Profesa Ester Mwaikambo : Mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Daktari bingwa
Muktasari:
- Katika safari ya kukamilisha lengo hilo aliweza kuwa mwanamke kwanza Tanzania kuwa Daktari Bingwa akibobea kwenye magonjwa ya watoto, huku pia akiwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania(Mewata) .
Kuna wanawake wengi waliolitumikia vizuri taifa hili kwa nafasi mbalimbali ikiwamo harakati za kupigania uhuru, hata za kuliletea maendeleo.
Profesa Ester Mwaikambo ni mmoja wa wanawake hao ambao wamekuwa wakihusika kwa kiwango kikubwa kwenye harakati mbalimbali za kuletea mapinduzi ya kijamii kwa mwanamke na taifa la Tanzania kwa jumla.
Kwa maelezo yake, Profesa Ester Mwaikambo anasema kuwa tangu awali lengo lake limekuwa ni kuleta ukombozi na kuondoa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanawake nchini.
Katika safari ya kukamilisha lengo hilo aliweza kuwa mwanamke kwanza Tanzania kuwa Daktari Bingwa akibobea kwenye magonjwa ya watoto, huku pia akiwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania(Mewata) .
Mwaka 2004, mwanamke huyo alikuwa mmoja kati ya waanzilishi wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Wanataaluma wa Sayansi na Teknolojia.Taasisi hiyo ambayo yeye ni makamu mwenyekiti, inajumuisha watalaamu mbalimbali waliobobea katika taaluma za sayansi na teknolojia.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili, Profesa Mwaikambo anasema kuwa kupitia taasisi hiyo, wamekuwa wakishughulika na uandaaji wa mapendekezo mbadala katika sera mbalimbali kuhusu tasnia hizo.
“Tunafanya tafiti na kuandaa mapendekezo tunayoyawasilisha katika wizara husika. Siyo kwa serikalini tu bali hata sekta binafsi, bila malipo yoyote,”anasema Profesa Mwaikambo.
Mbali na kutotambuliwa kama chombo cha kiserikali, lakini taasisi hiyo imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka serikalini kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia. “hii ni kwa sababu ni NGO’s ila tunafanya utaratibu wa kuitambulisha rasmi kama chater serikalini,”anasema Profesa Mwaikambo.
Anaongeza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikijikita zaidi katika utafiti wa kuangalia mbinu za kuishauri Serikali njia mbadala zinazoweza kurahisisha ufundishaji wa masomo ya sayansi hasa kwa mtoto wa kike.
“Mtoto wa kike ashawishike kupenda somo la sayansi, kwa mfano kuna kitabu tumeshaandika na baadhi ya maprofesa ambacho kinazungumzia ushawishi wa kupenda somo hilo. Lakini ukiangalia kiuhalisia changamoto ipo bado kubwa serikalini tu,” anasema Profesa Mwaikambo.
Majukumu mengine
Kwa kipindi cha miaka 20 sasa, Profesa Mwaikambo amekuwa akifanya kazi za utafiti na vyuo vikuu vya Utah, Salt lake, Noth Carolina, Duke Medical University na Manzies School of Research.
Mbali na hilo, pia ni makamu mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Hubert Kairuki cha jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Kikuu cha Tumaini Tanzania. Hadi sasa amekuwa ni mwalimu wa madaktari wanaosomea udaktari bingwa baadhi ya vituo vikiwa Hospitali ya Mwananyamala na Ilala. Profesa Mwaikambo anasema kuwa amewahi kutumia nafasi mbalimbali katika taasisi na mabaraza ikiwamo NECTA, IMTU, Tume ya Sayansi na Tecknolojia, pia Mwenyekiti wa MAT.
Katika mpangilio wa majukumu hayo, Profesa Mwaikambo anasema kuwa hapati changamoto kubwa ya kushiriki kutokana na mpangilio wa majukumu yake.
Tuzo zake
Hadi sasa Profesa Mwaikambo ameshatukiwa tuzo mbalimbali ikiwamo tuzo kubwa ya Harvad African Distinguish Lecturas Arwad kwa mwaka 2009. Mwaka 2008 tuzo hiyo ilichukuliwa na marehemu Chinua Achebe.
“Tuzo hiyo ni kubwa Afrika, hutolewa mara moja kila mwaka. Kabla kutunukiwa Chuo Kikuu cha Havard hupendekeza jina moja la Mwafrika aliyetoa mchango kwenye jamii na kupelekwa kwenda kozi ya mwaka mmoja,” anasema Profesa Mwaikambo.
Tunzo nyingine aliyopata ni ya martin Luther King katika mwaka 2012 ambayo hutolewa na Marekani ikiwa ni heshima ya utumishi uliotukuka katika jamii.
“Tunzo hiyo iaitwa Martin Luther King Drum Major for Justice Award, inatolewa kwa watumishi waliotambuliwa kutumika kwa kuzingatia haki za binadamu. Tuzo nyingine ni ya Women Archeavement (2009) inayotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini kupitia NIMR,”anasema Profesa Mwaikambo.
Historia yake
Profesa Mwaikambo ni mzaliwa wa Kijiji cha Mwika, Wilaya ya Moshi. Ni mwanamke mjane mwenye watoto watano, wawili wanaishi nchini Marekani na watatu wakiwa hapa Tanzania.
Mwanamke huyo husherehekea siku yake ya kuzaliwa kila inapofikia Desemba 12. Safari ya kufikia mafanikio yake ilianza kung’ara baada ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1962 ambapo Rais kwa wakati huo alitangaza nafasi za masomo kwa Watanzania wote waliohitaji kujiendeleza.
“Kabla ya uhuru nilikuwa na elimu ya cheti cha uuguzi niliyoipata katika Chuo cha Dar es Salaam Tecknology mwaka 1960, ndiyo nikapata nafasi ya kwenda kujiendeleza nchini Urusi mwaka 1962, ambako nilisoma miaka 7 na kupata shahada yangu ya kwanza,”anasema Profesa Mwaikambo.
Baada ya kupata Shahada ya Udaktari mwaka 1969, ameweza kufanikisha malengo yake kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya na elimu kwa mtoto wa kike hasa kuhusu somo la sayansi.