Ijue historia ya Serikali za mitaa Tanzania-2

What you need to know:

Kuanzishwa kwa uchaguzi wa madiwani katika halmashauri zote zilizokuwa zimeandikishwa na serikali ya kikoloni, Kuundwa kwa Halmashauri katika wilaya au miji ambayo zilikuwa hazijaundwa.

Serikali za mitaa ni chombo cha utawala wa umma, kilichopewa madaraka ya kuamua na kuendesha shughuli zake katika sehemu ndogo ya nchi au Taifa. Ifuatayo ni sehemu ya pili ya makala inayoelezea historia ya Serikali za mitaa Tanzania.

Baada ya uhuru, Serikali za baadhi ya nchi za Afrika kama vile Zaire (Congo Kinshasa), Uganda, Senegal na nyingine nyingi ama zilifuta mfumo wa serikali za mitaa au kubadilisha mfumo wake ulioanzishwa na Serikali za Kikoloni.

Kwa mfano, Serikali ya Tanganyika ya wakati huo haikufuta mfumo huo mara moja. Badala yake ilizirithi serikali za mitaa na kuzitumia kama nyenzo za kuleta maendeleo kwa misingi ya kidemokrasia.

Katika kipindi cha miaka ya mwanzo ya uhuru, yalikuwapo makundi matatu ya serikali za mitaa. Miongoni mwao ni zile zilizoundwa chini ya Sheria Namba 72 ya mwaka 1926 zilizokuwa 47.

Aidha, chini ya Sheria Namba 333 ya mwaka 1953, zilikuwa 9 kwa mijini na 10 kwa vijijini.

Kundi la tatu lilikuwa ni la Manispaa ya Dar es Salaam, iliyoundwa na Sheria Na. 105 ya mwaka 1946.

Mwaka 1962 Sheria na 333 ilirekebishwa kwa kuondoa mamlaka za wenyeji na mwaka 1963 Sheria Namba 13/62 ilipitishwa kusitisha utawala wa machifu nchini.

Inaelekea kuwa uamuzi wa kufuta utawala wa machifu nchini ulitokana na sababu kuu tatu. Serikali ya wananchi ilitaka kujenga mfumo wa kidemokrasia wa Serikali za mitaa. Aidha, ilionekana utawala wa machifu uliendeleza fikra za ukabila badala ya utaifa. Pia ikumbukwe kwamba wengi wa machifu waliwekwa madarakani na serikali ya kikoloni.

Kwa mantiki hiyo, machifu walikuwa kama mawakala wa serikali ya kikoloni. Mfumo huu usingeweza kukubalika katika Serikali iliyochaguliwa na wananchi.

Serikali ya wananchi ilikuwa na sera yake madhubuti juu ya serikali za mitaa. Ilibidi ichukue hatua kadhaa katika kutekeleza sera hiyo. Na hatua zilizochukuliwa ni:-

Kuanzishwa kwa uchaguzi wa madiwani katika halmashauri zote zilizokuwa zimeandikishwa na serikali ya kikoloni, Kuundwa kwa Halmashauri katika wilaya au miji ambayo zilikuwa hazijaundwa.

 

Mafanikio ya Serikali za mitaa 1961- 1972

Katika kipindi kati ya mwaka 1962 na 1972 Serikali za mitaa zilipata mafanikio machache na matatizo kuwa mengi.

Majukumu ya halmashauri yaliongezeka kama vile usimamizi wa elimu ya msingi, matibabu, barabara na maji.

Ingawa halmashauri za wilaya zilikuwa na majukumu mazito zaidi kuliko yale ya halmashauri za miji, inashangaza kuona kuwa sehemu kubwa ya ruzuku kutoka Serikali Kuu kwenda kwa Serikali za mitaa ilitolewa kwa halmashauri za miji.

Licha ya hali hiyo ya upendeleo kwa halmashauri za miji, kwa jumla halmashauri za wilaya ziliweza kutekeleza majukumu yake vizuri kwa kujikusanyia mapato kutokana na kodi na ushuru wa mazao na wakati huo huo kuhudumia miradi mbalimbali ya huduma za jamii.

Katika kipindi hiki mapato ya halmashauri yalishuka sana. Kushuka kwa uwezo wa halmashauri za wilaya kukusanya mapato ni ishara ya kukumbwa na matatizo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hivyo, halmashauri zikashindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Hali hiyo ndiyo iliyojitokeza kwa serikali nyingi za mitaa katika kipindi hiki cha mwaka 1962-1972. Matatizo yaliyozikabili serikali za mitaa yalitokana na sababu zifuatazo:

Kama ilivyoelezwa hapo awali kwamba, serikali za mitaa zilipewa majukumu mara baada ya uhuru na kwamba Serikali Kuu ilikuwa na nia ya kuleta maendeleo ya haraka kwa watu wake. Lakini vyanzo vya mapato kwa Serikali za mitaa vilikuwa vichache.

Halmashauri za wilaya, kwa mfano, ziliruhusiwa kukusanya mapato kutokana na kodi na ushuru wa mazao.

Ukusanyaji wa kodi kutoka kwa wananchi ulikuwa mgumu. Wananchi wengi walikuwa wakikwepa kulipa kodi ya kichwa.

Ilikuwa kama kero kwao na kusababisha matukio ya aibu na hata maafa. Kutokana na matukio hayo, Serikali Kuu iliamua kufuta kodi ya kichwa.

Aidha, ilipofika Mei, 1969 ushuru wa mazao nao ulifutwa. Uamuzi huo katika masuala mawili uliathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali za mitaa nchini.

Licha ya kwamba Serikali za mitaa zilitegemea zaidi misaada na ruzuku kutoka Serikali Kuu baada ya vyanzo kadhaa vya mapato yake kufutwa, pia katika kipindi hicho hicho Serikali Kuu ilipunguza ruzuku kwa serikali za mitaa.

Uamuzi huu ulitokana na sababu kwamba Serikali Kuu ilichukua baadhi ya majukumu ambayo hapo awali yalikuwa ya serikali za mitaa. Mifano ya majukumu hayo ni ulipaji wa mishahara ya walimu wa shule za msingi wa Daraja “A” na “B” na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kusomea.

Wizara nyingine, kama Afya, Ujenzi na Madini nazo pia zilichukua baadhi ya majukumu ya Serikali za Mitaa. Kutokana na upungufu wa mapato, halmashauri nyingi zilishindwa kutekeleza majumumu yao kwa ufanisi, hali ambayo ililaumiwa sana na Serikali Kuu.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.