Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa tofauti ya shule za dini na za umma kitaaluma

Wamafunzi wa Shule ya Sekondari ya Seminari Katoke ,wakisalimiana na Rais John Magufuli aliyewatembelea.Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Matokeo hayo yameshuhudia kiwango cha ufaulu kikiongezeka kwa asilimia 7.22 kutoka asilimia 70.35 mwaka 2016 hadi asilimia 77.57 mwaka 2017.

Januari 30, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.

Matokeo hayo yameshuhudia kiwango cha ufaulu kikiongezeka kwa asilimia 7.22 kutoka asilimia 70.35 mwaka 2016 hadi asilimia 77.57 mwaka 2017.

Wakati kiwango cha ufaulu kikiongezeka, matokeo hayo yameshuhudia pia shule binafsi zikiendelea kutamba dhidi ya zile za Serikali.

Katika shule 100, shule za Serikali zilizofanikiwa kupenya ni sita pekee. Shule hizo ni Mzumbe iliyoshika nafasi ya 21, Kibaha (31), Ilboru (39), Kilakala (40), Tabora Boys (60) na Tabora Girls iliyoshika nafasi ya 66.

Shule za dini vinara

Wakati shule za umma zikipigwa kumbo, katika kundi hilo, shule zinazomilikiwa na taasisi za dini zimeonekana kufanya vyema. Zaidi ya shule 20 za taasisi za dini, zimeingia katika orodha ya shule bora 100.

Baadhi ya shule zinazomilikiwa na taasisi za dini zilizoingia 100 ni, Shemsiye Boys iliyoshika nafasi ya 10, Don Bosco (16), Uru (20), Nyegezi (27), Centennial Christian (30), St Joseph Iterambogo (41), St Aloysius Gonzaga Boys (42) na St James (44), Makoko (61), Geita Adventist (75), Sanu (76) na Buhongwa Islamic (86).

Sababu za kufanya vizuri

Mdau wa masuala ya elimu, Ezekiel Oluoch anasema shule za dini zinafanya vizuri kuliko za umma, kutokana na kuwa na mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.

“Wanafunzi wengi wanaosoma shule za Serikali wanaishi nyumbani, lakini shule za dini wanaishi bweni. Hapa ndipo unaweza kuona tofauti. Mwanafunzi anapokuwa bweni anakuwa na nafasi kubwa ya kujisomea,” anasema na kuongeza:

“Mwanafunzi anayeishi mbali na shule anakutana na changamoto mbalimbali hasa watoto wa kike, jambo hili linarudisha nyuma kiwango cha elimu na inakuwa ngumu kufikia uwezo wa shule za dini ambazo hata walimu wao wako karibu na wanafunzi.”

Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Watoaji wa elimu wasiotegemea Serikali kusini mwa Jangwa la Sahara, Benjamin Nkonya, anasema shule za dini na binafsi mara nyingi zinafanya vizuri kwa sababu ya msukumo kutoka wizarani unaozitaka kuzingatia sheria na taratibu za utoaji wa elimu, jambo analosema linakosekana katika shule za umma.

“Wakija wanataka kila kinachotakiwa kuwapo kinakuwapo kwa hiyo kama ukali uleule ungetumika katika shule za Serikali, ufaulu ungekuwa mkubwa lakini kwa kuwa wanatubana sisi ndiyo maana unaona matokeo yanavyokuwa mazuri,” anaseama

Mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Frank Yohana, anakwenda mbali zaidi akisema shule za dini licha ya kuwa na mazingira mazuri, lakini mwanafunzi anapokwenda kusoma shule hizo anakuwa amejiandaa kufuata taratibu zao.

“Unajua zile shule za dini kama unakuwa mjanjamjanja, unafanya mambo yasiyoeleweka, maadili yake yatakuweka kando. Wale wako makini na maadili kabla ya masomo. Kwa hiyo ukilinganisha tu hata mwanafunzi anayesoma shule za dini anavyokuwa katika jamii na yule wa shule za Serikali utaona tofauti kubwa,” anaeleza.

Ratiba Seminari ya Katoke

Paul Masanja aliyesoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Katoke Seminari mkoani Kagera, anasimulia maisha katika shule hiyo yalivyokuwa tofauti na shule ya Serikali aliyosoma kidato cha tano na sita.

Anasema nidhamu, kuzingatia ratiba na ushirikiano kati ya walimu na wanafunzi, ni miongoni wa sababu kubwa za shule yao kufanya vizuri.

Masanja anasimulia ratiba ya shule hiyo kuanzia asubuhi wanapoamka hadi kulala kati ya Jumatatu hadi Ijumaa.

“Ratiba yetu ilikuwa inaanza saa 11:00 asubuhi, tunajiandaa nusu saa kisha tunaingia kanisani saa 11:30 asubuhi na hii ni wanafunzi wote wa kidato cha kwanza hadi sita. Tunasali hadi Saa 1:30 asubuhi, inapofika saa 1:40 asubuhi vipindi vinaanza hadi saa 2:20 asubuhi kipindi kinaisha,” anasema Masanja na kuongeza:

“Tunafanya usafi kwa dakika 10 hadi saa 2:30 asubuhi tunakwenda kunywa uji na ni dakika 10 tu hadi saa 2:40 tunakwenda paredi. Hapo hadi saa 3:00 kamili asubuhi.”

Anasema wanaingia darasani saa 3:10 hadi saa 4:30 kisha wanakwenda mapumziko hadi saa 5:00 asubuhi wanapoingia darasani hadi saa 6:20 mchana wanapokuwa mapumziko hadi saa 6:30 mchana mapumziko ya dakika 10 kisha wanarudi darasani hadi saa 7:50 mchana.

“Saa 7:50 mchana tunatoka kwenda kula hadi saa 8:30 tunarudi darasani. Saa 8:30 hadi saa 9:50 alasiri tunakuwa darasani. Saa 9:55 inagongwa kengele tunakwenda kujiandaa kufanya kazi za mikono kama kulima barabara, mashamba kama ni msimu wa kilimo na usafi wa jumla kwani hakukuwa na wafanyakazi,” anasimulia Masanja.

Anasema saa 10:55 jioni, inagongwa kengele tunakwenda kujiandaa kwa ajili ya michezo kuanzia saa 10.55 hadi saa 11:55 jioni hapo ndio mwisho wa michezo. Baada ya hapo inagongwa kengele ya kwenda kuoga hadi saa 12.55 jioni muda wa kuoga unakuwa umeisha.

“Saa 1:00 usiku tunakwenda kula mpaka saa 1:30 usiku. Saa 1:30 usiku tunaingia darasani kujisomea hadi saa 2:00 usiku. Kisha tunatoka wote kwenda kuangalia taarifa ya habari hadi saa 2:30 na hili la taarifa ya habari ni wote hakuna mjadala,” anaongeza kusema.

Anasema saa 2:30 wanarudi darasani kujisomea tena hadi saa 4:15 usiku. Mwalimu anaweza kutuomba aje kutufundisha, kama tukikubali anakuja au tukimwomba naye akakubali anakuja.

“Saa 4:15 tunakwenda kanisani kusali ni kama dakika 14 au 20, ina maana hadi saa 4:30 au saa 4:50, baada ya hapo tunapewa dakika 10 za kwenda bwenini kulala. Saa 5:00 usiku kila mtu alale kitandani mwake asionekane anazunguka zunguka,” anasema

Kwa msisitizo Masanja anasema “hakuna kujisomea, taa zinazimwa zote na ukikutwa na taa unafukuzwa shule au ukikutwa unasoma huo muda wa kulala unafukuzwa shule. Ratiba ya seminari imewekwa na kila mtu anaizingatia na ukienda kinyume chake unafukuzwa shule.”

Anasema hiyo ni tofauti na shule za Serikali ambako walimu na wanafunzi hawafuatilii ratiba waliyojiwekea na hata inapovunjwa, hakuna hatua kali za kinidhamu zinazochukuliwa.

Masanja anasema ratiba hiyo hubadilika kidogo siku za Jumatano na Alhamsi kama kuna kufanya kazi za kufua na wakati mwingine Jumamosi hujiandaa kwa nyimbo kwa ajili ya siku inayofuata ya Jumapili kuimba kanisani.

“Seminari si mchezo, tukifunga tu shule siku ya kufungua ni mtihani na mitihani ya seminari kama uko kidato cha nne mtihani unaanzia kidato cha kwanza kwa hiyo unapaswa muda wote kujua na mitihani ipo ya mara kwa mara,” anasema

“Mimi nilihitimu mwaka 2013 na kupata daraja la kwanza pointi 15 lakini nilipokwenda Pugu Sekondari (Dar es Salaam) mchepuo wa sayansi nilijikuta namaliza kidato cha sita nikipata daraja la pili pointi 22.”

Kwa nini alishuka kiufaulu? anasema: “Kuna tofauti kubwa shule za seminari na za Serikali; kwanza kulikuwa hatuzingatii ratiba, hakuna mitihani ya mara kwa mara kama kule nilikotoka, vitabu navyo tatizo, walimu hawafuatilii. Unajua walimu wa Serikali unakuta anasema nyie muelewe au msielewe mimi mshahara wangu upo palepale; mazingira ya shule hayahamasishi na ndiyo maana niliyumba.”