Miaka 15 ya kumbukumbu ya mauaji Zanzibar, wanasiasa wamejifunza nini?

What you need to know:

Mauaji ya Januari 27 yalitokea baada ya polisi kutumia nguvu kubwa wakati wakizima maandamano ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Ni miaka 15 sasa tangu mauaji yalipotokea kisiwani Pemba Januari 27, 2001 kutokana na mgogoro wa kisiasa ambao sasa unaonekana kuwa jambo la kudumu katika visiwa vya Zanzibar.

Mauaji ya Januari 27 yalitokea baada ya polisi kutumia nguvu kubwa wakati wakizima maandamano ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Wafuasi wa CUF walikuwa wakipinga matokeo ambayo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kumtangaza aliyekuwa mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Amani Abeid Karume kuwa Rais wa Zanzibar kwa kumshinda aliyekuwa mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad.

CUF walikuwa wanapinga matokeo hayo wakidai kwamba ‘yamepikwa’ na mgombea wao ndiye aliyekuwa ameshinda katika uchaguzi huo uliokuwa umeshirikisha vyama vingi vya siasa viwasini humo uliofanyika kwa mara ya pili tangu ule wa mwaka 1995.

Katika ghasia hizo za Januari 27, mwaka 2001 watu kadhaa walifariki kwa kupigwa risasi na wengine kujeruhiwa na baada ya tukio hilo mamia ya wananchi walikimbia kutoka Pemba na kwenda Tanzania Bara na wengine Mombasa, Kenya na Somalia.

Hali hiyo ilifanya Tanzania iondoke katika sifa yake ya kupokea wakimbizi nayo kwa mara ya kwanza ikaingia katika kundi la nchi zinazozalisha wakimbizi na kuitia dosari.

Jeraha halijapona

Wakati tarehe hiyo imefika huku Wazanzibar waliowengi wakiwa hawajasahau tukio hilo lilitokea Pemba na lile lililotokea siku moja kabla katika Kisiwa cha Unguja kwa kupoteza ndugu zao inaingia wakati Zanzibar ipo tena katika mgogoro wa kisiasa.

Mgogoro huo wa kisiasa umetumbukizwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha baada ya kufuta matokeo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Octoba 25,2015, siku tatu baada ya uchaguzi kufanyika huku waangalizi wa ndani na wa wakimataifa wakisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Wananchi wa Zanzibar kwa kawaida ni watulivu, wenye subira, hekima na watiifu na hayo yanajengwa zaidi kutokana na imani zao za dini na ndiyo maana pamoja na tukio hilo wametulia na wanaendelea na shughuli zao licha ya kuwa na hofu kubwa mioyoni mwao.

Subira ina mwisho wake, kwa hiyo wakati umefika kwa baadhi ya watu kuacha tabia za uchokozi ambazo zinaweza kuibua hasira miongoni mwa wananchi na kuvuruga amani iliyopo.

Hoja ya ubaguzi

Baada ya miaka 24 tangu kurudi kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini inashangaza kumsikia mtu akinadi hadharani kuwa watabadili Katiba ambayo itaruhusu mgombea wa CCM kugombea kiti cha urais wa Zanzibar na vyama vingine vigombee nafasi zilizobaki.

Tamko hili kama lingetolewa kwenye masikani yoyote lingepuuzwa kwani athari yake ingekuwa ndogo, lakini walielezwa wasomi wa vyuo vikuu ambao ni wafuasi wa CCM ambao kwa mazingira ya Zanzibar ndiyo wenye nafasi kubwa za kuchukua madaraka serikalini kwa hiyo kuwajenga kwenye misingi ya ubaguzi ni jambo la hatari.

Kabla hilo halijatua likazuka jipya kwa wana CCM kuwa na bango lenye ujumbe wa kibaguzi kwa siku mbili kwenye maandamano ya Umoja wa Vijana wa chama hicho na kwenye Sherehe za Mapinduzi.

Ujumbe huu wa kibaguzi ulikuwa una waambia machotara kwa maana ya watu wenye asili ya zaidi ya Kiafrika kama vile Kiarabu na Kiasia kuwa Zanzibar siyo ya, bali ni ya Waafrika.

Watu hawa walisahau kuwa katika CCM kuna machotara wengi kutokana na historia ya chama hicho ambacho kilizaliwa kwa muungano wa Tanu ya Tanzania Bara na Afro Shirazi (ASP) ya Zanzibar.

Hali halisi inaonyesha kuwa Baraza la Mapinduzi Zanzibar (BMZ) la kwanza baada ya mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964 ni wajumbe wawili ambao hawakuoa wake wenye asili ya Kiarabu au Kiasia na kwa hiyo kufanya kizazi chao chote kiwe cha machotara ambao sasa wengi wao wako madarakani.

Kwa Zanzibar ni jambo la kawaida kiongozi wa siasa au Serikali kuwa chotara kwa vile asili ya visiwa hasa vilivyozungukwa na Bahari ya Hindi ni vya watu mchanganyiko na ni jambo ambalo haliwezi kuepukika. Inasemekana Zanzibar hakuna ukoo usio na chotara.

Sasa kuleta ubaguzi wa aina hiyo katika kipindi kama hiki ni jambo la kusikitisha na lenye nia ya kutaka kutibua nyongo za Wazanzibari ambao waliamua kufunika ‘kombe mwana haramu apite’.

Ubaguzi wa aina hii hausaidii kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wala hauwasaidii katika kujitafutia maendeleo na riziki zao za kila siku, bali unazidi kujenga chuki na uhasama miongoni mwao.

Mchango wa Rais Karume

Jambo jingine ambalo linachefua ni kwa wana CCM kuzoea tabia ya kumzomea aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa Serikali iliyopita, Dk Amani Abeid Karume jambo ambalo halileti sifa na wala si jema kufanyika kwenye hadhara na kwenye wageni.

Jumanne ya Januari 12, mwaka huu, wafuasi wa CCM walimzomea Dk Karume wakati alipoingia na kutambulishwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein wakati wa Sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan.

Kumzomea Dk Karume ambaye ni shujaa aliyeiletea utulivu na amani Zanzibar baada ya uhasama wa miaka mingi kwa kuleta mwafaka kati ya CCM na CUF, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif ni jambo la huzuni na la kusikitisha.

Dk Karume anapaswa kuheshimiwa na kuenziwa na kama Zanzibar ingekuwa na tuzo yoyote anastahili kutunukiwa. Kwa kushirikiana na Maalim Seif waliitoa Zanzibar katika dimbwi la uhasama na mtafaruku mkubwa miongoni mwa wananchi.

Mashujaa hao wanapaswa kuheshimiwa na kila Mtanzania na kila mpenda maendeleo, kwani hali ya kisiasa Zanzibar ilikuwa imechafuka na ilikuwa haitoi fursa ya kutosha kwa maendeleo.

Inawezekana matukio haya yanajengwa kutokana na kiwewe na jinamizi lililowakumba wafuasi wa CCM kwa upinzani mkali walioupata kwenye Uchaguzi Mkuu wa urais uliofanyika Oktoba 25 mwaka 2015. Siku zote ukikubali kuwa katika vyama vya siasa uelewe kwamba kuna kushinda na kushindwa.

Uzalendo kwanza

Wazanzibari sasa watafakari upya kuijenga demokrasia ya kweli na kuacha fikra za kuwa chama ni kitu cha msingi kwa kuwa kinaweza kufa, lakini Taifa linaendelea kudumu. Leo viko wapi vyama vya Tanu, ASP, ZNP, ZPPP, Umma na vyama vingine ambavyo vilikuwa ndani ya mioyo ya wananchi.

Wazanzibari sasa tuwe na busara, tujenge umoja kwa lengo la kuijenga Zanzibar ili iweze kupata maendeleo kwa manufaa ya wananchi na amani idumishwe ili yale ya Januari 27, mwaka 2001 yasije kujirudia tena.

maoni@tz.nationmedia.com     

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.