Prime
Namna za kuijenga ndoa yako-2
Wiki iliyopita katika makala haya tulianza kuangalia kanuni rahisi za kukusaidia kuijenga ndoa yako. Makala iliyopita ilizitaja kanuni tano, wiki hii tunamalizia kuziangalia kanuni nyingine tano.
Kanuni ya kwanza epuka kumkosoa au kumrekebisha mwenza wako hadharani
Jitahidi usimkosoe au kumrekebisha mume au mke wako mnapokuwa katikati ya watu wengine, labda kiwe ni kitu chenye umuhimu mkubwa sana ambacho hakiwezi kusubiri.
Mara nyingine unakimbilia kumrekebisha kwenye kitu ambacho wala hakuna anayejali marekebisho hayo au marekebisho hayo hayamfaidishi yeyote kwenye hao waliopo, sasa kama ni hivi, unamrekebisha ili iwe nini?
Kwa taarifa yako, watu uliokuwa nao hawatokumbuka kile alichokuwa anazungumza mwenza wako ambacho ulihisi amekosea, ila watakumbuka ulivyokuwa unamkosoa na kumrekebisha bila busara.
Wakati mwingine hata mnapokuwa peke yenu usikimbilie kumkosoa au kumrekebisha hata kama unafahamu kuwa hata yeye unayemrekebisha ataelewa na kukubali marekebisho hayo. Kumbuka mara nyingi taarifa mnazokosoana au kurekebishana sio za muhimu sana, bali ule uhusiano wenu.
Shirikini na shirikishaneni katika imani yenu
Najua unaweza kutamani kufahamu nini kinaweza kupunguza kiwango cha kuvunjika kwa ndoa.
Najua utakubaliana na mimi kwamba idadi ya wanandoa kutengana inaongezeka kwa kasi tofauti na miaka ya nyuma. Na bahati mbaya wengi wao siku hizi wanatengana miaka ya mwanzoni ya ndoa zao.
Utafiti uliofanywa na Dk Greg Smalley unaonyesha wanandoa ambao wana imani, wanashiriki na kushirikishana mambo ya imani zao kama vile kusali wao pamoja na familia zao, wamepunguza nafasi za kutengana kwa kiwango cha ndoa moja kati ya ndoa 1,000.
Hiki ni kiwango kikubwa kupungua kwa nafasi za kutengana.
Kule kushirikiana katika mambo ya imani yenu kunawaleta karibu sio tu kimwili, bali kihisia na kiroho pia. Yamkini hamjawahi kufanya hivi na unashangaa nitaanzaje, anza taratibu kama vile unafanya mazoezi, pateni muda wa kuzungumza mambo ya imani yenu, kutafakari neno la Mungu pamoja, tafakarini uhalisi wa yasemwayo humo mkihusisha ndoa na familia yenu.
Kama imani yenu inaruhusu mtu na mwenza wake kusali pamoja, fanyeni hivyo na kama hairuhusu, peaneni mambo ya kumshirikisha Mungu halafu kila mmoja awe na muda mzuri wa mapatano, yaweza ikawa mwilini hamjakaa pamoja ila rohoni mkawa na nia moja.
Zungumza lugha ya jinsia ya mwenza wako. Ukichunguza kwa makini, utagundua ziko dini au imani zaidi ya tisa pamoja na jamii kadhaa ulimwenguni zinazosisitiza kila mwanamume kumpenda kwa dhati mke wake na kila mwanamke kumheshimu mume wake.
Dhana hii imelalamikiwa na wanaharakati wengi, ingawa bado uhalisia wake umesimama pale pale.
Kama wewe ni mume wa mtu, jifunze kumpenda na kuzungumzia mvuto wa mapenzi kwa mkeo. Liweke hili likae akilini mwako na usilisahau.
Hiki ndicho anachokihitaji mkeo zaidi ya vingine vyote.
Kama wewe ni mpenda kusoma vitabu, kitabu mahiri hili kinachokufaa kinaitwa; “Love and Respect” cha Emerson Eggerichs.
Ufahamu ufunguo wa moyo wa mpenzi wako
Ufunguo muhimu zaidi kwenye moyo wa mwanamke ni kumhakikishia ulinzi na usalama wake.
Endapo mwanamume ataweza kumhakikishia mke wake kila wakati kwamba ndiye aliyesimama namba moja hana mpinzani, basi mwanamume huyu atakuwa amemgusa mke wake sehemu muhimu sana moyoni mwake. Hii ndiyo kiu ya kila mwanamke.
Ufunguo muhimu zaidi kuliko yote kwenye moyo wa mwanamume ni mafanikio.
Endapo mwanamke anaweza kumwangalia mume wake na kumwambia “ninayaona mafanikio ndani yako”, “ninayaona mafanikio tele ya familia yetu kupitia wewe”, “wewe ni mtu shupavu, mtu wa maana sana” na maneno mengine ya kuinyanyua roho na nafsi yake, basi atakuwa ameligusa hitaji la msingi sana la mume wake.
Kanuni hizi zimeelezwa kwa kina kwenye kitabu cha Bill na Pam Farrel kiitwacho The Marriage Code: Discovering Your Own Secret Language of Love.
Jizoesheni na ongezeni kutumia lugha za vichocheo vya mapenzi
Daktari na mtaalamu wa mambo ya ndoa, John Gottman hufanya tafiti nyingi kwenye ndoa. Kati ya tafiti hizo zipo alizotumia muda mrefu kuangalia wanandoa wanazungumza nini mara kwa mara.
Mwanzoni alidhani wanandoa wengi wanazungumzia ndoa zao na mambo yanayowahusu.
Alidhani wanandoa wana lugha za kuamsha mapenzi na hamasa zao za kila siku juu ya uhusiano wao, lakini alichokikuta kilikuwa tofauti na alichokuwa akifikiria.
Dk Gottman aligundua wanandoa wengi huzungumza vitu ambavyo havina mchango wowote kwenye maisha yao ya ndoa, vitu ambavyo haviongezi hamasa yoyote kwenye mapenzi yao. Kwa mfano; wapo waliozungumza mambo ya mikopo waliyonayo, mambo ya kazini na changamoto zake, mambo ya marafiki zao, mambo ya miradi yao na ni wachache sana walizungumza juu ya hisia zao, wanavyowaza juu yao.
Lugha hizi zinazochochea mapenzi zaweza kuwa za maneno au hata lugha ya mwili.
Hapa lazima kuwe na uwezo wa mpenzi mmoja kufahamu nini mwenzake anamaanisha kwa kufanya anachofanya.
Inaweza pia kuwa ni mguso au kumgusa mwenzako na kutegemea mrejesho wa namna alivyojihisi baada ya mguso huo.
Inafurahisha zaidi kama lugha hizi zinatolewa na kupokelewa na wote wawili, hapa namaanisha, mnabadilishana lugha hizi, na sio mmoja ndio anatoa alama au hisia hizi tu na mwingine yeye ni kupokea tu.
Kwa kupokea na kufurahia vielelezo au vialama hivi kutoka kwa mpenzi wako unaendeleza na kuliboresha penzi lenu au ndoa yenu na kwa kukataa au kudharau kile mwenzako anachokugusia au kukuitia unaharibu na kupunguza ladha ya mahusiano yenu.
Kamwe usidhani vinavyoharibu au kuyaporomosha mahusiano ni vitu vikubwa sana, bali ni vitu vidogovidogo.
Vivyo hivyo, ukweli ni huohuo kwenye vitu vinavyoyajenga mahusiano.