Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mayweather,Pacquiqao waigawa Dar es Salaam

Muktasari:

Pambano la Mayweather na Pacquiao limekuwa likipigwa danadana, ila tayari promota Bob Arum amewasainisha mkataba mabondia hao ambao wapo tayari kuzichapa katika pambano ambalo limevunja rekodi kwani mabondia watachukua dola 250 milioni, huku Mayweather akilipwa asilimia 60 na Pacquiao, asilimia 40 ya fedha hizo.

Je, Amerika itakubali fedheha mbele ya Mfilipino? hili ni swali ambalo dunia inasubiri lijibiwe Mei 2 mwaka huu wakati miamba ya ndondi, Floyd Mayweather Junior wa Marekani na Manny Pacquiao wa Ufilipino watakapopanda ulingoni kwenye ukumbi wa MGM Grand mjini Las Vegas, Marekani kutafuta mbabe wa dunia wa uzani wa welter, kilo 69. Pambano la Mayweather na Pacquiao limekuwa likipigwa danadana, ila tayari promota Bob Arum amewasainisha mkataba mabondia hao ambao wapo tayari kuzichapa katika pambano ambalo limevunja rekodi kwani mabondia watachukua dola 250 milioni, huku Mayweather akilipwa asilimia 60 na Pacquiao, asilimia 40 ya fedha hizo.

Mayweather na Pacquiao ulingoni

Ndani ya ulingo kila mmoja ana aina yake ya uchezaji, Mayweather anacheza polepole, anatumia akili na kubadilika kulingana na mchezo huku Pacquiao akicheza ngumi za haraka haraka, ni staili ya kutompa mpinzani wake nafasi.

Pambano hili limebeba hisia za wanamasumbwi wa Tanzania ambao wameamua kulielezea:

Mada Maugo

“Ni pambano la karne, naweza kulifananisha na lile la Tyson na Evander au likawa zaidi ya lile, ni pambano ambalo dunia nzima itakuwa ikilifuatilia,” anasema bondia namba tatu kwa ubora nchini, Mada Maugo.

Maugo anampa Mayweather nafasi kubwa ya kushinda huku akibainisha kuwa pambano litakuwa zuri kuanzia raundi ya tano, kwani raundi za mwanzo kila mmoja atakuwa amempania mwenzake.

Habibu Kinyogoli

Kocha wa ngumi nchini, Habibu Kinyogoli anasema Mayweather ana nafasi kubwa ya kumpiga Pacquiao .

“Litakuwa pambano la kihistoria, nafasi ya ushindi ipo kwa Mayweather, ni bondia anayetumia akili, siyo bondia wa kutabirika, ana kitu cha ziada ulingoni.

“Anacheza kulingana na mchezo, anaweza kucheza ndani, nje, kati na vyovyote vile anavyotaka mpinzani wake,” anasema Kinyogoli.

Jay Msangi

Promota wa ndondi nchini, Jay Msangi anasema ni vigumu Mayweather kukubali kupigwa kwenye ardhi ya kwao.

Anasema upekee alionao Pacquiao ni kucheza ngumi haraka haraka, staili ambayo kama Mayweather asipokuwa makini anaweza kuwekwa katika mazingira magumu, kama atakubali kumpa nafasi Pacquiao aingie ndani.

Emmanuel Mlundwa

Rais wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania, Emmanuel Mlundwa anasema Pacquiao si bondia wa kupigwa kirahisi na kwenye pambano hilo anampa nafasi kubwa ya kushinda.

“Mayweather anacheza ngumi kali za kulia, lakini hana ‘jabu’, uchezaji wake ni wa taratibu, Pacquiao siyo bondia wa kupigwa kirahisi,” anasema Mlundwa.

Nasoro Michael

Bingwa wa dunia wa uzito wa juu kwenye mashindano ya Majeshi ya 1993, Nasoro Michael anasema aina ya uchezaji wa Mayweather, akiungwa mkono na mashabiki wa Marekani, vinamweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

“Simpi Pacquiao nafasi ya kushinda, kwanza atakuwa ugenini tofauti na Mayweather,” anasema Michael.

Historia zao mabondia hao

Floyd Mayweather Jr, alizaliwa Februari 24, 1977, Marekani na kupewa jina la Floyd Joy Sinclair, amekuwa mshindi wa tuzo ya Chama cha Waandishi wa Ngumi Marekani (BWAA) tangu mwaka 2007 na kupata tuzo nyingine kadhaa za masumbwi. Mayweather ana rekodi ya kutwaa mataji ya dunia ya WBC na WBA kwenye uzani wa welter, WBC uzani wa Super, WBA la vijana kwenye uzani wa kati.

Amecheza mapambano 47 na kushinda yote, 26 ameshinda kwa KO na hajawahi kupigwa, ana rekodi ya kutwaa medali ya shaba ya Olimpiki 1996. Majina ya utani anajulikana kama Pretty Boy, Money au TBE (The Best Ever).

Manny Pacquiao alizaliwa Desemba 17, 1978 Ufilipino na kupewa jina la Emmanuel Dapidran Pacquiao, majina yake ya utani ni Pac-Man, Ang Pambansang Kamao (The Nation’s Fist),The Mexicutioner, The Destroyer, Fighting Pride of the Philippines, Pambansang Ninon (National Godfather), The Fighting Congressman (citation needed) na The Filipino Slugger.

Amepigana mapambano 64 kati ya hayo ameshinda mara 57 na 38 ikiwa kwa KO, amepigwa mara 5 na kutoka sare mara mbili, ana rekodi ya kutwaa ubingwa wa WBC na anashikilia taji la dunia la WBO kwenye uzani wa welter. Mbali na ngumi, Pacquiao anacheza mpira wa kikapu, anafanya biashara, anaigiza, anaimba muziki na ni mwanasiasa, mjumbe wa Baraza la Congress la Ufilipino.