Kilio cha Musukuma na taswira halisi ya kisiwa cha Kerebe

Muktasari:
- Jambo moja liko wazi kwamba katika operesheni za kukamata zana hizo na uteketezaji wake, wanasiasa wa maeneo husika, wakiwamo madiwani na wabunge, wanakwepa kushiriki ili kulinda masilahi yao ama ya kibiashara au ya kisiasa.
Kilio cha Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma kukosoa bungeni uteketezaji wa zana za uvuvi zinazotajwa na Serikali kuwa haramu kimeitikiwa kwa mijadala na hisia tofauti katika visiwa mbalimbali vya Ziwa Victoria.
Jambo moja liko wazi kwamba katika operesheni za kukamata zana hizo na uteketezaji wake, wanasiasa wa maeneo husika, wakiwamo madiwani na wabunge, wanakwepa kushiriki ili kulinda masilahi yao ama ya kibiashara au ya kisiasa.
Wakati akichangia hoja hiyo bungeni, Musukuma anakosoa operesheni hiyo akieleza kuwa ni mwiba kwa wananchi kwa kuwa imepandisha bei ya debe la dagaa kutoka kati ya Sh25,000 na Sh30,000 hadi 40,000 na 50,000 huku akionyesha hofu ya wabunge wanaotoka Kanda ya Ziwa kutorejea bungeni kutokana na ghadhabu ya wapiga kura.
Hata hivyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina analieleza Bunge kuwa vita ya kupambana na uvuvi haramu haitasimama licha ya kwamba inawagusa baadhi ya wabunge na wenyeviti wa halmashauri.
Mpina anasema operesheni sangara 2018 aliyoiunda ina wataalamu wa uvuvi, wavuvi, Baraza la taifa la usimamizi wa Maizngira (Nemc) na polisi, hafanyi uamuzi mtu mmoja.
Anasema katika viwanda vyote walivyovikagua hawajakuta kiwanda kinachochakata samaki wanaoruhusiwa na kuna magari ya wabunge na wenyeviti wa halmashauri yalikamatwa na samaki wasioruhusiwa na watendaji wa Serikali wamesimamishwa.
Akibanwa na wabunge ili awataje wabunge Waziri anasema taarifa ya operesheni hiyo iko mbioni kukamilika na atakabidhi nakala yake na kamati ya bunge, ikieleza wote waliohusika na uvuvi huo haramu.
Akiwa Kagera hivi karibuni kushiriki operesheni ya kuteketeza zana haramu, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega alisema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri) unaonyesha kuwa Ziwa Victoria linaelekea kupoteza samaki wengi kutokana na uvuvi haramu na kuwa asilimia nne tu ya samaki wazazi ndio wamebakia.
INAENDELEA UK 24
INATOKA UK 23
Alisema asilimia 94 ni samaki wachanga ambao kwa kiwango kikubwa wanavuliwa kwa njia haramu, kati yake idadi kubwa wakiwa ni sangara.
Matokeo ya uvuvi haramu yameathiri hata uzalishaji kwenye viwanda vya samaki hasa mikoa ya Kanda ya Ziwa na baadhi vinakosa minofu ya kuchakata, jambo linalogusa uchumi wa wananchi na taifa.
Hivi karibuni Serikali imetaifisha zaidi ya tani mia moja za samaki aina ya sangara na kuzipiga mnada katika wilaya za Bukoba na Muleba na zaidi ya Sh200 milioni zilipatikana katika minada ya hadhara iliyofanyika. Matukio ya uvuvi haramu yameliathiri ziwa zima la Victoria hadi katika maeneo ya visiwani.
Safari ya Kerebe
Unahitaji muda wa zaidi ya saa mbili kukifikia kisiwa cha Kerebe kilichopo wilayani Muleba ndani ya Ziwa Victoria kwa usafiri wa boti yenye ‘mwendo wa harusi’ kutokana na uzito wa mawimbi.
Safari inaanzia katika bandari ya Bukoba kwa boti ndogo ya abiria ambayo hufanya safari zake mara tatu kwa wiki. Ukimya unatawala muda wote ndani ya boti ikiwa ni dalili ya hofu waliyonayo abiria.
Kisiwa cha Kerebe kilipoanza kuonekana kwa mbali mazungumzo yanaanza kurejea. Wapo wanaosema kuwa siku hiyo ziwa limechafuka sana, na wengine wakionekana kujutia uamuzi wao wa kusafiri siku hiyo.
Kerebe ni miongoni mwa visiwa zaidi ya 35 vilivyopo Wilaya ya Muleba ambavyo kwa ujumla wake vinachangia asilimia 70 ya makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo kupitia shughuli mazao ya samaki.
Wenyeji wa kisiwa hiki wamefichwa kwenye mchanganyiko wa makabila takribani yote kutoka mikoa inayozunguka ziwa hilo ya Kagera, Geita, Mara na Mwanza.
Uvuvi katika visiwa hivi hufanyika kwa kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine na kufanya kisiwa hiki kutokuwa na wakazi wengi wa kudumu. Kisiwa kina nyumba za kudumu kwa ajili ya kuwapangisha wavuvi.
Wakati wa mavuno mazuri ya sangara na dagaa kati ya Septemba na Aprili kila mwaka, idadi ya wakazi huongezeka hadi kufikia 5,000 na msimu unapoisha idadi hiyo hushuka na kufikia wastani wa wakazi 1,000 mpaka msimu unaofuata.
Kuna kambi tofauti za wavuvi wa dagaa na sangara. Baadhi yake kwa sasa zimefungwa kutokana na ukali wa operesheni ya kupambana na uvuvi haramu katika ziwa hilo inayokwenda sambamba na uteketezaji wa nyavu zisizoruhusiwa kisheria, yaani zenye matundu madogo yanayonasa samaki wachanga.
Katika kijiji cha Makibwa, mitumbwi imeegeshwa kando ya ziwa. Mmiliki aliyekuwa anaajiri zaidi ya watu 60 ameondoka kwenda kujipanga upya jinsi ya kuendesha uvuvi endelevu unaozingatia pia masilahi ya vizazi vijavyo.
Kuanzia hapa unaanza kuona jinsi mfumo wa maisha ya kila siku katika kisiwa cha Kerebe ulivyobadilika katika kipindi hiki cha vita ya kulinda samaki na mazalia yake.
Wengi wakimbia kisiwa
Kisiwa hiki kinaundwa na vijiji viwili vya Kerebe na Makibwa. Ugumu wa maisha uko wazi baada ya shughuli za uvuvi kuathiriwa na operesheni ya Serikali iliyopamba moto na idadi ya wakazi imeshuka kutoka wastani wa 600 hadi watu 400.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Tresphory Kamugisha anasema wakazi wengi wanaaga kuwa wanakwenda kutafuta shughuli mbadala kwa ajili ya kuendesha maisha ikiwa ni pamoja na kujihusisha na kilimo.
Pia, anasema kuwa hata wamiliki wamesimamisha shughuli za uvuvi wakisubiri unafuu utakaoletwa na mabadiliko ya Sheria ya Uvuvi ambayo Serikali imekiri ina upungufu na itapelekwa bungeni mapema mwaka huu kufanyiwa marekebisho.
“Wavuvi wengi waliobaki ni wale wanaotumia kasia na ndoano zinazoruhusiwa kisheria, wengine wameaga wanarudi vijijini kufanya shughuli za kilimo wanasema hakuna tena mzunguko wa fedha kwa kuwa shughuli za uvuvi hazifanyiki kama zamani,” anasema Kamugisha.
Kerebe hapakaliki
Katika Kijiji cha Kerebe kuna kambi tisa za uvuvi wa samaki aina ya sangara na zote zimeyumba kiuchumi baada ya wamiliki kulazimika kusitisha shughuli za uvuvi ili kukidhi matakwa ya kisheria.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Franco Augustine anasema mwitikio wa kufuata sheria ni mkubwa na hiyo ndiyo sababu ya baadhi yao wamelazimika kusitisha shughuli zao na wengine kufuatilia zana halali.
Anabainisha kuwa baadhi ya kambi za uvuvi zimesitisha shughuli na nguvu kubwa imeelekezwa kwenye ukataji wa mitego ili kukidhi matakwa kisheria ya kuwa na nyavu za inchi sita na saba, zinazonasa samaki wakubwa pekee.
Mwenyekiti wa wavuvi katika kijiji cha Kerebe, Mugeta Mauga anasema wanaunga mkono operesheni inayoendelea ingawa ina changamoto kubwa iliyosababisha wavuvi na familia zao kukimbia kisiwa hicho kutokana na ugumu wa maisha.
Anasema hata nyavu zinazotakiwa kisheria hazipatikani kwa urahisi, jambo lililosababisha wamiliki wa kambi za uvuvi kusimamisha shughuli na kulazimika kuondoka.
Anasema kuwa halikuwa jambo la kawaida kitoweo aina ya samaki kukosekana katika kisiwa hicho, lakini sasa jambo hilo linashuhudiwa baada ya makali ya kudhibiti dhana haramu.
Anasema nyavu zinazotakiwa kisheria haziwezi kunasa samaki katika maji ya kina kirefu na kuwa samaki huzalia katika kina kifupi.
Mauga anashauri operesheni hiyo ihusishe pia nchi jirani. Katika kisiwa hicho maarufu kwa uvuvi wa dagaa na sangara zana haramu zenye thamani ya zaidi ya Sh600 milioni zimeteketezwa zikiwamo zilizosalimishwa na wavuvi wenyewe.
Shule hatarini kufungwa
Shule ya Msingi Kerebe ndiyo eneo pekee la kupata elimu kwa wanafunzi wanaozaliwa katika kisiwa hiki. Wanaofaulu huifuata elimu ya sekondari katika kisiwa jirani cha Bumbire.
Wanafunzi wote sita wa darasa la saba waliofanya mtihani wa kuhitimu mwaka 2017 wamechaguliwa kuendelea na masomo Bumbire, wakiwemo wa kike watatu.
Shule ina wanafunzi 106 na walimu watano. Baada ya kuanza kwa operesheni ya kudhibiti uvuvi haramu zaidi ya nusu ya wanafunzi hawaonekani shuleni na wamelazimika kuondoka na wazazi au walezi wao.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Deusdedith Kakiziba anasema wazazi hawawezi kuondoka na kuwaacha watoto nyuma na kuwa utoro huo umekithiri hasa katika kipindi hiki cha kudhibiti uvuvi haramu.
Kati ya walimu watano wa shule hiyo hakuna mwalimu wa kike, jambo linalolazimu uongozi wa shule kuomba msaada kwa baadhi ya wajumbe wanawake katika kamati ya shule ajili kuwasikiliza wanafunzi wa kike kwa baadhi ya mambo.
Mwalimu Kakiziba anasema wamejenga ukaribu na baadhi ya wajumbe wanawake kwenye kamati ya shule ili kuwasikiliza wanafunzi wa kike na kuwapa ushauri kuhusu makuzi na mabadiliko ya miili.
Mahudhurio hafifu pia yanaonekana katika shule ya awali kwenye kijiji cha Makibwa. Ni wanafunzi saba tu wanaofika shuleni kati ya zaidi ya wanafunzi zaidi ya 15.
Mahudhurio hafifu pia yanahusishwa na harakati za wazazi waliokuwa wanafanya shughuli za uvuvi na biashara ya mazao ya samaki kuanza kuhamia maeneo mengine kutafuta shughuli nyingine za kipato.
Mfumo wa maisha katika kisiwa cha Kerebe umebadilika kutokana na wananchi kulazimika kutafuta njia mbadala ya kuingiza kipato.
Wakati hayo yote yakifanyiwa kazi, pia kilio cha wabunge na mahitaji ya Serikali yote yapimwe kwa pamoja na ili kuzingatia hatima ya Ziwa Victoria na ustawi wa vizazi vijavyo.