Ukimpata kwa hongo, atakuacha kwa hongo

Muktasari:

  • Nenda insta. Fuatilia kurasa za mastaa hata wasio mastaa. Angalia idadi ya wafuasi wake, linganisha na michango ya post zake kutoka kwa wafuasi wake. Hapa ndipo utapata picha kuwa nusu ya wakazi wa taifa hili wanafikiri na kufanya vitu vyepesi sana.

Unataka kujua akili za Wabongo? Basi twende insta na mitandao yote ya kijamii. Huko utaelewa mabwege wa Kibongo wanafuatilia na kutaka nini. Huko ndiko ambako mwenye akili na asiye na akili wote wana thamani sawa. Tuendelee!

Nenda insta. Fuatilia kurasa za mastaa hata wasio mastaa. Angalia idadi ya wafuasi wake, linganisha na michango ya post zake kutoka kwa wafuasi wake. Hapa ndipo utapata picha kuwa nusu ya wakazi wa taifa hili wanafikiri na kufanya vitu vyepesi sana.

Inakuaje mtu una wafuasi zaidi ya milioni. Lakini uchangiaji wao kwenye kitu unachoposti hauzidi watu buku? Hao laki nane na elfu tisini na tisa wapo kwa ‘peji’ yako kwa ajili ya nini? Ndipo utajua kuwa wengi hawajui lolote. Wanafuatilia vitu rahisi sana.

Kimsingi Wabongo hufuatilia chochote. Kusema chochote na kuwaza chochote. Hata mvuta bange akipuliza mimoshi yake na kuanza kufokafoka ovyo. Dakika mbili tu utashangaa nyomi la wananchi limemzunguka kumshangaa. Wabongo hushangaa hata honi za malori.

‘Ene wei’ siyo tu kwamba Wabongo wao hufuatilia kila kitu. Niweke sawa hapa, Wabongo wengi hawana shughuli za kufanya. Wanaweza kupoteza muda kwa kitu cha kipuuzi tu. Ndo hao waliojazana huko insta na mitandao mbalimbali. Wao hufuatilia lolote, chochote na yeyote.

Ukitaka upate ‘uprofesa’ wa ghafla. Fanya utafiti kwa Wabongo ujue hulka yao katika kufuatilia vitu. Utatunukiwa ‘Uprofesa fasta’ endapo utalipeleka hilo andiko kwa Wanazuoni, linalosema kuwa Wabongo hufuatilia upuuzi zaidi badala ya vitu makini. Ndo ukweli.

Zama mitandaoni. Nenda hata kwenye vyombo vingine vya habari. Ama sikiliza nyimbo wanazopenda Wabongo wetu. Kama hiyo haitoshi tazama wanasiasa wa aina gani wanapendwa Bongo? Okei unaweza kusema siasa ni mchezo mchafu.

Basi fuatilia viongozi wetu wa kiroho waliojazana kila kona. Chunguza aina ya viongozi hao wa kiroho wanaopendwa sana na Wabongo. Hili nalo ukiona ni la kawaida, basi ujue wewe ni sehemu ya aina yao. Nenda mtaani kwako tazama aina ya watu wanaohusudiwa.

Ama angalia hata kwa familia yako basi. Kuna mpuuzi mmoja ndio kipenzi cha familia. Lazima. Ndivyo ilivyo hata mashuleni. Bongo ukifanya mambo makini huwezi kupata ufuasi mkubwa. Bongo wanataka vitu flan flan hivi laini laini, vyepesi.

Hata nyimbo za wasanii tunazopenda ni zile zilizoimbwa kirahisi. Zenye maneno mepesi na laini. Hatutaki zile kitu ngumu ngumu na zenye jumbe kali kali. Dunia hii kila kitu ni rahisi kupata na kufanya. Na kupenda vitu rahisi ndipo tunapopata watu rahisi.
Tunapata pesa kirahisi na matumizi yetu ni rahisi na zinaisha kirahisi. Hata ndoa zetu zinafungwa kirahisi na zinavunjika kirahisi. Unakumbuka msala wa muuza madini kule Mwanza? Yule ‘Msukuma’ aliyekatisha uhai wa pisi yake kwa risasi za moto?

Alipenda asipopendwa na akatumia pesa kupendwa. ‘Waifu’ alienda kwenye shoo ya ‘Mondi’, wakati alimkatazwa kutoka na mumewe. Simu ilipigwa na ‘bebiake’ haikupatikana. Hasira kali zikampanda changanya na wivu. Usiku huohuo baba la baba akarejea ‘homu’, kifua kikiwa kimejaa na akili imevurugika?

Pisi kali ikiwa bado na ubora wake uleule wa urembo. Shepu tamu na rangi adimu ya Kirangi. Ikakatishwa uhai kwa risasi zile za ‘Kirambo rambo’. Hata baba la baba naye akaiacha dunia itumie pesa na mali zake. Akaamia kujiua kibwege kwa risasi na ‘kuresti ini pisi’ kama ‘waifu’ wake.

Wakati yeye alitumia risasi kuutoa uhai wa ‘bebiake’ na yeye mwenyewe. Huko Goba kuna Msukuma kaidedisha pisi’ yake kwa panga na yeye kujisogeza zake polisi. Katika mazingira kama ya yule wa Mwanza. Wivu wa mapenzi ukaondoa uhai wa kiumbe pendwa.

Narudi palepale kwa Wabongo kupenda vitu rahisi. Unampata demu kirahisi kwa sababu ya pesa ambayo lazima uliopata kirahisi. Unasahau kuwa pia wapo wenye pesa zaidi yako. Wanaweza kuibeba pisi yako kwa pesa kama wewe. Unabebewa demu na wenye pesa zaidi yako.

Demu ambaye hata wewe ulimpata kwa sababu ya pesa. Na siyo upendo wala ndoa na kuvumiliana. Yaani uliweka pesa mezani tayari hapo hapo akawa wako. Sasa unakasirikia, unaleta wivu na kuua na wewe kujiua baada ya kubebwa na wenye pesa zaidi. Ulitegemea nini?

Ulipotumia pesa, unadhani hawakuwepo watu waliompenda? Waliompenda lakini pesa zako zikafanya wapishe wakuachie. Sasa wapo watu wenye pesa zaidi yako ambao nao watambeba kwa sababu ni dem mpenda pesa.

Kwanini unatuondolea ua la dunia kwa wivu wako? Kwanini unatuondolea pambo la dunia kwa wivu wa kibwege? Wewe ulipotumia pesa kwake na kumpata, hukuwaza pesa zitakufanya umkose na wewe? Ukitumia pesa sana kwa mwanamke. Tegemea kuna siku atakuacha kwa sababu ya pesa.

Na ninyi wanawake acheni kula pesa za wanaume ambao hamuwapendi. Kama unaona huna malengo na jamaa yako acha kula pesa zake. Mnaacha vilio kwa wapendwa wenu huku duniani kwa tamaa ya pesa.