Tusiwacheke na kuwahukumu wenza wanapoachana
Muktasari:
- Nani anajua kesho yake au nani ni mkamilifu kiasi cha kuwacheka wengine badala ya kuwaonea huruma na kuwasaidia?
Canada. Kawaida, wawili wafungapo ndoa hutegemea kuishi pamoja hadi kifo kiwatenganishe. Haya ndiyo maneno wasemayo katika viapo vya ndoa kwa Wakristo.
Kwa imani nyingine, hatujui. Hata kama hawatamki au kutamkiana haya maneno, tunaamini wote wanaofunga ndoa hutegemea kuishi pamoja maisha yao yote. Hapa, swali ni je, ni kwanini ndoa huvunjika japo si zote? Hili swali, japo ni fupi na dogo ni gumu na halina jibu moja.
Tujuacho ni kwamba kudumu au kuvunjika kwa ndoa ni matokeo ya mambo mengi yakiwamo majaliwa, hasa wawili wanafungapo ndoa bila kujua wanachofanya japo wanaweza kujihisi wanajua wasijue hawajui.
Pia, yapo mambo mengine mengi ambayo ni matokeo ya matendo au tabia za wahusika. Hivyo, kudumu au kutodumu kwa ndoa ni mkusanyiko wa mambo mengi makubwa na madogo.
Kutokana na uzoefu, kitu tunachoweza kusema ni kwamba wanaojenga ndoa ndiyo hao waidumishao au kuibomoa. Mfano, wawili wanapofunga ndoa, hufikia uamuzi huu wao peke yao tena bila shuruti.
Hivyo, kila matokeo ya ndoa huwategemea wao. Hata hivyo, pamoja na kuamua wenyewe peke yao, wapo baadhi ya wanandoa ambao huigeuza ndoa kama klabu au ushirika. Hii maana yake ni nini? Bahati mbaya, wahusika huwaruhusu wasiohusika kujihusisha na ndoa yao.
Kimsingi, wawili husahau kuwa ndoa ikidumu au kuvunjika, wanufaika au waathirika ni wao na si hao waliowahusisha.
Tulichojifunza
Katika suluhisha migogoro mingi ya ndoa au kushuhudia zikivunjika, tumejifunza mambo makuu manne.
Mosi, wote huumia hata kuumizana kutokana na pigo au hasara wanayopata tofauti na walivyotegemea wala kupanga. Asikudanganye mtu kuwa anaweza kuacha au kuachika akasherehekea, japo siku hizi, kumezuka uongo wa walioachika au kuacha kujifanya wanasherehekea.
Ndiyo, wanaweza kutuonyesha kuwa wanasherehekea usoni, ila nyoyoni wanaumia. Hili, halina mjadala. Jiulize. Walipofunga ndoa walihuzunika au kufurahi? Jibu liko wazi. Sasa inakuwaje waathirika hawa washerehekee hasara na pigo kubwa kama hili?
Pili, wote huhisi hasara na hata upungufu. Kwanini wengine waweze sisi tushindwe? Binadamu, kiasili, anapenda mafanikio na kuchukia maanguko. Hivyo, ndoa inapodumu, wanandoa huona fahari na furaha.
Ikivunjika, hata wajikaze vipi, maumivu tena makubwa yapo. Kwanza, kuna wasiwasi wa namna jamii inavyowaangalia. Pili, kuna malengo na matarajio yaliyouawa. Na tatu, kuna aibu ya kushindwa. Mara nyingi, wengi walioacha au kuachwa hasa wenye watoto, hushindwa kuwashauri watoto wao juu ya ndoa kwa vile wao walishindwa.
Tatu, ipo jamii inayowazunguka. Hapa, ndipo kichwa cha makala hii kinapoingia na kugusa pabaya. Wengi hasa wasiojua uhalisia wa ndoa wanaweza kuwacheka na kuwaona wanandoa ambao ndoa yao imesambaratika na kuvunjika kama watu walioshindwa.
Hapa ndipo tatizo la kuwacheka wahusika au kuchekwa linapoanza. Kama tulivyosema, wanaovunja ndoa ni wanandoa wengine wakisaidiwa na wasio wanandoa kwa namna mbalimbali. Je, kuna haja ya kuwacheka au kuwaonea huruma?
Nani anajua kesho yake au nani ni mkamilifu kiasi cha kuwacheka wengine badala ya kuwaonea huruma na kuwasaidia? Kabla ya kuwacheka, vaeni viatu vya wahusika. Jiulize swali moja kuu japo dogo lakini lenye mafunzo makubwa na mengi “je, ingekuwa mimi, ningetaka wenzangu wanifanyie nini au kunichukuliaje?”
Tuwe na huruma na utu. Badala ya kuwacheka wanandoa, tushukuru Mungu kuwa hatupitii wanayopitia. Tujifunze kitu kutoka kwao badala ya kuwabagaza, kuwacheka, na kuwasimanga. Kumbuka hujafa hujaumbika na kutenda makosa ni asili ya binadamu.
Wanandoa ambao ndoa yao imevunjika ni kama wagonjwa. Hakuna haja ya kuwalaumu wala kuwasimanga bali kuwaonea huruma au kuwasaidia. Hakuna anayependa ndoa yake ivunjike japo wahusika wanavunja ndoa yao kutokana na ujinga juu ya mambo fulani fulani yawe ya kimalezi, kitabia, kiuhusiano, kiuchumi, kitaaluma, ubinafsi, uchoyo, upumbavu na hata kutojali mambo fulani kwa wakati fulani.
Tumalizie kwa kusisitiza kuwa kuwacheka wanandoa walioachana si kuwatendea haki. Maana, kitanda usicholalia hujui kunguni wake. Ni rahisi kuhukumu, kulaumu, hata kutweza.
Je, ushawahi kujiuliza? Ningekuwa mimi, ningependa nichukuliweje hasa kipindi hiki kigumu na pigo kubwa katika maisha? Ikumbukwe si wote wanaoacha au kuachika, huoa au kuolewa tena. Tuwaoneeni huruma watu hawa.