Dk Mwakyembe: Tutawapa mapokezi makubwa

Muktasari:

  • Infantino atakayeongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Ahmad Ahmad, Dk Mwakyembe alisema Serikali imeona ugeni huo ni mzito na haiwezi kuliachia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) peke yake kuratibu ziara hiyo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali imejipanga kuupa mapokezi mazuri msafara wa watu zaidi ya 64 wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, Gianni Infantino na kusema pia kuwa hiyo ni fursa ya Tanzania kujitangaza.

Infantino atakayeongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Ahmad Ahmad, Dk Mwakyembe alisema Serikali imeona ugeni huo ni mzito na haiwezi kuliachia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) peke yake kuratibu ziara hiyo.

“Kwa sababu hiyo tumeona tufanye kazi bega kwa bega na TFF ili kuhakikisha Infantino na msafara wake wanafurahi ziara hiyo.

“Tunataka kuionyesha Fifa kuwa Watanzania ni watu wa mpira, Watanzania wanapenda soka na ndiyo maana tunataka kuwapa heshima hata wakiondoka wakumbuke Tanzania,” alisema.

Waziri Mwakyembe alisema kama Serikali, watahakikisha msafara huo utakapokuwa nchini pamoja na ratiba zake, unapata fursa ya kukutana na Waandishi wa Habari.

Kuhusu kukutana na Rais John Magufuli, Dk Mwakyembe anasema Rais Magufuli ni mpenda michezo hivyo atafanya jitihada zake zote kuhakikisha anakutana na Rais Infantino atakapokuwa nchini.

‘’Kwakuwa Rais Magufuli ni mpenda michezo, lazima atapenda kuonana na Rais wa Fifa, Gianni Infantino, na mimi kama waziri mwenye dhamana ya michezo nitahakikisha hilo linawezekana,” anasema.