MAONI YA MHARIRI: Watanzania waungane kumaliza ukatili dhidi ya watoto

Muktasari:
Kipindi cha nyuma mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya kimataifa hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), yaliwahi kufanya utafiti kwa nyakati tofauti mitaani na shule za msingi na walibaini ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Tatizo la vitendo vya ukatili kwa watoto limezidi kuwa kubwa na takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kipindi cha Januari mpaka Julai, jumla ya matukio 2,571 ya watoto kufanyiwa ukatili yaliripotiwa.
Kipindi cha nyuma mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya kimataifa hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), yaliwahi kufanya utafiti kwa nyakati tofauti mitaani na shule za msingi na walibaini ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Lakini, taarifa mpya iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeweka wazi kiwango cha ukatili kwa watoto kinavyofanyika mikoani, Dar es Salaam iliyopimwa kwa wilaya inaonyesha hali ni mbaya na kama hakutafanyika juhudi za pamoja kwa kuwachukulia hatua za kisheria wahusika kiwango cha vitendo hivyo viovu kitazidi kuongezeka.
Wilaya tatu za Dar es Salaam zina idadi kubwa, kwani Kinondoni inaongoza kwa idadi ya watoto 187 ikifuatiwa na Temeke watoto 187 na Ilala 109.
Polisi kwenye taarifa yao waliitaja mikoa mingine yenye idadi kubwa kuwa ni Mbeya 177, Morogoro 160, Pwani 159 na Tanga 111. Siyo sifa kwa mikoa kutajwa kushika nafasi za juu kwenye vitendo viovu, hasa vya ukatili dhidi ya watoto.
Kinachosikitisha zaidi ni maeneo vinakofanyika vitendo hivyo na kwa mujibu wa takwimu za polisi, asilimia 49 ya vitendo hivyo vinafanyika nyumbani na wahusika wa unyama huo ni ndugu na jamaa, wakati asilimia 29 ya watoto walifanyiwa ukatili njiani kati ya shule na nyumbani na asilimia 15 walifanyiwa eneo la shule.
Tunaamini maeneo yote hayo yana watu wazima nyumbani wako wazazi, walezi na majirani, njiani wako wapita njia ambao ni watu wazima na shule kuna walimu. Tunajiuliza ule msemo wa ‘mtoto wa mwenzio ni mwanao’ uko wapi?
Lakini, kinachoonekana vitendo hivi kwa asilimia kubwa vinaanzia nyumbani jambo ambalo ni hatari zaidi, hata baadhi ya kesi zilizopo polisi zinaonyesha wahusika wengi wa vitendo hivyo ni ndugu na jamaa na linapojulikana viongozi ndani ya familia ndiyo huwa wa kwanza kutaka suluhu nje ya mkondo wa sheria. Tunajiuliza kama hali ni hiyo makuzi mema ya mtoto yatasimamiwa na nani.
Utafiti uliofanywa na shirika moja lisilo la kiserikali ulibainisha kuwa hata kesi zilizopo polisi nyingi zilishindikana kuendelea hatua ya mahakama, kwa sababu wahusika hasa ndugu wamekuwa wagumu kutoa ushirikiano wa kumchukulia hatua muhusika.
Tunaamini kama mshikamano ungekuwapo kati ya wazazi, walezi, viongozi wa dini, walimu shuleni na polisi vitendo hivi vingepungua kwa kiasi kikubwa kama si kuisha kabisa.
Polisi wanapotoa takwimu hizo hatudhani kama ni sifa kwao na hata wao hawaoni sifa kila mara kutangaza ongezeko la vitendo hivyo, wangependa zaidi wawe na takwimu za watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kuhukumiwa vifungo jela.
Watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo ni taifa la kesho, kuna haja ya kuungana kuwalinda watoto hao dhidi ya watu wachache wanaotaka kuwaharibia maisha yao. Pia, hatua kali za kisheria zinapaswa kuchukuliwa bila kuoneana aibu hata kama ndugu watataka kupindisha sheria.