Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazazi wanachangia watoto wao kufeli

Wanafunzi wakisaidiwa na wasamaria wema kuvuka barabara hivi karibuni

Muktasari:

Hata hivyo, jitihada hizi zimeonekana kugonga mwamba, kwani ubora wa elimu unaotolewa kwenye taasisi hizo unatia shaka. Matokeo ya mitihani ya kitaifa katika miaka ya karibuni unashadadia ukweli wa hali mbaya ya elimu ilivyo shuleni.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita Tanzania imekuwa na rekodi nzuri ya kupanua wigo wa elimu kuanzia idadi ya wanafunzi, miundombinu na hata idadi ya walimu.

Hata hivyo, jitihada hizi zimeonekana kugonga mwamba, kwani ubora wa elimu unaotolewa kwenye taasisi hizo unatia shaka. Matokeo ya mitihani ya kitaifa katika miaka ya karibuni unashadadia ukweli wa hali mbaya ya elimu ilivyo shuleni.

Mfano mzuri wa matokeo hayo ni yale ya kidato cha nne ya mwaka 2012, ambayo yameacha historia ya kusikitisha katika sekta ya elimu, kufuatia idadi kubwa ya watahiniwa wake kufeli.

Katika matokeo hayo, asilimia 60 ya watahiniwa walipata daraja sifuri.Wapo watahiniwa ambao hawakuamini matokeo hayo kiasi cha wengine kufikia hatua ya kujitoa uhai. Lakini wapo waliokataa rufaa ili warudie mitihani upya.

Kwa kuwa matokeo hayo yalizusha mjadala mkubwa wa kitaifa, Serikali kupitia Waziri Mkuu ikalazimika kuunda tume maalumu kuchunguza sababu za matokeo hayo kuwa mabaya.

Kimsingi, watu wengi katika jamii wanaamini kuwa miongoni mwa sababu kubwa zilizochangia matokeo hayo ni pamoja na migomo ya walimu, mazingira duni ya kufundishia, kukosekana kwa mtalaa na ukosefu wa walimu wenye sifa shuleni.

Hata hivyo, mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo anasema hoja ya mtalaa inayopigiwa kelele kila kukicha, siyo sababu ya msingi ya kufeli kwa wanafunzi.

Hata nami naamini kuwa yapo masuala mengine muhimu yanayochangia ufaulu mdogo katika mitihani yetu, ikiwamo wazazi wengi kutowajibika ipasavyo kusimamia maendeleo ya taaluma ya watoto wao.

Kwa mtazamo wangu, mchango wa wazazi katika ufaulu wa mwanafunzi unachukua asilimia kubwa kuliko muda anaoutumia akiwa shuleni.Wadau wanasema mpaka sasa ufuatiliaji wa wazazi unadaiwa kuwa ni asilimia mbili tu hapa nchini ukilinganisha na mataifa mengine.

Jukumu la mzazi ni kuhakikisha anafahamu mwenendo wa tabia za mwanaye shuleni, lakini sasa kazi hiyo wameachiwa walimu na watendaji wengine katika sekta ya elimu.

Sababu kubwa ya wazazi kutokuwa karibu na watoto wao zinaelezwa kuwa ni pamoja na mazingira ya nyumbani.

Jambo la kujiuliza mtoto anaporudi kutoka shuleni kila siku anakutana na kitu gani? Kama baba ni muuza nyanya basi ni sahihi akutane na matenga ya nyanya kama ilivyo kwa mwalimu atavyokutana na vitabu?

Ni dhahiri wazazi wengi hawana muda wa kukaa na watoto wao kujadili masuala ya elimu. Badala yake wamekuwa mstari wa mbele kulalamika pindi mambo yanapoharibika kama ilivyotokea katika matokeo haya.

Haiwezekani mwanafunzi amalize mwaka mzima wa masomo bila ya mzazi wake kumuulizia kuhusu maendeleo yake. Huku ni kutowajibika kulikozidi ada.

Nimezungumza na Edmary Edy ambaye ni mwanafunzi darasa la saba katika shule ya msingi Kawawa iliyopo Kigogo Luhanga jijini Dar es Salaam. Edmary anasema tangu ameanza masomo yake ya darasa la saba kwa huu hakuwahi kuhojiwa au kukaguliwa maendeleo yake shuleni.

Edmary anasema kila anaporudi nyumbani na wenzake,hutumia muda wake mwingi kwenda katika mazoezi ya mpira wa mguu.

”Sijawahi kuulizwa maendeleo yangu ya shuleni tangu niingie darasa la saba,ni mara chache sana inapotokea mzee wangu nakagua madaftari yangu”anasema.

Baba mzazi wa Edmary ni mfanyabiashara wa maziwa, hivyo muda mwingi baba yake humtumia katika biashara zake pale anapotoka shuleni.

Edmary ni mmoja kati ya maelfu ya wanafunzi ambao licha ya kuwapo mijini, wazazi wao hawana mpango nao katika maendeleo.

Watanzania tubadilike kwa kuchukua hatua za kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wetu badala ya kutupia lawama Serikali.