Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madhara ya kuwazuia watoto kuonesha hisia hasi

Muktasari:

  • Kwa kizazi tulichonacho sasa, jukumu la baba ni pamoja na kuweka mazingira salama na rafiki kwa familia kuonesha hisia hata zile tunazozionea aibu.



Morogoro. Bila shaka umeshawahi kusikia maelezo kuwa wanaume hawaongozwi na hisia. Tunaambiwa, ‘nature’ ndio inayowafanya wanaume wawe watu wanaoongozwa na akili zaidi kuliko hisia. Ukiyachunguza madai haya, kwa hakika, unagundua jaribio la jamii kudogosha hisia na kuzifanya ziwe kama aina nyingine ya udhaifu.

Maelezo haya ya ‘nature’ ya wanaume kuongozwa na akili, aghalabu, humaanisha uwezo wa mwanaume kufikiri kwa kina kabla hajachukua uamuzi na kwamba, kwa kawaida, huwa hana tabia ya kuzipa hisia nafasi anapofikiria jambo.

Tatizo la madai haya ni kule kuonesha kuwa mwanamke kwa asili yake huwa hatumii akili na kwamba uamuzi mwingi anaofanya huwa anakurupuka na hashirikishi tafakari ya kina.

Ukiachana na utitiri wa mazungumzo haya tunayoyasikia mtaani, nimewahi pia kusoma kitabu maarufu cha John Gray, mwandishi wa Kimarekani, aliyejaribu kutoa maelezo yanayoonesha tofauti za kijinsia baina ya wanaume na wanawake.

Ingawa ni kweli tofauti hizo za kitabia zipo, kama ambavyo tunatofautiana kimaumbile, bado madai haya ya Gray hayana ushahidi wowote wenye nguvu ya kisayansi kuonesha kuwa kila tofauti unayoiona baina ya wanaume na wanawake basi ni ‘nature’.

Kwa mfano, ukiangalia tafiti nyingi zinazochunguza ukuaji wa hisia unagundua kuwa utotoni, wavulana na wasichana hawatofautiani sana linapokuja suala la kuonesha hisia.

Wote, tafiti zinasema, hawaogopi kulia hadharani wanapodai kitu, wanapohisi kutokutendewa haki au wanapoumizwa.  Ukiwachunguza watoto unagundua wa kiume mwenye miaka minne hana tofauti ya msingi na wa kike wa miaka hiyo hiyo.

Hawa wote, kwa mfano, hawajizuii kuonesha huzuni wanaponyimwa kile wanachokihitaji, hawajizuii kuonesha wasiwasi wanapokabiliana na ugumu na kadhalika na kadhalika.
Lakini kadri wanavyokua, hatimaye tofauti za kijinsia huanza kujitokeza. Jamii huwafundisha watoto wa kiume kukana baadhi ya hisia zao na kujipambanua na hisia fulani. Kulia inakuwa jambo la fedheha kwa mtoto wa kiume. Kuonesha woga inakuwa jambo la jinai.

Lakini wakati huo huo jamii inamfundisha kujisikia fahari kwa kuwa hasira. Haishangazi, kwa mfano, mwanaume mtu mzima kuonesha hasira, na hata ghadhabu na hata asijisikie kufedheka.

Jamii imemfundisha kuwa hasira ni hisia sahihi kuonesha lakini sio woga, hatia na hisia nyingine ngumu. Ukikutana na mwanaume anayeonesha waziwazi hisia za ufahari wa kufanya kitu kizuri, kutambia hisia za tamaa za ngono hadharani na hata kujisifia kwa kuumiza na kuonea watu inaonekana ni jambo la kawaida.
Wakati mwanaume anafundishwa kuzuia ‘hisia za kike’ kama woga na aibu, jamii imemruhusu mwanamke kuogopa, kuhuzunika, kufedheheka na hata kulia hadharani. Hisia za ‘kiume’ kama hasira na ghadhabu ambazo mwanaume anaruhusiwa kuzionesha, jamii imemwaminisha mwanamke kuwa ni kosa (udhaifu) kuzionesha hisia hizo.

Katika baadhi ya jamii zetu, tunazo hadi sheria zisizo za wazi zinazomwaminisha mwanaume kuwa hata kuonesha uso wenye furaha moja kwa moja, kuonesha hisia za upendo waziwazi ni udhaifu. 
Huo ni mfano moja wapo wa namna mapokeo yanavyochangia kutengeneza ‘nature’ ya hisia na kuzigawanya katika makundi ya kiume na kike. Kile kinachoitwa wanawake hawana ‘nature’ ya kukasirika, kimsingi kinamaanisha mazingira ya kimalezi yanayomwaminisha mwanamke kuwa kukasirika ni jambo la fedheha.

Kile kinachoitwa wanaume huwa hawaogopi, kinamaanisha mazingira ya kimalezi yanayomwaminisha mwanamume kuwa kuogopa ni jambo la aibu. Kwa hiyo, ‘nature’ kwa hakika ni mkusanyiko wa matarajio mengi yanayolenga kumtofautisha mwanaume na mwanamke.

Huenda unajiuliza, kwani kuwatofautisha watoto kijinsia kuna tatizo gani kama lengo ni kuwaandaa kukabiliana na majukumu yanayoendana na jinsia zao? Kuna shida gani kumkomaza mwanaume awe imara? Kuna ubaya gani mwanaume kuficha baadhi ya hisia zake?

Tatizo ni hili. Mwanaume anaponyang’anywa uhuru wa kuonesha hisia fulani fulani, kwa kiasi kikubwa, anaathiri afya yake. Hisia kama fedheha, huzuni, sonona na kadhalika, hazipaswi kumezwa. Unapokuwa na uhuru wa kuzionesha unaipa nafsi yako fursa ya kupumua na hivyo kujipunguzia magonjwa mengi yasiyoambukizwa.

Kadhalika, kuficha hisia kunaathiri namna wanaume wanavyoshiriki malezi. Utimamu wa kihisia kwa watoto wetu, kwa kiasi kikubwa, unategemea uwezo wa wazazi kuwaruhusu kuonesha hisia zao bila kujificha.

Watoto, mathalani, wanatamani baba yao awaambie anawapenda, anawathamini na kwamba ni salama kwao kuonesha hisia hasa zile zinazoweza kumtafuna mtu ndani kwa ndani.

Kwa msingi huo, baba kuonesha hisia kwa familia yake haiwezi kuwa udhaifu. Muhimu ni namna nzuri ya kuonesha na kurekebu hisia hizo. Kwa kizazi tulichonacho sasa, jukumu la baba ni pamoja na kuweka mazingira salama na rafiki kwa familia kuonesha hisia hata zile tunazozionea aibu.