MIAKA 20 YA KIPANYA: Itaishi milele kutetea wanyonge (1)

Ali Masuod maarufu ‘Kipanya’
Muktasari:
Ali Masuod maarufu ‘Kipanya’, ni mmoja wa vijana hao. Yeye anajihusisha na harakati mbalimbali za kuleta mapinduzi ya fikra kwa kundi la vijana na Watanzania kutumia fursa, uwezo na kipaji chake katika uchoraji katuni maarufu kwa jina la Kipanya.
Dar es Salaam. Miongoni mwa Watanzania wengi, kuna vijana wachache walioamua kutumia maarifa na vipaji vyao ili kujiletea maendeleo na kuondokana na tatizo la kukosa ajira, wakijiajiri kwa kazi mbalimbali kisanaa kwa mikono yao.
Ali Masuod maarufu ‘Kipanya’, ni mmoja wa vijana hao. Yeye anajihusisha na harakati mbalimbali za kuleta mapinduzi ya fikra kwa kundi la vijana na Watanzania kutumia fursa, uwezo na kipaji chake katika uchoraji katuni maarufu kwa jina la Kipanya.
Mbali na uchoraji wa katuni, Masoud ambaye pia ni maarufu kwa jina la katuni anayoichora ya Kipanya ni mtangazaji, mshereheshaji, mwandaaji na mwongozaji wa vipindi kikiwamo cha Maisha Plus.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, msanii huyo anaeleza mengi ikiwamo safari ya maisha ya Katuni ya Kipanya, malengo na matarajio yake.
Masoud anabainisha kuwa alianza kazi ya uchoraji katika mazingira magumu yaliyosababisha kutembea umbali mrefu akitafuta ajira kabla ya kutambulika rasmi katika sanaa ya uchoraji katuni na mwaka huu ametimiza miaka 20 ya uchoraji wa Katuni ya Kipanya.
“Nafikiria mambo zaidi ya milioni moja katika kipindi cha nusu saa, lakini natumaini na kuamini inawezekana na siku moja nitafanikiwa,” anasema.
Swali: Katuni ya Kipanya imekuwa ikibadilika kadiri siku zinavyokwenda, anatafsiri nini katika maisha ya kila siku kwa Mtanzania?
Jibuu: Ni kweli, mwanzoni Kipanya alikuwa akionekana bila mavazi, akitembea kwa miguu minne, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda Kipanya akawa anabadilika kulingana na mazingira anayopitia au anayoingia.
Alianza akiwa hana mtoto kwa mwaka huo, lakini kwa sasa Kipanya ana mke na wakati mwingine anaonekana akitembea na mtoto wake. Kwa hiyo, kadri anavyoendelea kuishi, ipo siku atapata mjukuu.
Napenda Watanzania watambue kwamba, Kipanya ni mtetezi wa shida zao. Anatafsiri mambo mengi. Mara nyingi hufatilia mfumo wa siasa na utawala bora kwa sababu ndiyo mhilimili unaotoa majibu ya umaskini wa Mtanzania.
Unaweza kumwona akiwa bungeni, kwenye kamati ya kuibua maovu ndani ya vyama vya siasa. Kipanya ni Mtanzania anayehoji na kupigania matumizi ya rasilimali zake kumletea maendeleo. Huwezi kumwita mwanasiasa au mwanaharakati tu bali ni zaidi ya hayo.
Swali: Wazo la kutumia Mchoro wa Kipanya lilitokana na mtazamo gani uliokuwa nao kwa wakati huo?
Jibu: Mchoro wa Kipanya ni wazo lililokuja akilini baada ya kupata nafasi ya gazeti hilo la Majira, ambalo lilianza kuandika habari za siasa kwa uhuru zaidi, ikabidi nifikirie aina gani ya mchoro utakaokuwa ukiwakilisha mawazo yangu kwa njia ya katuni.
Ilikuwa ni ghafla Mchoro wa Kipanya ukanijia akilini na kuona unakidhi vigezo vya sanaa yangu.
Swali: Unaonekana kuanza kitambo uchoraji, ilikuwaje safari yako ya kielimu?
Jibu: Safari yangu ya upande wa elimu ilikuwa ni mwendo wa kuungaunga. Nimemaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi Kijitonyama mwaka 1986, lakini kutokana na sababu ambazo hadi leo sizielewi, sikuweza kufaulu katika mtihani wa darasa la sababu ingawa nilishishika nafasi kati ya moja hadi kumi kuanzia darasa la kwanza.
Kwa wakati huo, tayari nilikuwa nina msukumo mkubwa katika sanaa ya uchoraji.
Nikiwa bado njiapanda ya kuendelea na elimu ya sekondari, nikapata fursa adimu ya kusomea masomo ya Sanaa ya uchoraji (Fine Art) kwa miaka miwili, yaliyotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa kutumia mtalaa wa Chuo Kikuu. Hata hivyo, baada ya sisi kumaliza, darasa lile halikuendelea tena.
Nikiwa shule, nikaanza kuchora katuni zilizochapishwa katika Gazeti la Heko mwaka 1988, hapo nilikiwa na umri wa miaka 16, nilichora michoro ya hadithi za katuni.
Mwaka 1989 mwishoni, familia yetu ilipata ugeni wa mtoto wa mjomba wangu aliyekuwa akiishi Malawi. Kwa bahati nzuri alipoondoka nikaondoka naye kwenda Malawi.
Mazingira ya Malawi ilipokuwa ikiishi familia ya mjomba yalikuwa ni ya kijijini nami nilikuwa nimetokea mjini, hiyo mwaka 1990 nilipotakiwa kuanza masomo ya sekondari Malosa School eneo la Chilema kati ya Lilongwe na Blantyre nilianza kwa shingo upande na nikasoma kwa mbinde sana.
Nadhani utoto nao ulichangia, mwaka 1994 nikarudi Dar es Salaam baada ya kumaliza sekondari. Kwa msingi huo safari ya kielimu ni vizuri, mwaka 2008 nilijiunga na Chuo Kikuu Huria (OUT) kwa masomo ya Shahada ya Sayansi ya Siasa, ingawa miezi michache baadaye niliahirisha masomo na mpaka leo sijapata muda wa kuendelea.
Itaendelea wiki ijayo