Luiza Mbutu alipiga chini kwaya aingie Twanga Pepeta
Mwanamuziki wa bendi ya Twanga Pepeta, Luiza Mbutu amesema alipofanya maamuzi ya kuanza kuimba nyimbo za kidunia aliwagawa wanakwaya wenzake.
Luiza ambaye kwa sasa ana miaka 20 tangu ajiunge na bendi ya Twanga, amesema kuna wengine walimuona kama amepotoka huku wengine wakimtetea.
Amesema kutokana na hilo ilibidi awaeleweshe kwamba nayo ni kazi kama kazi nyingine na huko ndiko aliamua kwenda kutafutia mkate wake wa siku jambo ambalo baadhi walimuunga mkono.
Luiza alisema pamoja na kuhamia katika muziki huo wa dunia bado alikuwa akipata nafasi anaenda kanisani na kuimba japokuwa amekiri kwa sasa ameacha kutokana na ratiba zake kubadilika.
Akizungumzia kuhusu kukaa kwake muda mrefu Twanga bila ya kuhama, alisema amelazimika kufanya hivyo baada ya kujifunza kwa watu waliohama na kurudi.
“Kwangu mimi sijaona cha kunihamisha Twanga, mbali ya kuwa ndio bendi iliyonilea na kuwa mmoja wa waanzilishi, nimejifunza kwa wengine waliohama na baadaye kurejea.
“Kwani wasanii waliamuaga kuondoka Twanga mbali ya kutopata maslahi hayo waliyofikiria huko nje, lakini hata baadhi yao thamani imeshuka, kwa kuonekana na mashabiki kwamba hawana msimamo,”alisema Luiza.
Akiongelea kushuka kwa muziki wa dansi ukilinganisha na zamani, Luiza alisema kwake anaona ni jambo la kawaida kwani muziki ni kama biashara nyingine ambazo kuna wakati hupanda na kushuka.
Kutokana na hilo alisema wasanii katika muziki huo wanapaswa kuwa wavumilivu na wabunifu zaidi ili waweze kuendelea na kazi hiyo ambayo ndio inawaweka mjini.