Mzoeshe mwanao ulaji wa chakula bora
Hakikisha mwanao anakula kwa mpangilio. Unashauriwa pia kumfundisha jinsi ya kunywa maji na umuhimu wake kiafya. Ikiwa haya yote yatafanyika ni wazi kuwa atakuwa na tabia ya kula chakula bora, tena chenye virutubisho muhimu kiafya.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
Hapa Tanzania tumeshuhudia maradhi kadhaa kwa watoto yanayosababishwa na ulaji mbovu. Mara nyingi matatizo huwa ni mchanganyiko wa chakula.
Katika pitapita zangu nilifanikiwa kukutana na chapisho moja la kitabu maarufu kilichoandikwa na Daktari Bingwa wa Watoto kutoka nchini Marekani.
Jina la kitabu hicho ni Raising Baby Green kilichoandikwa na Dk Alan Greene kutoka kliniki ya Chuo Kikuu cha Stanford Marekani.
Anasema kuwa kila siku anapoangalia orodha ya watu wa kukutana nao, hukutana na watoto wanye matatizo yaliyosababishwa na matokeo ya ulaji wa wa chakula kingi, vyakula visivyokuwa na virutubisho sahihi kiafya, vyenye sukari, pia ukosefu wa mbogamboga.
Mara nyingi matatizo hayo hutengenezwa taratibu, hivyo mzazi bila kuelewa huwa ndiyo mrutubishaji wa matatizo hayo na mwishowe mtoto hupatwa ugonjwa unaohatarisha maisha yake.
Miongoni mwa magonjwa hayo ni kisukari, magonjwa ya moyo na mengine yanayofanana na hayo. Ukiangalia chanzo cha magonjwa hayo, utagundua kuwa ulaji mbovu unasababishwa na mtindo mbaya wa maisha.
Katika kupambana na matatizo hayo, daktari huyu alitoa mapendekezo kwa shule kufundisha lishe kama ilivyo kwa masomo mengine ya hisabati na sayansi.
Pia aliwataka wazazi kuwafundisha watoto aina bora na kiasi sahihi cha chakula kama wanavyowafundisha kuwa na tabia njema.
Hapa Tanzania tumeshuhudia maradhi kadhaa kwa watoto yanayosababishwa na ulaji mbovu. Mara nyingi matatizo huwa ni mchanganyiko wa chakula.
Kuna wale wenye matatizo yanayosababishwa na ulaji wa chakula usiokuwa na mpangilio, lakini pia wapo wanaokula chakula chenye upungufu wa virutubisho.
Matokeo ya hali hiyo tumeshuhudia watoto wetu wakipata matatizo ya utapiamlo, wengine wakidumaa na wapo pia wanaopata maradhi yanayosababishwa na unene uliopitiliza.
Zifuatazo ni baadhi ya njia zilizopendekezwa na wataalamu kupambana na tatizo hili:-
Jifunze virutubisho muhimu
Jifunze aina za virutubisho muhimu za vyakula vinavyotakiwa katika afya ya mtoto. Jenga mazoea ya kujua chakula cha anachokula siyo kwa jina lake, bali kwa virutubisho vilivyomo ndani yake. Kwa kufanya hivyo, mwanao atajifunza taratibu vyakula anavyotakiwa kula, huku akiviweka pembeni vile visivyokuwa na virutubisho muhimu kwa afya yake.
Mpe mwanao matunda mbalimbali
Hakikisha unamhamasisha mwanao kula matunda ya rangi mbalimbali. Kwa kuwa rangi za matunda nazo zina umuhimu kiafya. Ni vyema kumjengea mwanao utaratibu wa kula kila tunda.
Kwa mfano matunda yenye rangi ya njano yanatajwa kuwa na vitamin B kwa wingi, huku matunda yenye rangi ya kijani yanatajwa kuwa na Vitamini C kwa wingi. Kwa kuwa vitamin hivi ni muhumu katika ustawi wa afya ya mtoto wako ni vyema ukamhamasisha kula matunda ya aina zote kwa matokeo mazuri.
Hakikisha unasoma na kujua kila chakula kinacholiwa na mtoto wako
Mzazi unahusika moja kwa moja kujua kinacholiwa na mtoto wako.
Soma vitu vilivyomo kwenye chakula, hasa vile vya kutengenezwa viwandani. Kama unahisi kuna virutubisho visivyo sahihi mwepushe mwanao kwani siyo lazima ale kila anachokiona.
Mfundishe utaratibu wa kula
Hakikisha mwanao anakula kwa mpangilio. Unashauriwa pia kumfundisha jinsi ya kunywa maji na umuhimu wake kiafya. Ikiwa haya yote yatafanyika ni wazi kuwa atakuwa na tabia ya kula chakula bora, tena chenye virutubisho muhimu kiafya.
Zingatia umri katika mpangilio wa chakula
Katika umri mdogo, mtoto hupata nafasi ya kukua na kujenga misuli na mifupa yake. Ujenzi huo wa viungo vya mtoto hutengemea zaidi vyakula anavyokula. Ni muhimu kwa mzazi kuhakikisha mwanao anajenga mazoea ya kula vya kula vyenye kazi ya kujenga misuli na mifupa yake pia. Hii itamweka katika nafasi nzuri ya kukua kiafya.
Tuonane wiki ijayo!