Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kizazi cha kidijitali: Tunawakuza au tunawapoteza

Muktasari:

  • Tayari kuna mijadala imeshaibuliwa na inaendelea kujadiliwa ikihoji, teknolojia ni rafiki au adui kwa watoto.

Dar es Salaam. Katika dunia ya leo ya kidigitali, teknolojia imekuwa sehemu muhimu kwa maisha ya kila siku. Watoto wanazaliwa wakiwa na uwezo wa kutumia vifaa vya kidigitali kama vile simu janja, kompyuta na televisheni za kisasa kabla hata ya kujua kusoma au kuandika.

Hali hii inaleta changamoto kubwa kwa wazazi na walezi katika kuhakikisha kwamba, watoto wanatumia teknolojia kwa njia salama yenye manufaa na inayowakuza kiubunifu bila kuathiri maadili, afya ya akili na makuzi yao katika kijamii.

Nasema hivyo kwa sababu tayari kuna mijadala imeshaibuliwa na inaendelea kujadiliwa ikihoji, teknolojia ni rafiki au adui kwa watoto.

Kwa upande mmoja, binafsi naweza kusema kwamba teknolojia inaweza kuwa nyenzo nzuri ya elimu na ubunifu kwa mtoto.

Kwa sababu zipo programu nyingi za kielimu zinazowasaidia watoto kujifunza kusoma, kuandika, hesabu na hata maarifa ya sayansi kwa njia ya kuvutia.

Pia watoto wanaweza kutumia teknolojia kubuni michezo yao wenyewe, kuchora, kutengeneza muziki au hata kujifunza lugha mpya.

John Mdemi mtaalamu wa malezi anasema pia haya  yote huchangia kukuza ubunifu, fikra hna ustadi wa karne ya 21 ambao ni muhimu kwa maisha ya baadaye kwa mtoto.

Hata hivyo, upande wa pili wa sarafu unaonyesha picha tofauti. Watoto wengi wanatumia muda mwingi kwenye skrini kuliko inavyopendekezwa na wataalamu wa afya.

Daktari wa watoto, Sara Ruhabangila anasema kutazama vipindi visivyo na maadili vinaweza kumfanya mtoto akaiga tabia za kikatili au kutumia mitandao ya kijamii kabla ya umri unaofaa, kunaweza kuathiri maendeleo ya watoto.

Zaidi ya hayo, wataalamu wanasema matumizi makubwa ya teknolojia yanayopita kiasi, yanaweza kuhatarisha uhusiano kati baba, mama na watoto.

Na yanaweza pia yakamfanya mtoto awe anakosa usingizi na kujikuta anashuka kitaaluma.

Lakina kuna njia nzuri inayoweza kuwasaidia watoto kukua vizuri,  ambayo ni ile ya kuweka mipaka ya matumizi ya teknolojia.

Changamoto kuu kwa wazazi ni kuweka mipaka sahihi bila kuzuia ubunifu wa watoto. Mipaka haipaswi kuwa ya kukandamiza, bali ya kuelekeza.

Watoto wanahitaji mwongozo wa kutumia teknolojia kwa njia sahihi na si kuachwa wajifunze kwa kufanya  kama majaribio na makosa ambayo yanaweza kuwa na madhara makubwa kwao.

Niliwahi kuambiwa kwamba, ili kulitekeleza hilo, kwanza wazazi wanapaswa kuweka muda maalum wa matumizi ya vifaa vya kidigitali kulingana na umri wa mtoto.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza watoto wa chini ya miaka mitano wasitumie TV kwa zaidi ya saa moja kwa siku na watoto wadogo zaidi wasitumie kabisa.

WHO inasema hiyo husaidia kuzuia utegemezi wa teknolojia na kuwapa nafasi watoto ya kushiriki katika michezo ya kawaida na ya kijamii ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa ubongo.

Pili, wazazi wanapaswa kuchagua maudhui yanayofaa. Programu na vipindi vya kidigitali vinapaswa kuwa vya kielimu, vya kuburudisha kwa kiasi na visivyokiuka maadili.

Kuna majukwaa mengi yenye maudhui salama kwa watoto, lakini ni jukumu la mzazi au mlezi kuhakikisha kwamba mtoto anapata maudhui yanayomfaa.

Tatu, wazazi wanapaswa kuwa mfano bora. Tukumbuke kuwa watoto hujifunza kwa kuiga. Ikiwa mzazi hutumia muda mwingi kwenye simu au televisheni, basi ni vigumu kumwambia mtoto apunguze muda wake wa kutazama TV.

Bali wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto kutumia muda wao mwingi kufanya mambo ambayo hayahusishi masuala ya teknolojia kama vile kula pamoja au kucheza pamoja michezo ya jadi ambayo inasaidia kujenga mawasiliano bora na mafungamano ya kiroho na kihisia kati ya wazazi na watoto.

Lakini tukumbuke kwamba kuweka mipaka hakumaanishi kumzuia mtoto kutumia teknolojia kabisa.

Bali lengo ni kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanamjenga mtoto na si kumharibu. Watoto wanaweza kupewa nafasi ya kutumia programu za kubuni, kama za kuchora, kuandika hadithi au kutengeneza muziki. Aidha, wanaweza kuhamasishwa kushiriki mashindano ya kidigitali yakiwamo yale ya mashindano ya ubunifu na mafunzo mbalimbali.

Zaidi ya hayo, walimu na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana na wazazi katika kukuza matumizi bora ya teknolojia kwa watoto.

Hii itasaidia pia kutoa elimu sahihi kwa watoto kuhusu usalama mtandaoni, kuwafundisha kuwa na nidhamu ya kidigitali na kuwaelekeza jinsi ya kutumia maarifa ya kidigitali kutatua matatizo ya maisha.