Namna ya kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya uchaguzi
Muktasari:
- Moja kati ya vyama hivyo kilifikia hatua ya kususia uchaguzi mdogo uliofuata kwa madai kuwa malalamiko yao juu ya mambo yaliyojitokeza katika uchaguzi mdogo uliopita, yalishindwa kushughulikiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Katika chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni, kuliibuka baadhi ya malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa na wagombea juu ya baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika chaguzi hizo.
Moja kati ya vyama hivyo kilifikia hatua ya kususia uchaguzi mdogo uliofuata kwa madai kuwa malalamiko yao juu ya mambo yaliyojitokeza katika uchaguzi mdogo uliopita, yalishindwa kushughulikiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Kwa kutambua matakwa ya kisheria yanayoongoza chaguzi, Tume ilivikumbusha vyama vya siasa na wagombea kufuata Sheria za Uchaguzi katika kushughulikia malalamiko yanayojitokeza kwa kuwa hakuna ombwe la kisheria kuhusiana na jinsi ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko hayo.
Leo tunapambanua namna mgombea yeyote, Tume, Serikali au chama cha siasa kilichosaini Maadili ya Uchaguzi na kuweka mgombea katika uchaguzi, kinavyotakiwa kushughulikia malalamiko ya uchaguzi pale kinapoamini kuwa maadili ya uchaguzi yamekiukwa.
Chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi, mgombea, Tume na Serikali wana haki ya kuwasilisha malalamiko yanahusu ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi, kwa kufuata taratibu na ngazi husika kama ilivyoelekezwa katika maadili na si vinginevyo.
Malalamiko yoyote yanayojitokeza, yanatakiwa kuwasilishwa kwa maandishi kwa mwenyekiti wa kamati ya maadili katika ngazi husika, ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili katika ngazi husika anatakiwa kuitisha kikao cha wajumbe wa kamati hiyo ndani ya saa 48 baada ya kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, kamati itamtaka aliyelalamikiwa kuwasilisha utetezi wake kwa maandishi ndani ya saa 48 tangu kupokea malalamiko anayolalamikiwa.
Malalamiko yote yatajadiliwa na kuamuliwa katika kikao cha kamati ya Maadili ya Uchaguzi kwenye ngazi husika na kamati itayashughulikia na kutoa uamuzi wake mapema iwezekanavyo.
Katika kushughulikia malalamiko hayo, kamati inaweza kumuita mtu yoyote kutoa maelezo ili kusaidia kamati kufikia maamuzi yake kwa haki.
Akidi ya wajumbe wa kikao cha kamati ya Maadili ya Uchaguzi inatakiwa kuwa zaidi ya nusu ya wajumbe wote wa kamati hiyo kama tulivyowataja katika makala zilizopita.
Kamati ya Maadili ya Uchaguzi inatakiwa kuamua malalamiko yote ndani ya muda wa saa 48 baada ya kusikiliza au kupata maelezo ya utetezi kutoka kwa pande zote mbili ambazo ni mlalamikaji na mlalamikiwa.
Maamuzi yatakayofikiwa na Kamati ya Maadili ya Uchaguzi yatatekelezwa na pande zinazohusika na maamuzi hayo.
Ikitokea kuna umuhimu wa kufanya maamuzi kwa kupiga kura, wawakilishi wa mlalamikaji na mlalamikiwa hawataruhusiwa kupiga kura ya maamuzi hayo.
Malalamiko yatakayoshughulikiwa na Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ni yale ya kipindi cha kampeni za uchaguzi tu na si vinginevyo.
Malalamiko yatakayotokea siku ya upigaji kura, yatashughulikiwa na Msimamizi wa Kituo cha Kupigia Kura, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Msimamizi wa Uchaguzi au Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi.
Kamati ya Maadili ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuchunguza malalamiko yote yatakayowasilishwa kabla ya kufanya uamuzi wa malalamiko hayo.
Kamati inaweza kuelekeza malalamiko mengine kwenye mamlaka zinazohusika kama itakavyoona inafaa kwa hatua zinazostahili.
Iwapo itatokea upande mmoja haukuridhika na uamuzi wa kamati ya maadili kuhusu malalamiko yaliwasilishwa, upande huo una haki ya kukata rufaa ya kupinga uamuzi uliotolewa kwa kufuata utaratibu ufuatao.
Kama ni malalamiko yaliyoshughulikiwa katika ngazi ya kata, mlalamikaji atakaa rufaa ndani ya saa 24 tangu uamuzi husika ulipotolewa kwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo.
Uamuzi utakaotolewa na Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo utakuwa ni wa mwisho kwa malalamiko yote yaliyoanzia ngazi ya Kata.
Kama ni malalamiko yaliyoshughulikiwa katika ngazi ya Jimbo, mlalamikaji atakata rufaa ndani ya saa 48 tangu uamuzi husika ulipotolewa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa.
Upande ambao hautaridhika na uamuzi wa Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa, utakata rufaa ndani ya saa 48 baada ya uamuzi wa Kamati ya Kitaifa kutolewa, kwa Kamati ya Maadili ya Rufaa.
Uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Rufaa utakuwa ni wa mwisho kwa malalamiko yote yaliyoanzia Kamati ya Rufaa ngazi ya Jimbo.
Ikitokea kuna umuhimu wa kufanya uamuzi wa Kupiga kura, wawakilishi wa mlalamikaji na mlalamikiwa hawataruhusiwa kupiga kura ya uamuzi.
Upande usioridhika na uamuzi unaweza kufungua malalamiko ya Uchaguzi mahakamani baada ya Uchaguzi kumalizika kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 au Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa, Sura ya 292.
Mwandishi ni Afisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.Kwa maswali na maoni tuma kwenda [email protected] au sms 0767598602.