Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtoto wa kike anavyosongwa katika safari ya kupata elimu

Muktasari:

  • Ni ukweli kuwa kuna raha na manufaa makubwa ya kumsomesha mtoto wa kike.
  • Ni kwa sababu hii hawakukosea waliosema; ‘Ukimsomesha mtoto wa kike, umeelimisha Taifa.’ Huu ni mfano mmoja miongoni mwa mingi inayotetea haki ya mtoto wa kike kupata elimu.
  • Dunia inaamini kuwa mwanamke aliyesoma anajiamini na anaweza kupambana na changamoto nyingi za kimaisha zinazomkabili. Anaweza kuiendeleza familia yake na Taifa kwa jumla.

Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa kwa kina wakati wa maadhimisho ya ‘Siku ya Wanawake Duniani’ yaliyofanyika wiki iliyopita, ni suala la elimu kwa mtoto wa kike.

Ni ukweli kuwa kuna raha na manufaa makubwa ya kumsomesha mtoto wa kike.

Ni kwa sababu hii hawakukosea waliosema; ‘Ukimsomesha mtoto wa kike, umeelimisha Taifa.’ Huu ni mfano mmoja miongoni mwa mingi inayotetea haki ya mtoto wa kike kupata elimu.

Dunia inaamini kuwa mwanamke aliyesoma anajiamini na anaweza kupambana na changamoto nyingi za kimaisha zinazomkabili. Anaweza kuiendeleza familia yake na Taifa kwa jumla.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa maadhimisho hayo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu alikiri kuwa elimu ni kati ya vitu vya msingi kwa maendeleo ya mwanamke na ni kati ya masuala muhimu ambayo Serikali imewekea mkazo.

“Kulikuwa na vikwazo vingi vilivyoturudisha nyuma kama kikwazo cha ukosefu wa elimu,”anasema.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi anasema ni ukweli usiopingika kwamba maandalizi ya mama bora, huanza tangu akiwa msichana. Anasema ikiwa watoto wa kike watapata elimu, ni dhahiri kuwa wataandaliwa wanawake walioelimika na hivyo kuwa rahisi kupambana na ukatili wowote dhidi yao.

Liundi anasema ni lazima Serikali itengeneze mpango wa kuwasaidia watoto wa kike watimize ndoto zao kielimu ili kuandaa wanawake bora wajao.

“Tunapoadhimisha siku ya mwanamke, lazima tutafakari kwa kina suala la elimu, tupo wapi na tunaelekea wapi kwa sababu huwezi kuwa na mwanamke bora usipowekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike, ” anasema.

Anafafanua kuwa kauli mbiu ya ‘Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi’ haiwezi kufikiwa ikiwa wasichana watabaki nyuma kielimu.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Eda Sanga anasema kati ya vitu walivyokuwa wakitilia mkazo tangu kuanzishwa kwa chama hicho miaka 30 iliyopita, ni kupigania haki ya mtoto wa kike kupata elimu.

Changamoto

Liundi anasema licha ya kuwa Serikali imejitahidi kutoa elimu bure kwa wanafunzi tangu shule za msingi na sekondari bado zipo changamoto nyingi zinazokwamisha jitihada hizo.

“Changamoto hizi zikimalizika tunaweza kufikia malengo madhubuti ya kumkomboa mwanamke,”anasema.

Anafafanua kuwa elimu bure inayotolewa na Serikali, lazima iende sambamba na miundombinu itakayomwezesha mtoto wa kike kupata elimu hiyo.

Ndoa na mimba za utotoni

Wakati wanawake wanaadhimisha siku ya mwanamke, Tanzania inatajwa kuwa moja kati ya nchi zenye viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni.

Liundi anasema kati ya vitu vinavyokwamisha elimu kwa mtoto wa kike ni ongezeko la ndoa na mimba za utotoni.

Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti uliochapishwa mnamo Januari, 2016 liliitaja Tanzania kuwa ni kati ya nchi tatu barani Afrika kwa ndoa na mimba za utotoni kwa asilimia 28.

Pia, Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), linasema kwa wastani watoto wa kike wawili kati ya watano huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Takwimu za utafiti wa Idadi ya watu na Afya Tanzania (TDHS, 2010) zilibaini kuwa asilimia 37 ya watoto wa kike Tanzania huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Shirika la Watoto Duniani (UNICEF 2012) liliainisha mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni kuwa ni Shinyanga (59), Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48) na Morogoro (42),

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ambaye pia ni balozi wa kampeni ya ‘Msichana wa Kitaa’ Julieth Frank anakiri kuwa mimba na ndoa za utotoni ni kikwazo kwa wasichana kufikia ndoto za maisha yao.

“Nilifanya utafiti wangu Morogoro, nimegundua mambo mengi kubwa ni wasichana wengi kuacha shule kwa sababu ya ndoa na mimba. Kama kweli tunataka kumkomboa mtoto wa kike, lazima tupambane na vikwazo hivi,”anasema.

Julieth anasema wasichana wengi huingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa sababu nyingi, ikiwamo kudanganywa, ugumu wa maisha, kutojua elimu ya afya ya uzazi, mila pamoja na desturi potofu.

Anasema kupitia kampeni ya ‘Binti wa Kitaa’ amebaini kuwa wapo wasichana wengi waliokatisha masomo yao kwa sababu hizo, jambo linalokwamisha ndoto ya kumkomboa mwanamke kifikra.

Msichana aliyewahi kuacha shule kwa sababu ya mimba, Jesca Silsa anasema angetamani kuona wasichana waliopata mimba wanaendelea na masomo.

Ukatili wa kijinsia

Kipigo, ubakaji, utumikishwaji na vitendo vingine vya kikatili dhidi ya watoto wa kike, vimekuwa vikiwanyima fursa ya kupata elimu.

Liundi anasema ikiwa ukatili wa kijinsia utakomeshwa miongoni mwa jamii, watoto wa kike watafikia ndoto yao.

Mwanafunzi Julieth anasema hakutakuwa na haja ya kusherehekea siku ya mwanamke duniani wakati ambapo watoto wa kike wanaachwa nyuma kielimu.

“Binafsi wazazi wangu walinisomesha na sasa nipo chuo kikuu. Nimeshuhudia wasichana wenzangu wengi wakiacha shule kwa sababu ya vitendo vya ukatili, hiki ni kikwazo,”anasema.

Mkakati wa Serikali

Akizungumza katika mkutano wa kujadili masuala ya wanawake uliokuwa umeandaliwa na TGNP, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto na Walemavu, Ummy Mwalimu, anasema Serikali imezingatia usawa katika usaili wa wanafunzi kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo.

“Usawa kwenye elimu utatufikisha mahali pazuri,” anasema.

Pia, ipo mikakati mingi ya Serikali katika kufikia malengo ya kumkomboa mwanamke.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni mpango kazi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliozinduliwa mwaka jana, ukilenga kupambana na mambo yanayokwamisha jitihada za wanawake kufikia malengo yao.

Anasema Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu na kupunguza ukatili wa mabinti kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Ummy anasema Serikali ina mpango wa kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 13, kupunguza ukatili asilimia 39 mpaka asilimia 20 na kupunguza ukatili wa kingono kwa watoto wa kike kutoka asilimia 33 hadi kufikia asilimia 16 na kwa watoto wa kiume kutoka asilimia 14 hadi asilimia saba.

Faida za kumsomesha mtoto wa kike

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Tawama), Martina Mgilundi anasema kumsomesha mtoto wa kike ni njia sahihi ya ustawi wa jamii.

“Faida ya kumsomesha mtoto wa kike inaanzia kwa mtoto wa kike mwenyewe, jamii inayomzunguka na Taifa zima. Mwanamke aliyesoma anajiamini, haburuzwi ovyo. Ana maamuzi yaliyo sahihi,”anasema.