Kaa mbali, hawa wapo kwenye gemu kitambo

Muktasari:
Leo hali imebadilika na muziki umetengeneza ajira na unachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kupitia matamasha na uuzwaji wa kazi za wanamuziki jambo ambalo linahesabiwa kwamba ni mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Muziki wa kizazi kipya umetimiza miaka 15 tangu chimbuko lake ambalo kimsingi uliweza kupenya mwaka ya 2000 baada ya vita kali kati ya vijana na wazee ambao mwanzoni walishindwa kuuelewa.
Leo hali imebadilika na muziki umetengeneza ajira na unachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kupitia matamasha na uuzwaji wa kazi za wanamuziki jambo ambalo linahesabiwa kwamba ni mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Hivi sasa vijana wengi wamejiajiri katika muziki, kuna watayarishaji, wapigapicha za filamu na mnato, wanahabari pia mameneja ingawa ipo dhana iliyojengeka kwamba kutokana na ubunifu duni uliopo katika sekta hii ndiyo chanzo kikubwa cha muziki huo kutodumu kwa muda mrefu. Ungana na Sterehe ambapo katika makala haya imewachambua wanamuziki waliokuwapo zamani ambao mpaka sasa wanaendelea kutikisa medani ya muziki wa kizazi kipya kwa mtiririko huru bila kujali nani wa kwanza na nani wa mwisho.
1. Dully Sykes
Huyu ndiyo Bongo Fleva mwenyewe, wakati muziki huu unaanza, wengi walikuwa wakiufanya kwa mtindo wa Hip Hop wakiiga wanamuziki wa ulaya wakihisi kwamba kizazi kipya ni kufoka.
Dully Sykes alikuja na mtindo wa kuimba jambo ambalo wasanii wenzake mwanzoni walilidharau. Nyimbo kama Nyambizi, Julietha, ndizo zilizomtambulisha na mpaka leo ni mwanamuziki ambaye panga pangua, kama una mpango wa kuandaa tamasha kubwa la muziki wa kizazi kipya ili linoge, mtie Dully ndani, utafurahi. Dully Skyes kwa sasa anatamba na ‘singo’ yake ya Togola.
2. Khaleed Mohamed TID
Utambulisho wake ulikuwa wimbo wa Zeze ambao ulifanyiwa picha za video na Kampuni ya 2 Eyes iliyokuwa ya kwanza yenye nguvu kutambulika kwenye medani ya muziki wa kizazi kipya.
2 Eyes leo hawapo, kila mtu kaenda kwake lakini Khaleed Mohamed bado anasonga mbele na muziki wa kizazi kipya, amekua zaidi na sasa anamiliki bendi yake mwenyewe inayojulikana kwa jina la Top Band.
Ukiulizia jinsi alivyoanza, TID alikuwa ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za Kiingereza, lakini alipokuja kugundua muziki uko mtaani na kutumia lugha ya nyumbani ndiyo alitoka na mpaka leo anaendelea kuishi kwa kutumia muziki wa kizazi kipya.
3. Lady Jaydee
Ukizungumzia wanamuziki waliodumu kwa muda mrefu na kuonyesha mafanikio mpaka sasa huwezi muacha mwanadada huyu. Jide ni mmoja kati ya wanamuziki waliousimamisha muziki wa kizazi kipya nchini na kuufikisha hapa ulipo tangu akiwa mwanamuziki mdogo, mpaka leo ni mwanamuziki mkubwa mwenye heshima kubwa.
Mwanzoni watu hawakumuelewa alipokuwa anafanya muziki wa rap, kipindi hicho ambapo matamasha yalikuwa yakifanyika Diamond Jubilee na Kilimanjaro PoolSide. Lakini alipoamua kubadili miondoko na kuimba akaeleweka na kujizolea mashabiki wengi wa jinsi yake waliowavuta watu wao wa karibu kuwa mashabiki wake.
Jana alikuwapo, lakini leo ni mfano wa mwanamuziki mkubwa na mwekezaji ambaye ametumia kipaji chake cha kuimba vizuri na kutengeneza maisha yake.
4. Juma Nature
Tangu anaanza muziki na wimbo wake wa kumuonya kijana anayebadili tabia na kuidharau mila ya Mtanzania ulioitwa `Jinsi Kijana, mpaka leo hii, ukimuweka jukwaani, Juma Kassim Kiroboto (Nature) na msanii mwingine yoyote wa kizazi kipya lazima ataangushwa.
Sababu ya msingi ni aina ya muziki anaoimba unaendana na maisha ya kila siku ya Mtanzania na hata majina ya nyimbo zake ni majina ya vitu ambavyo Mtanzania wa kawaida kabisa ni rahisi kuvielewa.
Ugali, Mugambo, Kighetogheto na mengineyo ni kati ya majina ya nyimbo za Nature ambazo zilitikisa sana medani ya muziki wa kizazi kipya na mpaka leo akipanda jukwaani anagusa hisia za watu ndiyo sababu mpaka leo anaitingisha medani ya muziki wa kizazi kipya.
5. Profesa Jay
Alianza kuwa shabiki, mkereketwa wa kutupwa wa kundi la muziki wa kizazi kipya la Hard Blasters. Alikuwa akishirikiana na kundi hili katika kuandika na mikakati mingine ya kuendesha kundi lakini ghafla naye akajikuta akishiriki wimbo mmoja uliohamisha kabisa hisia zake za kimaisha.
Wakati huo alikuwa ni mfanyakazi wa kampuni ya simu na ndipo akahamia kwenye muziki baada ya kujihakikishia usalama ndani ya kibao cha Chemsha Bongo.
Hapo ndipo Nigga Jay wa Mitulinga akaanza kujulikana na safari ya muziki ikaanzia hapo.
Mpaka leo hii Profesa Jay ni mwanamuziki anayeweza kusimama jukwaani na kuangusha nyimbo 15 bila mashabiki wake kukaa chini kutokana na ubora wake katika medani ya muziki wa kizazi kipya.
6. AY
Jina lake kamili ni Ambwene Allen Yessayah. Ni mwanamuziki wa muziki aina ya Komesho, Rap na Hip Hop. Ametoa nyimbo nyingi zilizowahi kutambazikiwamo Raha Tu 1-2, Raha Kamili, Machoni kama watu na Binadamu zilizo weza kupenya katika soko la Afrika Mashariki na Afrika.
Kipaji cha AY kilianza kung’aa pale alipokuwa na kundi la East Coast Team linaloongozwa na Gwamaka Kaihula kama King Crazy GK na mwenzake Khamis Mwinjuma maarufu kama Mwana Falsafa au Mwana FA. Licha ya kundi hilo kuvunjika bado mwanamuziki huyo ameendelea kutamba mpaka leo.
7. Mwana FA
Tofauti na AY, Mwana FA yeye hakufanikiwa kuliteka soko la muziki Afrika lakini nyimbo yake kama Zamani imeweza kutikisa katika anga ya muziki wa Bongo.
Mwana FA naye kama ilivyo kwa rafiki yake AY walikutana katika Kundi la East Coast Team chini ya uongozi wake Crazy GK lakini baada kundi hilo kuvunjika bado ameendelea kufanya makubwa katika tasnia hiyo mpaka sasa ambapo ameendelea kupata show mbalimbali na kutowaangusha mashabiki wake.