusababisha dalili za matatizo ya afya, ambayo yanaweza kuongezeka na kuwa magonjwa kamili.
Hata hivyo, vyanzo hivi vya msongo wa mawazo hutofautiana kati ya mtu na mtu, aina ya kazi, na hali ya maisha ya watu. Kwa mfano, matatizo ya kifamilia na changamoto za kiuchumi hutofautiana na hivyo kuathiri aina na madhara ya msongo wa mawazo kwa mfanyakazi.
Tukiangalia kwa undani msongo wa mawazo kazini, unaweza kuwa katika aina zifuatazo:
Msongo Unaotokana na kazi yenyewe
Huu ni msongo wa mawazo unaosababishwa na hali ya kazi yenyewe. Mfano, mazingira ya kazi yanapokuwa magumu au yasiyofaa, mzigo wa kazi unapozidi uwezo wa mtu, au muda unakuwa mchache kulinganisha na wingi wa kazi.
Aidha, msongo huu unaweza kusababishwa na hatari zinazohusiana na kazi, hasa kwa wanaofanya kazi za mikono katika viwanda au maeneo hatarishi ambapo kuna uwezekano wa kuumia au hata kufa.
Msongo unaotokana na nafasi ya mtu kazini
Msongo huu unatokana na nafasi ya mtu ndani ya ofisi na majukumu yanayohusiana nayo.
Ugumu unaweza kuletwa na mgongano wa majukumu, au wafanyakazi wanapopandishwa cheo na kukuta mzigo wa kazi umeongezeka. Pia, wafanyakazi wanapokuwa katika nafasi moja kwa muda mrefu huku wenzao wakipandishwa madaraja, hii inaweza kusababisha msongo wa mawazo.
Hii ni kwa sababu kupandishwa daraja kazini kunatarajiwa kuonyesha kuthaminiwa kwa kazi na kuboresha hali ya kiuchumi. Kukosa fursa hizi kunaweza kusababisha mfanyakazi kuwa na msongo wa mawazo.
Msongo unaotokana na mahusiano kazini
Msongo huu unatokana na mahusiano duni kati ya wafanyakazi, au kati ya mwajiri na wafanyakazi.
Mfanyakazi anapokuwa na uhusiano mbaya na mkuu wake, walio chini yake, au wenzake, anaweza kuhisi kutengwa au kubaguliwa. Pia, mgawanyo usio sawa wa majukumu unaweza kusababisha msongo wakati baadhi ya wafanyakazi wanahisi wamepewa kazi nyingi au kazi zinazodai ufanisi mkubwa.
Unaotokana na muundo wa ofisi
Msongo huu unatokea pale ambapo mfanyakazi hana ushiriki wa kutosha katika maamuzi ya ofisi, hasa maamuzi yanayomgusa moja kwa moja. Pia, inapotokea kwamba mfanyakazi anakosa uhuru katika kufanya kazi zake, au anafuatiliwa kwa karibu katika kila jambo analofanya, hii huweza kuleta msongo. Kukosekana kwa ushauri wa kutosha kuhusu kazi za kila siku pia ni sababu.
Kwa ujumla, mambo haya yote huchangia kusababisha hali ya wasiwasi kazini, kutojiamini, na kushindwa kuvumilia changamoto za kazi. Dalili za hali hii ni pamoja na mapigo ya moyo kuongezeka, ongezeko la kolestro mwilini, uvutaji sigara uliopitiliza, kujitenga, ulevi, na kutopenda kazi.
Msongo huu unaweza kumfanya mfanyakazi azungumzie mara kwa mara nia yake ya kuacha kazi na kujiunga na kampuni au ofisi nyingine. Ikiwa dalili hizi hazitashughulikiwa mapema, zinaweza kusababisha magonjwa ya moyo na magonjwa ya akili.
Itaendelea wiki ijayo.