Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NANI NI NANI SERIKALI YA JPM?- Balozi Ombeni Sefue-Katibu Mkuu Kiongozi

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue      

Muktasari:

Balozi Sefue ana miaka 61 hivi sasa na ifikapo Agosti atatimiza miaka 62 kwani alizaliwa Agosti 26, 1954 katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Historia na Elimu

Balozi Ombeni Yohana Sefue ndiye Katibu Mkuu Kiongozi (Chief Secretary) katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa na kuapishwa kushikilia wadhifa huo katika Serikali ya Rais John Magufuli. Yeye ni mtaalamu wa usimamizi wa umma na mwanadiplomasia mwenye uzoefu mkubwa.

Balozi Sefue ana miaka 61 hivi sasa na ifikapo Agosti atatimiza miaka 62 kwani alizaliwa Agosti 26, 1954 katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na sekondari ya juu hapa nchini Tanzania alijiunga na Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo - Mzumbe (sasa Chuo Kikuu Mzumbe) kusoma Stashahada ya Juu ya Usimamizi wa Umma na Sera (Stashahada hiyo ni sawa na shahada ya kwanza inayotolewa hivi sasa) na alihitimu mwaka 1977.

Kisha, alikwenda nchini Uholanzi kwa ajili ya masomo ya juu zaidi na mwaka 1981 akahitimu Shahada ya Uzamili ya Sera na Usimamizi wa Umma kutoka Taasisi ya Masomo ya Jamii iliyoko jijini The Hague.

Mwaka 1984, alisoma na kuhitimu mafunzo ya Usuluhishi wa Kimataifa kutoka Shule ya Kimataifa ya Amani (International Peace Academy) na mafunzo ya changamoto za kuchumi na kijamii katika nchi zinazoendelea kutoka taasisi ya International Relations and Socialist Integration with the Presidium of the Bulgarian Academy of Sciences.

Mwaka 1986 alipata mafunzo katika ngazi ya cheti cha Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia kutoka Kituo cha Mafunzo ya Diplomasia cha Tanzania na Msumbiji (sasa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam).

Uzoefu

Alikuwa mwanadiplomasia na mshauri katika Ubalozi wa Tanzania mjini Stockholm, Sweden kati ya mwaka 1987 hadi 1992. Akiwa hapo alipata bahati ya kufanya kazi za kibalozi zikihusisha nchi za Denmark, Norway, Finland na Iceland.

Kati ya mwaka 1993 na 2005, alifanya kazi ya uandishi wa hotuba na Msaidizi kwa Marais wawili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi (1993-1995) na Benjamin Mkapa (1995-2005) na ni wakati huo alipohudumu katika nafasi ya Katibu Binafsi wa Rais (Mkapa).

Mwaka 2002 hadi 2004 aliendelea kufanya kazi na Mkapa aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Kamisheni ya Masuala ya Kijamii na Utandawazi iliyokuwa chini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Balozi Sefue ndiye aliyesimamia uandaaji wa taarifa ya “Utandawazi wa Haki; Fursa kwa Wote” (Tafsiri yangu). Ripoti hii ilitolewa mwaka 2004.

Mwaka 2005, alimsaidia Mkapa alipokuwa aMkuu wa Kamisheni ya Afrika (Kamisheni ya Tony Blair) ambayo ilizalisha ripoti iitwayo; “Mfanano wa Masilahi Yetu; Ripoti ya Kamisheni ya Afrika ya mwaka 2005” (tafsiri yangu) na wakati huo Balozi Sefue alishiriki kwa karibu katika vikao vya wakuu wa nchi vya G8 wakati ripoti hiyo inajadiliwa mjini Gleneagles, Scotland Julai 2005.

Kwa ujumla, miaka 13 ya kufanya kazi chini ya marais wawili ilimpatia uzoefu wa kutosha. Ameshiriki kwa kina katika masuala mbalimbali ya uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Amekuwa na uzoefu pia wa utatuzi wa migogoro ambao aliupata wakati wa Mkapa na alishiriki moja kwa moja katika kutafuta suluhu ya migogoro ya Nchi za Maziwa Makuu na kushiriki kwenye mikutano ya kimataifa ukiwamo ule wa uchumi uliofanyikia Davos na Afrika Kusini, Jukwaa la “Sino – African” pamoja na mchakato wa “Ticad”.

Ndani ya nchi, Balozi Sefue alimsaidia Rais Mkapa kwa kufanya kazi na taasisi kadhaa za kimataifa kama vile Taasisi ya Hernando de Soto’s iliyojihusisha na masuala ya uhuru na demokrasia, Taasisi ya Rais Clinton iliyojihusisha na uanzishwaji wa taasisi za kupambana na Virusi vya Ukimwi na Ukimwi. Ameshiriki kwenye mchakato wa mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa kwa kuweka msisitizo kwenye uchumi mkubwa na mazingira ya kibiashara wakati wa Mkapa.

Oktoba 2005 hadi Juni, 2007 Sefue aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na mwakilishi huko Cuba. Juni 2007 hadi Agosti, 2010 akawa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na mwakilishi huko Mexico. Agosti 31, 2010 akateuliwa kuwa Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa jijini New York. Kwa kipindi cha Oktoba 2010 hadi Desemba 2012 , BaloziSefue alishikilia wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirikiano wa Kuondoa Njaa na Umaskini barani Afrika ambayo makao makuu yake ni jijini Washington, Marekani.

Balozi Sefue aliapishwa kwa mara ya kwanza kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Disemba 31, 2011. Kwa nafasi yake, ndiye Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma. Alianza kazi Januari Mosi, 2012 hadi Novemba 2015. Kuanzia Januari 2012, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Biashara. Desemba 30, 2015 Rais JPM alitangaza orodha mpya ya makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao na kwenye nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi aliendeleza uteuzi wa Balozi Sefue.

Wadhifa huu wa Katibu Mkuu Kiongozi katika Katiba unatambulika kama “Katibu wa Baraza la Mawaziri”. Ibara ya 60 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imeeleza; “Kutakuwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri ambaye atakuwa ndiye mtendaji mkuu katika Ofisi ya Baraza la Mawaziri na atatekeleza shughuli zifuatazo kwa kufuata maagizo ya jumla au maalumu atakayopewa na Rais, yaani: (a) kuandaa ratiba ya mikutano ya Baraza na kutayarisha orodha ya shughuli za kila mkutano; (b) kuandika na kuweka kumbukumbu za mikutano ya Baraza; (c) kutoa taarifa na maelezo ya uamuzi wa Baraza kwa kila mtu au chombo cha umma kinachohusika na uamuzi wowote; na (d) kutekeleza kazi na shughuli nyingine zozote atakazoagizwa mara kwa mara na Rais”.

Nguvu

Kwanza, kwa sababu ukatibu mkuu kiongozi ni kazi ya usimamizi wa utendaji - inahitaji mtu mwenye uzoefu wa kukaa serikalini muda mrefu. Naam, Sefue amekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 39 sasa (miongo minne). Hili peke yake linamfanya kuwa na vigezo vyote vya kuongoza watendaji na watumishi wa umma serikalini kwa ufanisi.

Weledi wake katika masuala mengi ya jumla, kufanya kazi chini ya marais wawili kabla ya Dk Magufuli kunampa kila sababu ya kuwa mtu muhimu ki-kumbukumbu na ki-miongozo kwa Rais aliyepo hivi sasa. Masuala ya kuongoza taasisi ya urais siyo kubahatisha, kunahitaji uamuzi thabiti unaotokana na uzoefu na kumbukumbu zilizo wazi. Watendaji walio karibu naye wanasema anazo sifa hizi muhimu.

Mwisho, kwa sababu Dk Magufuli si mweledi wa masuala ya kimataifa na licha ya kuwa na Waziri wa Mambo ya Nje mwenye upeo mkubwa, lakini akiwa Ikulu, alihitaji kuwa na mtu mwenye uelewa mpana na aliyeyaishia maisha ya siasa za kimataifa. Jambo hili pia linambeba kwa sababu amekulia katika dipolomasia na anayo nafasi ya kuwa mshauri mkubwa wa kila siku wa Rais katika masuala ya dharura ya kidiplomasia hata kama Waziri wa Mambo ya Nje amesafiri.

UDHAIFU

Jambo la kipekee ambalo limetia doa utendaji wa Balozi Sefue ni kushiriki katika “kumsafisha” aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi dhidi ya kashfa ya Escrow.

Balozi Sefue alimsimamisha kazi Maswi kwa muda kuanzia Desemba 23, 2014, kwa kutumia madaraka aliyonayo akiwa mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa wmma wanaoteuliwa na Rais, wakiwamo makatibu wakuu ili kupisha uchunguzi dhidi yake.

Mei 8, 2015 alitangaza matokeo ya uchunguzi na kueleza kuwa Maswi hakutenda kosa lolote la kinidhamu katika sakata hilo. Uamuzi au matokeo ya uchunguzi wake uliibua maswali na minong’ono mingi miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala ya utawala bora na nidhamu ndani ya Serikali na wengi walimkosoa wakisema hakutoa sababu za kutosha za kwa nini Maswi hana hatia wakati wakubwa wake wanashinikizwa kujiuzulu.

Matokeo ya uchunguzi wa juu ya Maswi yaliwakumbusha wafuatiliaji wa mambo juu ya uchunguzi mwingine uliowahi kufanywa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Philemon Luhanjo juu ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini David Jairo ambaye alidaiwa kuhusika kukusanya fedha za kwenda kuwahonga wabunge ili kurahisisha upitishwaji wa bajeti ya wizara hiyo lakini baadaye Luhanjo akatangaza kuwa Jairo hana hatia. Wachambuzi walianza kutilia shaka mwendelezo huu wa makatibu wakuu viongozi na kuanza kujenga shaka kuwa huenda wadhifa huu unatumika kuwalinda watendaji wabovu badala ya kuwarudisha kwenye nidhamu.

Jambo la pili dogo lililohojiwa na kuchukuliwa kama udhaifu wa kiongozi huyu ni kuhusu sakata la vitanda vya muhimbili ambalo liliibuka mwishoni mwaka jana. Baada ya Rais JPM kuagiza Sh250 milioni zilizopunguzwa kutoka kwenye michango ya kuwapongeza wabunge zitengwe na kununua vitanda, Balozi Sefue alionekana kuwa mstari wa mbele kusimamia mchakato huo kwa nguvu hata katika mambo madogo ambayo angeliwatuma watendaji wake wakayakague pale Muhimbili.

Wengi walishangazwa kwani kwa miaka yote aliyokuwa Katibu Mkuu Kiongozi alionekana akisimamia majukumu makubwa ya Ikulu kuliko yale ya hadhi ya usimamiaji wa ufungaji wa vitanda. Wakosoaji wake walieleza kuwa huenda hiyo ilikuwa mbinu ya kumuonyesha Rais JPM kuwa yeye ni mtendaji imara. Wengi walishangaa kwani anafahamika kama mtendaji imara na wala hahitaji kujitwisha majukumu ambayo angetuma watendaji wa chini. Hizo ni dalili mbovu katika kujiamini kwa kiongozi.

Mwisho, hivi sasa anaonekana kuanza tabia ya “u-kasuku”, hata kwa mambo madogo yasiyomhusu. Mathalan, baada ya Dk Makongoro Mahanga (aliyekuwa Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi chini ya CCM) kutoa “kaandiko” kadogo akikosoa uteuzi wa makatibu wakuu wengi, aliamua kumjibu tena kwa lugha za “ki-mipasho”. Hali ile ilitafsiriwa na wakosoaji wake kwamba ameanza kuonyesha dalili za kutaka kuwa msemaji wa Ikulu badala ya kuwa msimamizi wa Ikulu. Hali hiyo ikiendelea ina maana kutakuwa hakuna haja tena ya kuwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu.

Matarajio

Matarajio ya Balozi Sefue ni kutumia uhuru wa kiutendaji wa mkubwa wake wa kazi ili kujiwekea rekodi ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi bora kuliko wote wa hivi karibuni. Hilo linawezekana kwani mwelekeo wa Serikali aliyomo umekwishaonyesha dalili za kutoa fursa hiyo.

Watumishi wa umma na watendaji wengine wa Serikali wanaamini kuwa uzoefu wake kwenye nafasi hii ni wa muda mrefu na bila shaka anaijua Ikulu kuliko mtu yeyote kwa zama za sasa, anajua pia mianya ya utendaji mbovu na watumishi wazembe na waliopewa mamlaka makubwa au wasiowasimamia ipasavyo walio chini yao. Kazi ya kuchukua hatua akishirikiana na Rais ndilo tarajio la kipekee huku mitaani.

Changamoto

Changamoto ya kwanza ambayo itakuwa inamkabili ni namna ya kuratibu masuala ya Baraza la Mawaziri. Siku hizi mambo yote yanayozungumziwa kwenye Baraza la Mawaziri hata kabla halijaisha yanakuwa yamezagaa mitaani. Utaratibu huo haukuwapo enzi za Mwalimu Nyerere, ukashamiri kipindi cha Mwinyi, ukaendelea lakini kwa kudorora kipindi cha Mkapa na ukasambaa kwa kasi ya upepo wakati wa JK. Tayari JPM ameshajenga misingi ya kufanya mambo kwa nidhamu ya siri kwa hiyo mwenye changamoto ya kuimarisha misingi hiyo ni Balozi Sefue.

Changamoto ya pili ni usimamizi wa Ikulu yenyewe. Hivi karibuni, Ikulu ya Tanzania imekuwa siyo mahali “patakatifu tena”, imekuwa siyo mahali pa heshima. Kila mtu anaweza tu kujiendea na kufanya anachotaka. Katika awamu iliyopita Rais JK alikuwa na kazi ya ziada ya kupokea kila mtu Ikulu, hata wale ambao inaonekana wamekwenda kusaka “ujiko”. Nasema kunapaswa kuwa na taratibu madhubuti za mtu kufika Ikulu. Haiwezekani mtu anataka tu kumsalimia Rais anafunga safari anakaribishwa anamsalimu Rais na kuondoka. Naamini JPM hawezi kuwa na muda huo wa kuchezea lakini naiona changamoto kwa Balozi Sefue kuondoa yale mazoea ya zamani, Ikulu ipokee wageni muhimu tu ili kumpa Rais muda wa kutosha kufanya mambo ya msingi.

Changamoto ya tatu iko kwenye kumpa rais ushauri sahihi. Hivi karibuni tumewahi kuona rais akisimama mahali na kuongea mambo yaliyokosewa kitakwimu au katika upeo wa ukweli. Hii inasababishwa na uwepo wa watendaji wenye uwezo mdogo au kuwa na watu wenye milengo ya aina moja katika taaluma.

Ni wakati muafaka sasa kwa Balozi Sefue kumshauri vizuri Rais ili awe na majopo ya washauri, kama ni uchumi asiwe na mshauri mmoja, ni bora kuwa na washauri watano au saba wa uchumi – wanaweza kuwa walimu wa chuo kikuu au vinginevyo. Kila panapotokea masuala yanayohitaji kufanya uamuzi wa kiuchumi, wanapewa na kujifungia siku kadhaa na kumshauri Rais kwa pamoja. Baadhi ya watendaji ambao nimezungumza nao serikalini wanasema tabia ya marais wetu kushauriwa na mtu mmoja kwenye sekta fulani, yamekuwa na madhara makubwa kwa kipindi kirefu kwani washauri hao hujikuta wakiweka misimamo ya milengo yao kitaaluma bila kujali kuwa milengo hiyo haina nafasi kwa dunia ya sasa na matokeo yake kilichoshauriwa kinakosa mashiko.

Changamoto ya nne ni usimamizi wa nidhamu za watendaji serikalini. Hili ni kubwa zaidi, mfano wa yaliyowahi kusimamiwa na ofisi yake wakati akiwapo na hata nyuma yake, ni uthibitisho tosha wa uozo unaoendelea serikalini. Yale ya Jairo na Maswi ni muhtasari tu, habari kamili zimejaa tele kila sekta. Kazi ya kusimamia watendaji ina changamoto za kipekee na inataka weledi, ujasiri na umakini wa kutosha. Anayo nafasi hivi sasa ya “kutumbua majipu” ya utendaji kwani anacho kibali na msaada wa mwajiri wake kwa hiyo jukumu lake kubwa kwa sasa ni kutengeneza mfumo ambao utasaidia majipu yatumbuliwe kila mkoa, kila wizara lakini kwa kufuata sheria na kutenda haki.

Kukiwa na mfumo wa udhibiti wa watendaji kwa haki kila kona ya nchi, hatutasikia michezo ambayo imekuwa ikiendelea kwa miongo kadhaa sasa.

Hitimisho

Huenda Balozi Sefue alikuwa na kiu ya kusimamia mambo makubwa wakati wa JK lakini akazuiwa na staili ya uongozi ambayo iliambatana na kujuana, kulindana na kutochukua hatua kwa mambo makubwa. Uwezo na uthabiti wa Balozi Sefue utajulikana hivi punde kwani yumo kwenye Serikali mpya ambayo imekuja na taratibu mpya za kupambana na wazembe, wala rushwa na mafisadi. Hana pa kujificha tena, ameshakuwa “exposed” (amewekwa hadharani) na sasa naamini kila mmoja ataijua rangi ya kiongozi huyu. Tumpe muda tujue mbivu na mbichi. Namtakia kila la heri.

*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi*

KUHUSU MCHAMBUZI

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Adv Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; [email protected]).