Rais Uhuru na kibarua cha kuunda Baraza la Mawaziri

Muktasari:

  • Si rahisi kwa Rais Uhuru kufanya hivi kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni watu wengi wanaotarajia kuteuliwa kuwa mawaziri.

Baada ya kuapishwa wiki jana kwa muhula wake wa pili na mwisho, Rais Uhuru Kenyatta sasa anajipanga kuteua Baraza jipya la mawaziri.

Si rahisi kwa Rais Uhuru kufanya hivi kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni watu wengi wanaotarajia kuteuliwa kuwa mawaziri.

Kwa sababu ya kivumbi cha uchaguzi wa Agosti 8 na ule wa marudio wa Oktoba 26, chama cha Jubilee kilitafuta uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa waliokuwa wa upinzani na kuwashawishi wasimame nacho ili kikishinda uchaguzi, watapewa nyadhifa gani serikalini.

Isitoshe, kuna wanasiasa waliochangia kwenye mfuko wa kampeni wa Jubilee nao pia hawawezi kukubali kubaki nje huku wengine wakila minofu.

Vilevile, kuna shinikizo kutoka kwa Wakenya wa matabaka mbalimbali wakiwamo wapiganiaji wa haki za kibinadamu, wakuu wa taasisi za dini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambao wanamtaka kiongozi huyo afungue macho yake zaidi wakati huu na kuwateua mawaziri kutoka kabila nyingine.

Tangu 2013, Baraza la Mawaziri la Rais Uhuru lina asilimia 80 ya watu kutoka makabila mawili: Kikuyu na Wakalenjin ilhali Kenya inajivunia makabila 42. Wakalenjin na Wakikuyu pia ndio wengi zaidi katika nyadhifa nyingine nje ya jukwaa la siasa. Kampuni takriban zote za Serikali na hata benki zinaongozwa na watu kutoka makabila hayo.

Hali hii si nzuri kwa sababu haionyeshi sura nzuri ya Kenya.

Kwa kuwa Katiba inakubali mawaziri 22, Rais atakuwa na kibarua kigumu cha kufurahisha kila mtu. Itabidi awaudhi wengine na kuwafurahisha wengine.

Baraza la Mawaziri la sasa lina watu 18. Kutokana na msukumo kutoka kila kona, Jubilee inaweza kuongeza idadi hiyo ifike 22 ambayo inakubalika kisheria. Hii itahakikisha wanasiasa kama vile aliyekuwa mbunge wa Budalang’I, Ababu Namwamba ambaye alihamia Jubilee kutoka kwa chama cha ODM cha Raila Odinga. Kwa vile alishindwa kwenye uchaguzi mkuu wa hivi majuzi na mpinzani wake mkuu Raphael Wanjala, Namwamba anatumai kuwa atapewa wadhifa wa uwaziri. Kuna fununu kuwa tayari mwanasiasa huyo amewekwa kwenye orodha ya mawaziri wapya.

Pia, aliyekuwa seneta wa Mombasa, Hassan Sarai alihama muungano wa Nasa baada ya kushindwa na Gavana Ali Hassan Joho. Sarai alikuwa amewania ugavana baada ya kupuuza ushauri wa wataalamu wa kisiasa. Japo alijua kuwa hawezi kushinda vita na Joho, mwanasiasa huyo alijitosa uwanjani na hatimaye, alichunwa ngozi na kuachwa na majeraha ya mechi.

Sarai alipoona dunia ni duara, akaamua kuhamia Jubilee baada ya uchaguzi wa Agosti 8 na tangu wakati huo, amekuwa akiomba Mola amwangazie ili ateuliwe kuwa waziri. Mwanasiasa Gideon Munga’ro ambaye pia ni mtu wa pwani kama Sarai, pia anapania kuteuliwa waziri. Kinyume na Sarai, Mung’aro ameifanyia mengi Jubilee kwa sababu aliondoka upinzani miaka mitatu iliyopita na kujiunga na Jubilee. Kati ya wanasiasa hao wawili wa Pwani, Mung’aro ana nafasi kubwa ya kuingia kwenye Baraza la Mawaziri.

Mbali na hao, kuna wanasiasa chungu nzima kutoka Pwani waliohama Nasa na kuingia Jubilee lakini hawakufua dafu katika uchaguzi. Bila shaka, huku wakitetemeka kwa sababu ya baridi ya kutokuwa bungeni, tumaini lao kuu ni kuteuliwa kuwa mawaziri au wakurugenzi watendaji katika kampuni za Serikali. Hata paka mzee hunywa maziwa. Wakikosa hayo, wataomba wateuliwe kama mabalozi na kadhalika.

Ahadi ni deni. Ili aweze kulipa deni, Uhuru hana budi kutumia umakini, ushauri na mtazamo wa kizalendo ili asije akawafungia wengine nje.

Ni desturi ya siasa kuwa mawaziri wengine hawana budi kutimuliwa kutoka katika baraza ili kutoa nafasi kwa mawaziri wapya. Baraza la sasa, lina mawaziri goigoi, wasioaminika na wanaoshukiwa kusifu Jubilee kwa vinywa vyao lakini nyoyo zao ziko mbali na chama hicho. Hao ndio chuma chao kiko motoni na wakati ukiwadia, wataonyeshwa mlango wazi na kuamuriwa wapotelee mbali. Waziri wa Leba na mashauri ya Afrika Mashariki Phylis Kandie ni mmoja wao. Wengine wanajijua na fimbo itawafikia wakati ufaao.

Vilevile, kuna baadhi ya mawaziri waliofanya vyema kwa kazi zao na kuwafurahisha mabosi wao. Waziri wa Masuala ya Nje, Amina Mohamed ni mmoja wao. Waziri huyu amemsaidia Rais Uhuru kwa moyo wake wote na alijitolea kutembea ulimwengu mzima akifanya kampeni za kuwaokoa Rais Uhuru na Naibu wake William Ruto kutoka katika hatari ya kufungwa Uholanzi kufuatia kesi za mauaji na uvunjaji wa haki za kibinadamu zilizokuwa zinawakabili.

Je, Uhuru atamteua waziri mwingine kutoka kwa kabila la Waluo au atamwacha Waziri wa Ulinzi, Rachel Omamo kuendelea kuchapa kazi? Habari zisizothibitishwa zinasema kwamba Omamo huenda akaondolewa kutoka kwa wizara hiyo na kuhamishwa kwa wizara nyingine.

Waziri wa kipekee Mmasai Joesph Nkaiserry alifariki dunia katikati ya mwaka huu katika kisa cha kutatanisha. Waziri wa Elimu, Fred Matiang’I ndiye anahudumu kama waziri katika wizara hiyo. Je, Uhuru atamteua Mmasai mwingine kusimamia wizara hii. Kwa muda mrefu wizara hii imekuwa na mawaziri Wamasai. Tutangoja kuona kama historia itajirudia.

Matiang’I amefanya vizuri mno katika wizara ya Elimu. Kwa hivyo, itakuwa vigumu kwa Uhuru kumuondoa. Waziri huo asiye na mzaha wakati wa kazi, amemaliza udanganyifu katika mitihani ya kitaifa na kuleta mabadiliko mazuri katika sekta ya elimu.

Kwa sababu hii, Matiang’I anafaa kuendelea kuhudumia umma kama waziri wa Elimu ili aendeleze kampeni zake za kuinyoosha sekta hii iliyokuwa imeanza kuoza.

Rais anatarajiwa kufikisha bungeni Jumatano au Alhamisi majina ya walioteuliwa kujaza nafasi za uwaziri. Zoezi hili limechelewa kwa sababu ya mizozo bungeni kutokana na wabunge wa Nasa kuapa kwamba hawawezi kuketi bungeni kuwahoji walioteuliwa.

Wanasema kwamba wakifanya hivyo, watakuwa wanaunga mkono ushindi wa Rais Uhuru wa Oktoba 26. Kwa hivyo, watasusia wajibu huo. Wanasiasa hao wamekataa kuhusishwa na kamati mbalimbali za Bunge ijapokuwa Nasa imewateua viongozi wa walio wachache bungeni na seneti.

Mbali na hayo, Nasa inajitayarisha kumwapisha Raila Odinga mnamo Desemba 12 kama Rais. Hata hivyo, juhudi zao zimeanza kufuatiliwa na Serikali. Mshauri wa uchumi wa Nasa ambaye anategemewa mno katika kuhakikisha kwamba sherehe hiyo inaendelea bila bughudha, Dk David Ndii alinaswa na maofisa wa ujasusi alipokuwa likizoni Pwani mnamo Desemba 3 na kuzuiliwa rumande na kuachiliwa baadaye.

Kuna hofu wanasiasa na wakereketwa wa Nasa zaidi wanacheza mchezo wa paka na panya na maofisa hao wasije wakatiwe mbaroni.

Katika mitandao ya kijamii, wafuasi wa Nasa wanasema wako tayari kujihusisha na juhudi zozote zinazoweza kuleta ukombozi wa tatu nchini.

Matukio hayo yataendelea kuzidisha kidonda cha siasa kati ya Jubilee na Nasa na kufanya shughuli za Bunge kukwama na kuathirika.

Ningekuwa Rais Uhuru, ningewaita viongozi wa upinzani na kujadiliana nao kuhusu jinsi ya kuleta Wakenya wote pamoja ili kuepukana na mizozo inayoweza kupasua nchi.

Kumbuka kwamba, Wakenya zaidi ya milioni sita ambao ni wafuasi wa Raila Odinga hawawezi kutosha kwenye magereza ya Kenya hata kama jela zaidi zitajengwa.

Ni wakati wa Kenya kuwa na mwamko mpya kwa minajili ya vizazi vijavyo.