Chumvi ni hatari, je unapaswa kula kiasi gani?
Chumvi hutumiwa kila siku na wanadamu katika vyakula, lakini pale inapotumika kwa wingi inaweza kuleta madhara ya kiafya.
Chumvi inapokosekana katika baadhi ya vyakula huvifanya kukosa ladha nzuri hivyo ni vigumu kuacha matumizi ya chumvi.
Uwepo wa kiambata cha sodium katika chumvi ndiyo sababu ya wataalamu wa afya kuonya juu ya matumizi makubwa ya chumvi, hii ni kutokana kuongeza msukumo wa damu mwili.
Msukumo unapokuwa juu kupita kiasi ni kihatarishi cha kuweza kupata matatizo ya moyo na kiharusi (stroke).
Magonjwa haya mawili ndiyo chanzo cha vifo vingi katika nchi zenye uchumi wa kati mpaka mkubwa.
Vilevile ulaji wa chumvi nyingi unahusishwa na kutokea kwa magonjwa mengine ikiwa saratani ya mfuko wa chakula, udhaifu wa mifupa, unene na mawe katika figo.
Taasis kubwa za afya duniani ikiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO) zimekuwa zikitoa mapendekezo mbalimbali ya kiasi cha chumvi ambacho ni salama kiafya kutumia kwa siku.
Kiujumla duniani kote kiwango cha chumvi ambacho ni salama kinachopendekezwa kutumia kwa siku ni miligramu 1,500 ambacho ni karibia na nusu kijiko cha chai na isizidi miligramu 2,300.
Tafiti zinaonyesha kuwa kiwango hiki cha chumvi ni salama kwa matumizi na hakiambatani na upandaji mkubwa wa msukumo wa damu mwilini.
Inakadiriwa kiwango cha ulaji chumvi kwa watu waliowengi kwa siku ni miligramu 2,300-3,400 kwa siku ambacho ni sawa na kijiko kimoja cha chai mpaka na kimoja na nusu kwa siku.
Kiwango hichi ni hatari kiafya, ni vizuri kuchukua tahadhari mapema na kuanza kujidhibiti kutumia kiasi kikubwa cha chumvi hasa chumvi ya kuongeza mezani.
Kwa mazingira yetu ya Kitanzania, chumvi huliwa zaidi hasa wakati wa kula nyama choma, chipsi na vyakula vya migahawani au katika sherehe.
Katika mazingira haya watu wengi hutumia zaidi chumvi ya mezani na kuiongeza kiholela katika mlo wanaokula. Ni ngumu zaidi kukadiria kiasi cha chumvi kilicho salama kwa kutumia kichupa chenye tundu.
Mbinu ambayo ni rahisi ambayo inaweza kusaidia kupunguza utumiaji chumvi usio salama hasa ya mezani ni ile ya kuchukua chumvi kwa mtindo wa kufinya na dole gumba na kidole cha shahada.
Kiasi ulichofinya katika vidole hivyo ndiyo unatakiwa kula kwa mlo huo.
Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba, kudhibiti ulaji wa chumvi nyingi ni rahisi kuliko madhara yake ambayo ni vigumu kuyatibu yanajitokeza. Chukua tahadhari mapema tumia chumvi kwa kiasi.