Ukifanya haya unaathiri makuzi ya mtoto wako

Mfano wa picha ya wazazi wakicheza na binti yao. Picha kwa msaada wa Akili Bandia (AI).

Kila mtoto ana ndoto ya kuishi maisha mazuri bila kujali anatokea katika familia ya maisha aina gani, iwe ya kitajiri, kati hata ya kimasikini, ndiyo maana wapo wanaopambana tangu wakiwa wadogo.

Kutokana na familia wanazotoka, watoto wamejikuta wakishirikishwa katika biashara za wazazi wao tangu wakiwa wachanga hadi wanapofikia umri wa kujitegemea.

Wapo watoto ambao wamejikuta wakiambatana na wazazi wao katika biashara na kushinda nao kuanzia asubuhi hadi usiku kwa ajili ya kuwasaidia kuhudumia wateja na wengine wakiwa hawana sehemu ya kuwaacha bila kujali wanapokuwa nao wanawaweka watoto wao kwenye hatari.

Kutokana na hali hiyo, Mwananchi ilifanya utafiti wa kufahamu kwa nini wazazi wanaamua kuwashirikisha watoto kwenye biashara wanazofanya wakati wanatakiwa kujisomea na wengine kujifunza masuala mbalimbali, ikiwepo kucheza na wenzao sehemu wanazoishi.

Wazazi tuliozungumza nao wanasema kuwa hali ya uchumi na mazingira kutokuwa rafiki ni sababu ya wao kwenda na watoto au kuwashirikisha kwenye biashara zao kama wasaidizi.


Wazazi walonga

Mariam Kinyogori, muuza chakula mbezi Luis anasema amejikuta anamtumia mwanawe katika biashara yake ya chakula kama msaidizi wake na hata ikitokea amepata tatizo lolote binti yake anaweza kuendelea na biashara hiyo na kuweza kuwasaidia wadogo zake ambao ni wadogo.

“Si kwamba napenda kumtumia mtoto wangu katika biashara yangu ya chakula, hii imetokana na wasaidizi ninaowapata hawadumu na wengine si waaminifu, hivyo kuna wakati napata hasara kwa sababu ya kuwatumia watu baki,” anasema Mariam.

Anasema kwenye biashara kuna mambo mengi mazuri na mabaya ambayo mtoto hatakiwi kuyafahamu, hususan kwa yale mabaya, lakini wanayafahamu kwa kuwa ni uhalisia na si uigizaji.

Mariam anasema katika eneo hilo kuna kila aina ya tabia ambazo si nzuri kwa watoto kujifunza, licha ya kuwapeleka watoto wao kwani mazingira yanaweza kuwaharibia na kuyabeba mambo mabaya na kuacha mazuri.

Anasema kuna hatari ambayo anamuweka mwanaye na inawezekana kutotimiza ndoto zake za kusoma kwa sababu muda mwingi anaotakiwa kusoma wakati wa usiku anautumia kutafuta kipato kwa ajili ya kujikimu na familia yao.

“Wakati mwingine nikifikiria kuhusu maisha niliyopitia mimi sitamani wanangu wapitie, tatizo linakuja sina uwezo wa kumlipa msichana kwa sasa na mabinti tunaowapa kazi wanaishia kutuibia na kuondoka,” anasema Mariam.

Naye Janeth Julius, mkazi wa Buguruni anasema analazimika kutembea na mtoto wake kwenye biashara kwa sababu hakuna mtu wa kumuachia kutokana na mazingira anayoishi si salama.

“Dunia kwa sasa imeharibika, siwezi kumuacha mtoto wangu, hivyo najikuta natembea naye kwenye biashara zangu za kuuza mboga, hapo inakuwa jua na mvua yangu na ninatoka na mtoto asubuhi tunarudi tutakapomaliza,” anasema Janeth.

Anasema si kazi rahisi kutembea na mtoto katika maeneo tofauti maana hampi mtoto nafasi ya kucheza na wenzie wala kujifunza vitu vya kitoto kutokana na muda anaorudi nyumbani ni wa kuchelewa, hivyo si rahisi kupata watoto wenzie wa kucheza naye.

Jafari Mohamed anasema baadhi ya wazazi wanawatumia watoto wao kama sehemu ya kujipatia fedha kwa kuwavutia wateja wengi kwa kucheka na wanaume.

“Kuna biashara ambazo wateja wake ni wanaume, unakuta mama haogopi kuwa na mtoto wake hadi wakati wa usiku bila kujali kuwa anamuweka mtoto wake kwenye mazingira hatarishi kwa sababu anakutana na watu wenye tabia tofauti,” anasema Jafari.

Anasema wakati mwingine watoto wanashuhudia wazazi wao wakiwa wanashikwa na kufedheheshwa na wanaume, hivyo mtoto anakuwa anasoma mazingira na kufikiria huo ni uhalisia wa biashara hivyo wanakua wakiwa na fikra ya walichokiona. Jafari anasema baadhi ya wazazi wanatengeneza kizazi kitakachokosa maadili ambayo yametengenezewa mazingira na wazazi wenyewe wakati wa kutafuta kipato.


Kisaikolojia ikoje

Akizungumza na Mwananchi, mwanasaikolojia Ramadhani Massenga anasema watu wanaishi kwa kuona matendo na si kwa kusikia, hivyo kila kinachoonekana kinaenda kukaa kwenye ubongo na kutoka si rahisi.

Hivyo, katika malezi ya watoto anasema kuna vitu vinatakiwa kuzingatiwa, hususan wakati wa kupima uwezo wa mtoto katika kutambua vitu.

“Mazingira anayoishi mtoto ndiyo yanayoweza kuelezea kuwa huyo mtoto ana akili au hana, kwani wazazi wanaokuwa na watoto wao kwenye biashara wanaweza kupata athari za mmomonyoko wa maadili bila kutambua,” anasema Massenga. Anasema athari zake zinatokea kwa watoto wanaokwenda shule au kuishi mazingira ya mbali na mzazi wake anakuwa na kumbukumbu ya matukio yaliyotokea kwenye mazingira ya biashara ya mzazi au mlezi wake.

“Hapo ndipo wazazi wanapokosa msaada kwa sababu mtoto hajui wa kumsikiliza nani na hana uwezo wa kupambanua mambo kwa kina kwa kutambua zuri na baya, kwani mzazi wake ameamua kumpeleka sehemu ambayo mtoto anajifunza lugha na kuona matukio yasiyofaa katika malezi yake,” anasema.

Anasema wazazi wamejikuta wakiwabebesha watoto vitu ambavyo hawakustahili, lakini kutokana na mazingira waliyopelekwa na mzazi wao wanajikuta hawezi kuthamini na kuheshimu watu wengine.

Katika malezi ya watoto anasema wazazi wanatakiwa kuwapa nafasi ya kucheza na kupumzika na hawatakiwi kuwa katika mazingira yatakayoathiri utoto wao kwa kuwepo kwa matendo yatakayotendeka ya kumzidi umri.

Mkaguzi wa Polisi, kata ya Mgusu, Mkoa wa Geita, Alfred Nkoma aliwahi kusema wazazi wamekuwa vinara wa ukatili wa kiuchumi kwa watoto kutokana na wao kuwatumikisha kwenye shughuli za kujipatia kipato na kuwanyima fursa ya kupata elimu.

“Wanawake manwakatili watoto bila kujua,unamkuta mama kamtuma mtoto kuuza mkaa wengine ndizi na vitumbua muda ambao wenzake wako darasani wengine jioni hadi usiku wanatembeza ndizi au karanga baa huu ni ukatili,”alisema Nkoma.