Shule aliyosoma Samia yatimiza miaka 133

Sehemu ya madarasa yaliyokarabatiwa shuleni hapo, ambaypo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuyazindua.

Ni zaidi ya karne na zaidi, Shule ya Sekondari Kizimkazi, bado inaendelea kuzalisha wanafunzi.

Mmoja wa wanafunzi waliopitia hapo ni Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye siku chache zijazo anatarajiwa kufika shuleni hapo kwa ajili ya kufungua majengo mapya yaliyofanyiwa ukarabati.

Mkuu wa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1910, Haji Juma Hamisi, anasema jumla ya Sh277milioni zimetumika katika ukarabati wa shule hiyo kongwe iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja.

“Shule ya Kizimkazi ina historia kubwa kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan amesoma hapa na baadaye alihamia shule nyingine, hivyo unaweza kuona ni shule ambayo imetoa viongozi bora kama tunavyomuona katika utendaji wake” anasema.

 Anasema ndani ya uzio wa sekondari hiyo kongwe, zipo shule mbili ambazo ni shule ya msingi Kizimkazi na shule ya awali.

Mwalimu Haji anasema mbali na rais Samia, yupo baba yake mzazi, marehemu Suluhu Hassan ambaye alikuwa ni miongoni mwa walimu waliofundisha shule hiyo.

Pia yupo, Abdulhamid Yahaya Mzee ambaye alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya awamu ya saba , Mohamed Haji Hassan(Mohamed Raha) ambaye alikuwa mshauri wa rais katika mambo ya siasa wa awamu ya saba na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kusini Unguja, Ali Rashid Suluhu.

Mwalim Haji anasema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 148, ufaulu wake wa kidato cha nne kwa mwaka jana ulikuwa ni asilimia 92, huku kimkoa ikishika nafasi ya nne wakati kitaifa ikishika nafasi ya 34 kati ya shule 205 zilizopo Unguja.

“Kati ya wanafunzi 27 waliofanya mtihani wa kudato cha nne, wanafunzi 26 walifaulu isipokuwa mmoja ndio alipata daraja sifuri,” anasema.

Kwa upande wake, mwalimu wa Shule ya msingi Kizimkazi, Mahafudhi Said Omary amesema shule hiyo ni miongoni mwa miradi inayotarajia kuzinduliwa na rais Samia Suluhu Hassani, Julai 31, 2023, wakati wa kilele cha tamasha la siku ya Kizimkazi .

“Mradi wa kwanza ulizinduliwa mwaka 2018/ 2019 ambopo ulikuwa ni ukumbi wa mikutano na kituo cha wanafunzi kufanyia mikutano pamoja na madarasa matano. Mwaka 2020 tulizindua madarasa manne kwa ajili ya wanafunzi wa chekechea, mwaka 2022 tulizindua jengo moja la maabara ya fizikia, kemia na bailojia” anasema mwalimu na kuongeza

“Mwaka 2023, pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua madarasa yetu 13 na vyumba viwili vya kompyuta vyote vipo hapa Kizimkazi” anasema.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa taasisi ya Tanzania Centre for Education (TCE) Yusuf Ogutu, anasema upo uhusiano mkubwa kati ya mazingira ya kujifunzia na ufaulu kwa wanafunzi wote wa kike na wale wa kiume.

“Huduma isiyoridhilsha hasa ya madarasa, maeneo ya kujisitiri inawanyima morali wanafunzi wote bila kujali jinsia. Mfano kama choo hakina matundu ya kutosha, hakina paa, hakina milango madhubuti ya kumhifadhi mtumiaji kwa wakati huo, hakina maji, mtumiaji hawezi kuwa huru kukitumia, hivyo kitendo cha kuboresha shule kongwe ni jambo la kupongezwa’ anasema Ogutu.

Sabra Ali Mohamed, ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanamke Initiative(MIF), anasema lengo lao ni kugusa maeneo makubwa manne visiwani Zanzibar ambayo ni elimu, afya ya akili, afya ya uzazi na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

‘‘Matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka jana katika sekondari ya Kizimkazi Mkunguni yameonyesha wazi jitihada zetu zimeanza kuzaa matunda ndani ya mkoa wa Kusini Unguja, kwani ufaulu umeongezeka na kufikia asilimia 92.’’