Historia ya Serikali za Mitaa na mkakati wa kupeleka madaraka kwa wananchi

What you need to know:

Mpaka hivi sasa sehemu ya utawala bora katika Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa iliandaa zaidi ya vipindi 312 vya robo saa kwa kila kipindi kuhusu uboreshaji wa mfumo na taratibu za uendeshaji wa Serikali za Mitaa.

Majuma kadhaa sasa tumekuwa tukielezea historia ya Serikali za Mitaa nchini. Leo tunaendelea na mfululizo wa makala yale tukiangalia utekelezaji wa uamuzi ulioidhinishwa na Serikali kuhusu mpango wa uboreshaji wa mfumo wa Serikali za Mitaa na mkakati wa kupeleka madaraka kwa wananchi.

Kabla ya kuanza kutekeleza mpango wa uboreshaji wa ufumo wa Serikali za Mitaa, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira ya kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.

Ilipitisha mambo kadhaa ikiwamo Sheria mpya ya Tawala za Mikoa, Sera ya Uboreshaji wa Serikali za Mitaa, mabadiliko ya Sheria za Serikali za Mitaa na kuidhinisha uboreshaji wa mfumo wa Serikali za Mitaa pamoja na mkakati wa utekelezaji wake.

Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ulianza kutekelezwa rasmi Januari, 2000 katika Halmashauri 38 za awamu ya kwanza.

Katika tathmini ya utekelezaji wa mpango huo iliyofanyika mwaka 2001, pamoja na mambo mengine, ilishauriwa kuwa mpango utekelezwe nchi nzima kwa yale mambo ambayo hayakuhitaji matumizi ya fedha nyingi; na mambo mengine yaliyohitaji utafiti na fedha nyingi yatekelezwe hatua kwa hatua.

Mpango ulitekelezwa katika halmashauri zote 114 na utekelezaji huu ulikwenda sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Uboreshaji wa Utendaji Serikalini (PSRP) ambao uliishia mwaka 2011.

Lengo kuu lilikuwa ni kupunguza idadi ya Watanzania waishio katika umaskini kwa kuboresha wingi na ubora wa huduma zitolewazo kwa wananchi na hasa wale maskini.

Maelekezo ya Serikali kwamba wananchi waelimishwe kuhusu Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa yamekuwa yanatekelezwa kuanzia Januari mosi mwaka, 2000 kwa njia ya vipindi vya redio na televisheni pamoja na makala za magazeti.

Mpaka hivi sasa sehemu ya utawala bora katika Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa iliandaa zaidi ya vipindi 312 vya robo saa kwa kila kipindi kuhusu uboreshaji wa mfumo na taratibu za uendeshaji wa Serikali za Mitaa.

Mbali ya vipindi vya Madaraka kwa Umma vilivyoandaliwa na kutangazwa kila wiki, sehemu ya Utawala Bora katika Programu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ilikuwa ikishirikiana na Taasisi za Redet na IDS za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vikundi mashuhuri vya sanaa kuandaa vipindi vya majadiliano na michezo ya maigizo kwa njia ya redio na televisheni.

Lengo ni kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kutumia haki zao za kiraia kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za Kiserikali na katika hatua zote za uchaguzi wa uongozi wa ngazi mbalimbali za utawala na uongozi.

Pia makala mbalimbali kuhusu maeneo muhimu ya uboreshaji mfumo wa Serikali za Mitaa ziliandikwa na kuchapishwa kwenye magazeti ya Kiswahili na Kiingereza yanayosomwa na watu wengi.

Kwa kutumia njia zote hizo, programu iliweza kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu maana, malengo na mikakati ya utekelezaji wa Progaramu ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa na nafasi yao katika uhitimishaji wa lengo kuu la programu hii.

Kuwahamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za Kiserikali ikiwa ni pamoja na kuhudhuria na kushiriki mikutano ya wakazi wa maeneo wanamoishi.

Kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo yao wenyewe katika maeneo wanamoishi na ya nchi kwa jumla.

Mbali ya kuwaelimisha, kuwafahamisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu haki na majukumu yao kwa kupitia sehemu ya utawala bora, programu iliandaa na kuwezesha ufafanuzi wa kanuni.

Taratibu na miongozo ifuatayo inayoendana na usimikaji wa misingi ya utawala bora katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa zilifanya kazi ya uandaaji na ufafanuzi wa taratibu na miongozo kuhusu uchaguzi wa viongozi katika ngazi ya msingi (mtaa, kitongoji na kijiji).

Vile vile kulikuwa na uandaaji na ufafanuzi wa kanuni za maadili ya madiwani, uandaaji wa ufafanuzi wa taratibu za uendeshaji wa shughuli za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora (uongozi wa demokrasia, utawala wa sheria, haki, usawa, ushirikishwaji wa Wananchi, uadilifu, usikivu, ufanisi katika kufanya na kutekeleza uamuzi, uwazi na uwajibikaji).

Kulifanyika pia uandaaji na ufafanuzi wa taratibu za utawala bora katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa, uandaaji na ufafanuzi wa maelezo ya msingi kuhusu uandaaji wa mipango na bajeti shirikishi kuanzia ngazi za msingi hadi ngazi ya halmashauri.

Pia uandaaji na ufafanuzi wa mwongozo kuhusu maandalizi ya mipango ya utekelezaji wa mapambano dhidi ya rushwa katika ngazi ya halmashauri.

Mengine ni kuongezeka kwa ari na ushiriki wa wananchi katika mikutano ya wakazi wa mitaa, vitongoji na vijiji na kwa ushiriki wao, katika kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya mahali wanamoishi, kama inavyodhihirika katika upangaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.