HALIMA KINGU : Nguli wa upambaji anayeamini katika kujituma bila kuchoka
Halima Kingu.
Muktasari:
- Hata hivyo, ni wachache kati yao wenye utaalamu wa kutumia vipodozi kwani wengi wao hutumia wabunifu katika urembo kupamba nyuso zao na wakati mwingine kuwabunia mitindo ya nywele.
Matumizi ya vipodozi kwa mastaa ni miongoni mwa mambo yanayochangia mvuto na muonekano.
Hata hivyo, ni wachache kati yao wenye utaalamu wa kutumia vipodozi kwani wengi wao hutumia wabunifu katika urembo kupamba nyuso zao na wakati mwingine kuwabunia mitindo ya nywele.
Hapa nchini kuna vipaji lukuki vya wabunifu wa tasnia hiyo na miongoni mwao ni Halima Kingu.
Huyu ni mtaalamu wa urembo na mama wa watoto watano ambaye pia ni mkurugenzi wa Kampuni ya SMYNO Glam, ambaye hivi sasa anafanya kazi katika kituo cha televisheni TV 1 kama mpambaji.
Halima amekuwa akiwapamba watangazaji wote wa televisheni hiyo, lakini kubwa zaidi amekuwa akiwapamba mastaa na wasanii mbalimbali wanapofika kufanya mahojiano katika kituo hicho.
Wanaponogewa huwa wanamtafuta mwanamke huyo awapambe hata wanapotaka kwenda katika shughuli zao za kawaida.
“Ninafanya kazi na Vanessa Mdee, Mwasiti Almas, Feza Kessy, Judith Wambura (Jide), Mzee Yusuph, Mrisho Mpoto na mwanamitindo Ally Dax,” anafafanua.
Pamoja na kupamba mastaa mmoja mmoja, Halima pia amekuwa akifanya ya kuwapamba wanamitindo wanaoshiriki maonyesho mbalimbali.
“Nimewahi kuwapamba wanamitindo walioshiriki shindano la kusaka wanamitindo la Tausi Likokola na Peroni la Ally Remtulah, Swahili Fashion Week na mengine mengi,” anabainisha.
Nini siri ya mafanikio yake?
“Siri pekee ya mafanikio yangu ni kujituma. Hili ni suala la msingi kabisa katika kazi yeyote ile, kwani ukiangalia historia yangu utagundua ni kwa vipi juhudi zangu zimeweza kunifikisha hapa nilipo,” anaelezea huku akitabasamu. Tofauti na wataalamu wengine, Halima hakuwahi kuhudhuria shule ya urembo, lakini alijifunza kutoka kwa waliobobea kwenye fani hiyo.
Akizungumza kuhusu hilo anasema kuwa tangu akiwa mdogo amekuwa akivutiwa zaidi na mambo yanayohusu urembo hasa wa mwanamke.
“Urembo umekuwa sehemu ya maisha yangu tangu nikiwa mdogo. Nakumbuka wakati nikiwa na miaka mitano nilikuwa nikijua kusuka nywele, kadri siku zilivyokuwa zikienda nikawa napata kujifunza urembo mwingine hadi nikabobea,” anaeleza.
Baada ya kubobea katika shughuli hizo, Halima alitumia ujuzi wake kujiingizia kipato. Hata baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari aliona ni bora ajajiajiri kupitia fani hiyo ya urembo.
“Muda mfupi baada ya kumaliza elimu yangu ya sekondari niliona kuna haja ya kujiari hasa kwa kutokana na ujuzi nilio nao, lakini kabla ya hatua hiyo nilienda kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye saluni moja iliyopo Sinza, Mugabe.”
Anasema hapo alifanya kazi kwa muda kabla ya kujiajiri na kufungua saluni yake maeneo ya Upanga.
“Nikiwa upanga nilipiga hatua na hata kupamba maharusi, kwa kuwa ndoto yangu ilikuwa ni kuwa mpambaji mkubwa nimeendelea na kazi hiyo na sasa napamba watu wa kada mbalimbali,” anaelezea.
Hivi sasa anafanya kazi hiyo kwa ufanisi akitumia vipodozi kutoka Marekani.
“Kikubwa ninachozingatia ni ubora wa kazi, hili haliwezi kukamilika ikiwa nitatumia vipodozi visivyo na ubora,” anafafanua.
Kazi ya upambaji ina changamoto zake kama ziilivyo nyingine, akizungumza kuhusiana na hilo, Halima anabainisha kuwa changamoto kubwa inayomkabili katika utekelezaji wa majukumu yake ni pamoja na upatikanaji wa vipodozi halisi.
“Nalazimika kuagiza nje ya nchi kwa kuwa hivi vinavyopatikana hapa, vingi huwa ni feki.”
Mipango yake ya baadaye
“Kwanza kabisa najipanga kwenda shule kwa ajili ya kuongeza ujuzi zaidi katika kazi yangu, pili nina mpango wa kuendeleza vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupitia fani yangu hii ya upambaji,” anafafanua na kuongeza.
“Kikubwa ninachotaka kuwahusia kazi siyo lazima kuajiriwa, unaweza kujiajiri na kuendesha maisha yako kupita sanaa kama hii ya urembo.”
Pia, ana mpango wa kusajiri kampuni yake ya SMYNO Glam na kuipanua kufikia kuwa na matawi nchi nzima.
“Wito wangu kwa wanawake wenzangu ni kuwa yafanyie kazi mawazo yako ukijiamini unaweza basi utaweza kweli. La nyongeza wanawake tupendane na tusaidiane usimcheke mwenzio kwa matatizo yake msaidie,”anahitimisha.
Usilolijua kuhusu Halima
Alizaliwa mwaka 1976 katika Kijiji cha Kidudwe wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro.
Ni mtoto wa tano katika familia ya watoto nane.
Ana watoto watano ambao ni Sabrina, Muharram,Yassir, Nahya na Omary (SMYNO)
Kifupisho chake ndio jina la kampuni yake.
Ndoto yake ilikuwa ni kuwa daktari, lakini mapenzi yake juu ya vipodozi yaliibadilisha.