TUONGEE KIUME: Je, mahari si sehemu ya kuchochea mfumo dume?
Moja ya vitu vinavyonitatiza linapokuja suala la ndoa ni mahari. Ni kama nywele za kichwa, zipo hapo siku zote lakini zipo kwa ajili ya kazi gani hujui.
Mahari ipo miaka nenda rudi kama mila au desturi, huku idadi kubwa ya watu wanaoitekeleza wakiitafsiri kama pesa au kitu ambacho hutolewa na mwanaume kama malipo kwa familia ya mwanamke pindi anapotaka kumuoa.
Lakini kimantiki, vitu pekee vinavyolipiwa chini ya jua ni bidhaa na huduma. Tunalipia sabuni ya kuogea na dawa za meno dukani, tunalipia mafuta ya kupikia na sukari kwa mangi hizo ni bidhaa.
Wakati tukienda hospitali tunalipia matibabu, kwenye basi tunalipia nauli, huku Yanga na Simba zikicheza tunalipia ili kuingia uwanjani kutazama mechi hizo ni huduma.
Sasa tukirudi kwenye mahari, kwanini tunailipa familia ya mwanamke ili kumuoa binti yao? Je, ni kwa sababu mwanamke ni bidhaa au ni huduma? Kama sio kwanini tunalipa ili kuoa?
Kuna baadhi ya watu wanajenga hoja kwa kusema kuwa unalipa kama zawadi kwa familia ya mwanamke kwa kumtunza binti kipindi chote hicho sawa ni kitu kizuri, lakini kwa upande wa pili, hata mwanaume ana wazazi, alitunzwa kipindi chote na familia yake, itakuwaje kama familia ya mwanamke nayo ikitoa zawadi ya pesa nyingi au ngombe kwa familia ya mume, haitapendeza?
Lengo hapa sio kwamba na wanaume pia wawe wanatolewa mahari, lengo ni kujaribu kuona mahari ipo hapo siku zote kwa ajili gani? Kama ipo kwa sababu zisizokuwa na msingi, kwanini iendelee kuwepo? Yaani kwanini tusiitoe kama ina sababu zisizoeleweka.
Au kama tunaipenda sana, basi familia zote mbili zilipe mahali. Familia ya mwanamke ilipe mahari kwa familia ya mwanaume na ya mwanaume ilipe mahari kwa familia ya mwanamke.
Kuna watu watabeza tunachokizungumza hapa, kwamba wanaume siku hizi wamekuaje? Wanadai kulipiwa Mahari pia. Lakini kama watatokea watakaobeza hivyo, wajiulize kwanini wanabeza mwanaume kulipiwa mahari, watagundua kuwa kumbe hii kitu mahari ina kawaida ya kumshusha mtu anayelipiwa, anaonekana mdogo, anaonekana hana nguvu, anaonekana hajiwezi, anaonekana ni bidhaa, anaonekana ni mtoa huduma tu jambo ambalo kiukweli halistahili kuwemo ndani ya ndoa.
Kwa mtazamao wangu, mahari kwenye ndoa ni kama kipande cha utumwa kilichobaki, na kikapewa jina lingine zuri zuri ili kuufanya utumwa kuwa halali.
Natamani siku moja nione wanaharakati wanaotetea haki za wanawake, siku moja waamke na hii ya kupinga Mahari kwa mwanamke pindi anapoolewa kwa sababu inamshusha thamani mwanamke na huenda ni moja ya sababu zinachochea mfumo dume kwa nguvu kubwa.
Nadhani mila na desturi ya kulipa mahali ni moja ya tamaduni unatakiwa kuzitema. Wewe una mtazamo gani kuhusu mahari? Je ni kitu kizuri kuendelea kuwepo? Au kipigwe chini tu?