Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni wajibu kujenga Tanzania yenye utu na ubinadamu

Muktasari:

  • Kennedy aliongeza: “Raia wenzangu wa ulimwengu: msiulize nini Marekani itawafanyia, isipokuwa mjiulize kile tunachoweza kufanya kwa pamoja kwa ajili ya uhuru wa binadamu.”

Januari 20, 1961, Rais John Kennedy, katika maneno ya mwisho-mwisho, kwenye hotuba yake baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Marekani, alisema: “Na hivyo, Wamarekani wenzangu: msiulize nchi yenu itawafanyia nini, jiulizeni nini mtaifanyia nchi yenu.”

Kennedy aliongeza: “Raia wenzangu wa ulimwengu: msiulize nini Marekani itawafanyia, isipokuwa mjiulize kile tunachoweza kufanya kwa pamoja kwa ajili ya uhuru wa binadamu.”

Inampasa kila Mtanzania kujiuliza ni nini anaweza kuifanyia nchi yake ili kujenga Taifa bora ambalo mtoto na mjukuu wake wataishi. Yale ambayo anayaona hayafai, basi angalau afanye kitu yasije kuendelea yakawaumiza mwanaye na mjukuu.

Yenye kutokea sasa, kama tukio la hivi karibuni la Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Kata ya Kisutu, Dar es Salaam, Elizabeth Mambosho, kukamatwa na kuwekwa mahabusu pamoja na mtoto wake mchanga mwenye matatizo ya kiafya, ni masuala ya kuchora mstari wa masahihisho.

Imeelezwa kuwa Elizabeth alikamatwa hospitali, Morocco, Dar es Salaam, Aprili 25, mwaka huu, alipompeleka mwanaye kwa daktari bingwa wa watoto kwa sababu mtoto wake tangu alipozaliwa amekuwa na matatizo ya kiafya.

Ni wiki tatu tu tangu Elizabeth alipojifungua ndipo alipokamatwa na mtoto wake. Ilielezwa kwamba Elizabeth alijifungua kwa upasuaji, hivyo kipindi anakamatwa alikuwa anauguza kidonda. Elizabeth na mwanaye mgonjwa wakalazwa mahabusu, Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Zingatia kuwa walikamatiwa hospitali. Yapo maelezo kuwa daktari wa watoto aliomba mtoto abaki hospitali anatibiwa lakini hakusikilizwa. Usiku wakiwa mahabusu mtoto alizidiwa lakini hakuna msaada wowote ulitolewa zaidi ya mabishano, mpaka asubuhi alipoachiwa kwa dhamana.

Vaa nafsi ya familia ya Elizabeth; kama ndiye mkeo aliyejifungua kwa upasuaji na mwanao mgonjwa wamelala mahabusu. Ikiwa ni dada yako na mpwa wako. Labda ni mwanao na mjukuu wako.

Ukitafakari vizuri zipo hisia utazipata. Hizo ambazo umezipata hazifikii machungu ya wana familia ya Elizabeth.

Hiyo ndiyo Tanzania?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aya ya kwanza kabisa katika utangulizi, inasomeka: “Kwa kuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.”

Chukua maneno uhuru, haki, udugu na amani. Utaona kwamba hekima iliyolileta Taifa la Tanzania pamoja, ilibeba makusudio ya kuwafanya Watanzania waishi kama ndugu.

Kila Mtanzania ni ndugu wa Mtanzania. Sasa inakuwaje mtu anakubali ndugu yake mgonjwa na mtoto anayeumwa walale mahabusu bila kupata matibabu?

Katika kuulinda undugu wa Mtanzania, vimewekwa vyombo mahsusi vya kusimamia utekelezaji pale ambapo Mtanzania anapofanya makosa.

Jeshi la Polisi lipewe mamlaka ya kupokea na kusikiliza malalamiko kabla ya kuyaweka kuwa tuhuma, kisha kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.

Mahakama ndiyo chombo cha kutafsiri sheria na kutoa haki. Sasa basi mtu kukutwa na hatia au kuondolewa hatiani ni uamuzi ambao hutolewa na mahakama. Kwa mantiki hiyo, Elizabeth hana hatia kwa makosa yoyote, isipokuwa hoja za polisi hubaki kuwa tuhuma. Sasa unamzuia mtoto kupata matibabu kisa mama yake anatuhumiwa?

Katiba ya Tanzania, ibara ya 13, ibara ndogo ya 6 (b), inatamka: “Ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.”

Soma tafsiri hapo, kisha fikiri mantiki ya kumkamata mtu hospitali alikompeleka mwanaye mgonjwa. Mtoto mchanga wa wiki tatu.

Ni dhahiri ipo misingi ya utu ambayo inakiukwa. Katiba na sheria za nchi, zinatoa haki kwa watuhumiwa. Kwamba hata mtuhumiwa ana haki za msingi. Haikushindikana polisi kusubiri Elizabeth amalize taratibu za kumpatia matibabu mwanaye. Kulikuwa na namna ya kufanya.

Mfano wa tukio la Elizabeth ujenge wajibu wa kufanya, kwamba kila Mtanzania anatakiwa kuhakikisha mwanaye au mke wa mtoto wake, siku zijazo hatendewi kama Elizabeth. Afikirie kuwa mjukuu wake mchanga wa wiki tatu na aliye mgonjwa, hatalala mahabusu bila matibabu.

Wajibu huo unatakiwa ujengwe kwenye nguvu ya mihimili. Nchi iwe na wabunge wenye kutambua wajibu wa kumtetea mpigakura. Wabunge wenye kuzingatia dhima ambayo mhimili wao umeubeba kikatiba mbele ya wananchi. Wajibu huo uifanye Serikali kuliheshimu Bunge.

Lazima Bunge lijipambanue kwamba kweli lenyewe ni chombo cha uwakilishi na lipo kuisimamia Serikali.

Wabunge nao wawe na utambuzi pasipo kuyumba kwamba uimara wao ndiyo nchi itakuwa imara. Nidhamu kwa Katiba na sheria za nchi, kwa kiasi kikubwa hutegemea nguvu ya Bunge. Kama Bunge si imara, vyombo vya dola vitawaumiza wananchi.

Upo wajibu wa kuijenga Tanzania bora yenye kuheshimu utu wa kila mtu. Mahakama ambacho ni chombo cha kutoa haki, kisiwe eneo lenye kulalamikiwa kwa kupindisha haki. Upo wajibu mkubwa wa kuhakikisha mtoto na mjukuu wako watatendewa haki mahakamani bila ushawishi wa rushwa na nguvu ya mamlaka.

Ni wajibu wa rohoni

Malalamiko si ujenzi. Wananchi wanatakiwa waanze kuwafanya wabunge wao waone wajibu wa kujieleza. Wawe wanatoa ripoti ya utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge na yale ambayo wanakusudia kufanya. Wabunge wawe wanajipambanua na wananchi waridhie kuhusu uhusika wao bungeni.

Ikiwa mbunge anakwenda kuzungumza mipasho na vijembe bungeni, iwe hivyo kama wapigakura wake wameridhia. Haifai katika nchi kuwe na masuala yenye kuhitaji nguvu ya Bunge ili yanyooshwe, lakini kunakuwa na kusuasua kwa wabunge kuchukua hatua.

Masuala ya kupotea kwa kijana wa Kitanzania, Ben Saanane, umepita mwaka mmoja na miezi sita sasa. Mwandishi wa habari wa kujitegemea aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, inaelekea miezi sita sasa tangu alipotoweka. Mwanamuziki wa Hip Hop, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’, alitekwa na wenzake watatu mwaka jana na kuachiwa baada ya siku tatu.

Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, alipigwa risasi na kufariki dunia, Februari 16, mwaka huu. Akwilina alikuwa kwenye daladala na alipigwa risasi wakati polisi walipokuwa wakidhibiti maandamano ya viongozi na wafuasi wa Chadema.

Hakuna ambacho kimepata kuelezwa na kikatoa matumaini kuhusiana na Saanane, Akwilina na Azory.

Hata Roma na wenzake ambao walionekana, nchi haijaelezwa nini kiligundulika kuhusu kupotea kwao na kujikuta wapo ufukwe wa Bahari ya Hindi, Ununio, Dar es Salaam.

Mbunge wa Singida Kaskazini (Chadema), Tundu Lissu alipigwa idadi kubwa ya risasi Septemba 7, mwaka jana na mpaka leo hakuna mtu aliyewahi kukamatwa ili ahusishwe na tukio hilo. Ongeza idadi kubwa ya watu waliokutwa wamekufa kando ya Bahari ya Hindi, nao majibu hayajapatikana.

Inatakiwa kila mmoja afikiri nini ataifanyia Tanzania ili kujenga Taifa ambalo watu wakipotea basi majibu yanatafutwa mpaka yapatikane. Hata yakikosekana, basi ionekane dhamira na juhudi za kuyatafuta. Mtu akishambuliwa kwa risasi, juhudi kubwa ziwepo kuwatafuta wahalifu.

Bunge kama chombo chenye kuisimamia Serikali, lina wajibu wa kuingilia kati na kufanya uchunguzi wa kibunge pale ambapo vyombo vya utawala vinapokosa majibu ya kuridhisha kuhusu masuala yenye kuisumbua nchi. Mfano hivi karibuni Mkurugenzi wa Mashtaka alitangaza kufunga jalada la Akwilina.

Taarifa iliyotolewa ni kuwa Akwilina alipigwa risasi kwenye mazingira ya hekaheka za watu wengi, kwa hiyo imekuwa vigumu kutambua risasi iliyompiga ilitoka kwenye bunduki gani. Zaidi, ilielezwa kwamba mwili wa Akwilina haukukutwa na risasi.

Majibu kama hayo yanapotoka kwenye vyombo vya Serikali, ndipo Bunge huona wajibu wa kuingia kati na kufanya uchunguzi ili kujiridhisha kama kweli imeshindikana kumpata aliyempiga risasi Akwilina?

Serikali imepewa mamlaka makubwa mno. Hata hivyo, Bunge limepewa nguvu kubwa kabisa ya kuweza kuidhibiti.

Nguvu hizo ambazo Bunge linazo ili zitumike sawasawa, inahitaji wabunge wakali na wenye misimamo inayolalia masilahi ya wananchi kwa kizazi cha sasa na kinachokuja.

Bila Bunge kuonyesha makucha yake, Serikali haitaliogopa, itaendelea kutenda kwa mazowea.

Ikiwa wananchi hawataona umuhimu wa kuwakabili wabunge na kuwahoji kuhusu namna wanavyotimiza wajibu wao wa kuisimamia Serikali, mambo yatabaki kama yalivyo sasa. Ndiyo sababu kila mmoja anahitajika kufanikisha ujenzi wa nchi yenye kesho iliyo bora.

Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Simu: +255 713 355 717