TEHAMA: Ushindani wa teknolojia kwenye simu
Muktasari:
- Kuanzia vioo vinavyopinda mpaka betri zinazoweza kukaa kwa miezi kadhaa, teknolojia kwenye simu za mkononi inazidi kubadilika.
- Zifuatazo ni baadhi ya teknolojia za miaka ijayo zinazokaribia kuingia sokoni kwa ajili ya wateja mbalimbali.
Teknolojia inazidi kubadilika siku hadi siku. Kila kampuni inajitahidi kuja na teknolojia mpya au kuboresha zilizopo ili kudhibiti masoko yake na hata kuvutia mengine sehemu mbalimbali za dunia.
Kuanzia vioo vinavyopinda mpaka betri zinazoweza kukaa kwa miezi kadhaa, teknolojia kwenye simu za mkononi inazidi kubadilika.
Zifuatazo ni baadhi ya teknolojia za miaka ijayo zinazokaribia kuingia sokoni kwa ajili ya wateja mbalimbali.
Kuingia maji ni moja ya changamoto kubwa kwa vifaa vya elekroniki. Kwa sasa, kuna kampuni nyingi zinazofanya utafiti ili kutengeneza vifaa vya elekroniki visivyoingia maji kwa kutumia teknolojia ya ‘nanocoating’ kwenye vifaa vya ndani ya simu.
Teknolojia hii itafanya vifaa hivyo visiguswe na maji. Nina matumaini utafiti kuhusu suala hili utafanikiwa na kutengeneza bidhaa kama simu, komputa na vifaa vingine visivyoweza kuingia maji.
SamSung na LG tayari wana simu zenye uwezo wa kujikunja. Hata hivyo, mwonekano wa kioo ndio sababu kubwa ya vifaa vingi tunavyotumia leo hii; inahitajika sehemu iliyonyooka ili kioo kitoshe. Lakini kama kioo kingeweza kujikunja, ungeweza kubuni mwenyewe mwonekano wa kifaa na hata kuikunja na kuifunga kwa ajili ya kuhifadhi.
Samsung na LG wameshafanya majaribio ya vioo vinavyojikunja maarufu kama ‘Flexible screens’ na utafiti unaonyesha vitatumia umeme kidogo kuliko vile vya kawaida.
Kampuni ya Westen Digital ina bidhaa inayoitwa WD Livewire; hii ni adapta inayofanya kazi kama kiunganishi cha intaneti. Kama nyumba yako imefanyiwa mfumo mzuri wa umeme, huna haja tena ya kutumia waya nyingine za fiber au modem kwa ajili ya intaneti.
Ukitumia kifaa hicho utaweza kuchaji kompyuta yako na vile vile kupata huduma ya intaneti kwa mwendo uleule. Teknolojia hii kwa sasa inaitwa ITPL au Internet through power lines.
Wengi tunabeba vifaa vingi kwa wakati mmoja kuanzia simu, iphone, kompyuta mpakato huku vyote hivyo vikiwa na kifaa chake cha kuchajia.
Ingawa vingi vinatumia mfumo wa USB, unahitaji kutumia waya ili umeme uingie. Lakini sasa baadhi ya watengenezaji wa vifaa hivyo wameanza kuweka kifaa kinachowezesha kuchaji bila waya maarufu kama ‘Wireless charging.’
Kamera nyingi tunazotumia kwa ajili ya upigaji picha zinahitaji mtu anayeweza kukaa eneo zuri ili kupata picha nzuri. Hivi sasa mambo yameanza kubadilika, kampuni ya LYTRO ina kamera inayoweza kubadilika kwa kubonyeza kitufe.
Huna haja tena ya kukaa sehemu nzuri, kamera hii inachukua taarifa zote muhimu kuhusu picha na mwanga wote. Aidha, hauhitaji flashi wala 3D. Kampuni za kutengeneza simu kama QIKU, XOLO na Huawei zimeanza kutengeneza simu zenye kamera hii.
Kwa kawaida, betri inaweza kukaa siku moja au mbili, lakini fikiria upate betri unayoweza kuichaji mara moja kwa mwaka! Hii inawezekana kwa kutumia teknolojia ya fuel cell ambayo inazalisha umeme unaokaa muda mrefu kuliko zile betri zinazotumia madini ya liion na alkaline.
Betri hizi zinaendelea kufanyiwa utafiti na majaribio; zinategemewa kutumika katika vifaa kama simu, kompyuta na vinginevyo.