Salome Nyoni:Mke wa naibu waziri anayelilia maadili kwa wanawake

Muktasari:
Hata hivyo, anashauri: “Wanawake tukiwa na ushirika tutaweza kuelezana, tutumie misikiti na makanisa au vikundi turejeshe maadili ya mwanamke, na siyo kutoa lugha chafu barabarani.”
“Namshukuru Mungu na najivunia mchango wangu kwa taifa, kwani nimefundisha kwa miaka 42. Nimefundisha Kifaransa na maarifa ya nyumbani watoto wengi wa kike, hata wa kiume na baadhi wamerudi kuja kunishukuru kutokana na maendeleo waliyopata maishani,”
Ni sehemu ya maelezo ya mama Salome Nyoni aliye na umri wa miaka 64, mzaliwa wa Sali, Mahenge wilayani Ulanga katika Mkoa wa Morogoro.
Mwanamke huyo sasa amestaafu, lakini sasa anajishughulisha na ufugaji, kilimo cha uyoga kupitia kikundi na kutoa ushauri kwa wanawake wenzake kuhusu mambo mbalimbali ikiwamo malezi.
“Kwa sasa najishughulisha zaidi na ufugaji na kilimo, ninalima uyoga pia natumia muda wangu kwa kutoa semina na ushauri nasaha kwa jamii hasa wanawake wenzangu. Natoa ushauri pia kuhusu namna ya kutengeneza mbegu za uyoga. Hutoa pia mafunzo ya malezi nikitumia mfano wa maisha yangu kwa kutoa ushauri nasaha. Binafsi nilianza maisha na hata sasa naishi kwa kumtegemea Mungu,” anasema mama Nyoni na kuongeza:
“Ukisema mimi naweza, peke yako huwezi bila ya Mungu, niliyofanya kama kipofu Mungu amejibu. Wanawake tushirikiane na tumtumainie Mungu katika kila jambo.”
Anabainisha kuwa huendesha kilimo cha uyoga akiwa na kikundi kinachojulikana kama St Monica wakiwa wanawake 10 wakiwa miongoni mwa wanawake 288 katika mradi wa Uyoga Trust unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa (UN) katika Manispaa ya Morogoro.
Salome ambaye ni mama wa watoto saba akiwa na wajukuu 18 na kitukuu kimoja, alipata elimu yake katika Shule ya Msingi Sali aliposoma darasa la kwanza hadi la nne, Kwiro aliposoma darasa la tano hadi la saba kabla ya kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika Sekondari ya Mtakatifu Agnes mkoani Tabora mwaka 1955.
Hata hivyo, hakuweza kuendelea na masomo baada ya kuugua, badala yake alijiunga na Chuo cha Ualimu Mhonda katika mwaka 1956 na 1957, ambapo mwaka 1959 alianza kufundisha Shule ya Msingi Itete.
Mwaka mmoja baadaye alifunga ndoa na Nazar Nyoni, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu kati ya mwaka 1975 hadi 1980.
Mwaka 1962 mama Nyoni alifanikiwa kwenda Uswisi kwa masomo, ambapo alipata Diploma ya Maarifa ya Nyumbani na kujifunza Kifaransa na aliporejea, alianza kufundisha Lugha ya Kifaransa Shule ya Sekondari Kibasila, kabla ya kwenda tena kusomea Diploma ya Lugha ya Kifaransa mwaka 1978-1979 na kufundisha shule mbalimbali nchini.
Mwaka 1993 alistaafu kutoka serikalini, lakini baadaye alisomea Diploma ya Katekesi katika Chuo cha Salvatorian mjini Morogoro na kufundisha somo la dini katika shule tofauti mjini humo, ambapo sasa anamiliki Shule ya Awali iitwayo Rosemery Perler, ambayo pia ipo mjini Morogoro.
Nafasi yake kama mke wa waziri
Akizungumzia alivyoitumia nafasi ya mumewe aliyekuwa naibu waziri wa elimu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Hayati Julius Nyerere, mama Nyoni anaeleza kuwa alimsaidia kuonana na kujuana zaidi na watu.
“Imenisaidia kuonana na kujuana na watu zaidi, lakini mwenyewe alikuwa ndiyo mwalimu wangu maishani mwangu. Alikuwa mkali sana, huwezi kwenda kwa jirani, kwa sababu hiyo hatukujua umbea au ulimwengu. Alitufundisha namna ya kuchangamana na watu na kuvumilia,” anasema.
Maisha ya sasa na zamani
Akizungumzia maisha ya sasa na zamani Mama Nyoni alieleza: “Wakati huo wanawake tulijiheshimu na kuwa na aibu kama wanawake lakini leo wasichana hata wanawake, hawana aibu ya kike. Mavazi yanatisha, lugha ya matusi, wanawake wanaongea matusi ya nguoni, ukiyasikia masikio yanawasha, lakini wengine wanashabikia mambo hayo ya kihuni bila aibu. Ni tofauti na zamani mwanamke wa aina hiyo angezomewa.”
Akionyesha hofu anasema: “Sijui kama kuna cha kurekebisha, naona mambo yamekwenda mbali.”
Hata hivyo, anashauri: “Wanawake tukiwa na ushirika tutaweza kuelezana, tutumie misikiti na makanisa au vikundi turejeshe maadili ya mwanamke, na siyo kutoa lugha chafu barabarani.”
Akizungumzia elimu hasa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana Mama Nyoni anasema kuwa matokeo mabaya ya mtihani huo yamesababishwa na Serikali kutokuwajali walimu na kutokutekeleza matakwa yao hata kuiondolea heshima iliyokuwepo kwa walimu miaka iliyopita.
“Chanzo cha matokeo mabaya ni kwamba, walimu wamegoma, wamefanya mgomo baridi kwani hawasikilizwi. Pia mabadiliko ya muhtasari na mitalaa,” anasema akiongeza:
“Nashauri Serikali isipokee kila kitu kipya kuhusu elimu ya taifa letu, siyo huyu kaleta tunapokea, yule kasema vile tunabadili, hali hiyo inawachosha walimu. Ni muhimu sasa walimu wasikilizwe shida zao wasidharauliwe. Sisi tulivumilia siyo walimu wa sasa.”