Maalim Seif anavyoendelea kuishi mioyoni mwa watu

Muktasari:

  • Simulizi, maono na mambo aliyoyaamini Maalim Seif Sharif Hamad bado yanaendelea kuishi, ndivyo unavyoweza kusema. Hii inatokana na wanasiasa na wasomi kuendelea kuzungumzia harakati zake, wakisema alikuwa kiongozi wa mfano

Unguja. Simulizi, maono na mambo aliyoyaamini Maalim Seif Sharif Hamad bado yanaendelea kuishi, ndivyo unavyoweza kusema. Hii inatokana na wanasiasa na wasomi kuendelea kuzungumzia harakati zake, wakisema alikuwa kiongozi wa mfano.

Enzi za uhai wake, Maalim Seif alikuwa kiongozi na mwanasiasa aliyependa haki, usawa, mtu mwenye msimamo anayependa maridhiano, ili kuleta utengamano wa hali ya kisasa Zanzibar. Maono na mambo aliyoyaamini yameendelea kuishi kwa watu kuzungumza na kutoa ushuhuda wao.

Hili lilidhihirika katika mkutano wa pili wa Taasisi ya Maalim Seif (MSF), uliofanyika hivi karibuni mjini hapa. Mkutano huo ni mwendelezo wa kumuenzi Maalim Seif na mwaka huu ulibeba mada ya ‘elimu, ukuzaji, vipaji, ubunifu na uwezeshaji’.

Mkutano huo uliwashirikisha wanasiasa mashuhuri, akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliyesema Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye msimamo, subira na mwanamapinduzi wa kweli.

Kinana anasema enzi za uhai wake, Maalim Seif alikuwa anapenda kuona vijana wanapata elimu bora inayoendana na mahitaji ya wakati yenye kuwajenga kiudadisi.

“Nilipata bahati ya kumfahamu Maalim Seif kwa miaka mingi iliyopita akiwa kiongozi ndani ya CCM, hata alipohama na baadaye kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, hakuyumbishwa na tofauti za kimtazamo za vyama vyetu.

“Maalim Seif aliamini kwa dhati kuwa elimu ndio mkombozi wa kweli wa mwanadamu, ndio maana alijituma katika elimu ya msingi hadi chuo kikuu bila kukata tamaa. Bila shaka viongozi wakati huo waliona na kuthamini kazi ya Maalim Seif ndio maana walimpa jukumu la kuongoza wizara ya elimu,” anasema.

Kinana anasema wakati Maalim Seif akipewa jukumu hilo, fursa za elimu zilikuwa ndogo na hafifu, lakini kwa ujasiri mkubwa kiongozi huyo alichukua hatua madhubuti na kujitwika dhamana ya kufanya kazi kwa ustadi.

Anasema kutokana juhudi zake, vijana wengi wa Zanzibar walipata nafasi za elimu ndani na nje ya nchi. Kinana anasema Maalim Seif aliamini katika elimu kwa sababu ndio mkombozi wa maisha na uhai wa binadamu.

Wakati Kinana akieleza hayo, Balozi Ali Abeid Karume anasema enzi za uhai wake Maalim Seif alikuwa mchapakazi. Anasema wakati akihitaji cheti cha kidato cha sita kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya nchi alipata wakati mgumu wizarani.

“Nilimtuma mtu akachukue, lakini akajibiwa ni kweli cheti cha Ali kipo lakini ni mali ya Serikali, sikufanikiwa, lakini wakati huo Maalim Seif alikuwa waziri, aliposikia aliingia kati na kuamuru nipewe, namkumbuka kwa mambo mengi likiwemo hili,” anasema Balozi Ali.

Kwa upande wake, mfanyabishara maarufum Rostam Aziz anasema ukikaa na Maalim Seif unahisi umekaa na kiongozi, kwani huhitaji kusema chochote bali uwepo wake ulidhihirisha.

“Maalim Seif ni aina ya viongozi ambao ni nadra sana kutokea katika nchi. Huwa ni zawadi kutoka kwa Mungu na huchukua miaka mingi na vizazi kadhaa kabla ya kuja mwingine.

“Kwa nguvu ya kisiasa aliyokuwa nayo angeweza kuamrisha lolote na wafuasi wake wakatekeleza, lakini yeye mara zote alijali maslahi mapana ya nchi yake na watu wake,” anasema Rostam, aliyewahi kuwa mbunge wa Igunga mkoani Tabora.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu anasema Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye misimamo kuhusu Zanzibar, hasa amani, maendeleo ya kiuchumi, elimu, uwekezaji, uhuru na mamlaka kamili ya visiwa hivyo.

“Maalim Seif alikuwa mtu anayemini katika kukaa na kuzungumza, hilo limejidhihirisha wiki mbili zilizopita Zanzibar kulikuwa na mkutano wadau wa siasa kujadili demokrasia ya vyama vingi. Sote kama wanasiasa tumeshiriki kujadili hali hii,” anasema Mwalimu.

Mwalimu anasema MSF bado inaendeleza jitihada za kufanya maono, fikra na ndoto za aliyekuwa kiongozi wao zikiwa zinaendelea kuishi. Anasema namna bora ya kumuenzi Maalim Seif ni kufanya mkutano na kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo viongozi kukumbusha wajibu wao.

Katika mkutano huo wa demokrasia, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema, “maelewano ya kijamii hayawezi kudumu iwapo kila siku mtakuwa mnakumbushana au kutishana kwa mambo yaliyopita, kiini cha maelewano na maridhiano ni ujasiri na kuacha kutonesha vidonda, maana tukifanya hivyo kila mara kamwe haviwezi kupona na maelewano ya kweli huanza na methali inayosema ‘yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.”

Balozi mstaafu wa Norway nchini Tanzania, Jorunn Maehlum anasema Maalim Seif alikuwa anatamani kuona usawa kwa kila mmoja.

Anasema alikuwa na dhamira njema kwa nchi zote mbili; Tanganyika na Zanzibar. Kiongozi aliyeamini suluhu ya mikwamo ya kisiasa ni mazungumzo.

Anasema licha ya changamoto kadhaa alizokutana nazo katika harakati zake za kuleta usawa kwa wote katika maisha yake, hakukata tamaa kusimamia alichokiamini.

“Alipigania haki za wananchi wake muda wote, atakumbukwa kwa hilo na ipo haja ya kuendelea kuenzi maono yake,” anasema.

Profesa Thomas Burgess, mtafiti na mwandishi wa kitabu cha historia ya Maalim Seif, anasema mambo aliyopitia na kuyafanya kiongozi huyo yalikuwa makubwa na yenye historia ya kusisimua, kwani alitaka haki na aliishi katika maisha ya kutojikweza, hakupenda kujilimbikizia mali.

Anabainisha kwamba alikuwa na kanuni zake za kutatua na kushughulikia matatizo. “Kitabu hiki kinaeleza mambo mengi ya Maalim na mwakani kitawekwa katika lugha ya Kiswahili, ili kila mmoja akisome na kumjua Maalim alikuwa mtu wa namna gani.”

Uwezo wa Maalim Seif kuwa na ushawishi kwenye jamii hakuibuka ghafla kwenye siasa, bali alitoka nao wakati wa makuzi yake hata alipokuwa shuleni.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anasema suala la chama kuwa na ofisi mpya kisasa ya makao makuu lilikuwa miongoni mwa mambo aliyoyataka Maalim Seif enzi za uhai, jambo ambalo wamelitekeleza kwa vitendo kwa kuzindua jengo lao wiki iliyopita.