Unyanyasaji wafanyakazi visiwani Zanzibar umulikwe

Katika siku za hivi karibuni kampeni ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji hasa wanavyofanyiwa watoto na akina mama imepamba moto.
Wanajamii, wakiongozwa na vyombo vya habari, wamekuwa wakifichua maovu ya aina kwa aina, yakiwamo ya unyama usioelezeka wa baadhi ya watu kunajisi watoto.
Pia, lipo eneo jingine la udhalilishaji na unyanyasaji unaendelea Zanzibar, ambalo kwa bahati mbaya limefumbiwa macho na husikii likizungumzwa, hivyo kuonekana kama vile halipo au ni jambo la kawaida.
Udhalilishaji huu ni ule uliopo katika maeneo ya kazi na hasa katika sekta binafsi. Huu unafanywa na wageni na wenyeji wanaoendesha biashara mbalimbali mijini na vijijini.
Wengi wa wafanyakazi katika sekta hizo hawana mikataba ya kazi na anapotokea mfanyakazi kudai mkataba hufunguliwa mlango na kuambiwa kwaheri ya kutoonana.
Wafanyakazi hawa hawana pa kwenda kulalamika na kutokana na shida ya kupata ajira wengi wanabaki kuvumilia, huku wakiumia kiafya na kimaisha.
Pia, wapo wafanyakazi hata katika kampuni kubwa ambao hawana mapumziko ya mwisho au katikati ya wiki, zikiwamo siku za sikukuu, ziwe za kitaifa au za dini.
Baya zaidi ni kwamba hapana malipo ya fedha wala chakula kwa watu hawa kwa kufanya kazi saa za ziada au siku za sikukuu.
Watu hawa wanalia na hawana wa kuwanyamazisha na hawana pahala pa kwenda kutoa malalamiko yao. Zipo tetesi kwamba waliojaribu kudai haki zao kupitia Idara ya Kazi na vyama vya wafanyakazi, wamejikuta wakikosa haki yao.
Vilevile mazingira ya hizo kazi nayo ni mabaya zaidi. Katika kampuni mbalimbali utaona wafanyakazi wa kike wanaingia au kutoka kazini usiku wa manane, kama vile hapawezi kuwekwa ratiba ya kuzingatia usalama wao.
Vilevile baadhi ya kampuni hazitoi usafiri na zile zinazofanya hivyo huwateremsha hawa wanawake mbali na makazi yao na hivyo kuhatarisha maisha yao. Hii ni hatari, hasa wakati huu ambao uhalifu umekua kwa kasi na kusikika habari za watu kubakwa kila mara.
Wamiliki wa kampuni hizi na maduka ya biashara wanafanya watakavyo kwa wafanyakazi wao, bila ya kujali afya zao na usalama wao kwa kuwa wanajua kwamba hakuna mwenye uwezo au utashi wa kuwakemea.
Wakati umefika kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kulitupia jicho suala hili na kuwasaidia wafanyakazi hao.
Ninachoweza kusema, tena bila ya kutafuna maneno, ni kwamba kinachofanyika ni sawa na utumwa mamboleo. Kosa la hawa wafanyakazi ni umaskini walionao au kupata ajira itakayowapunguzia njaa.
Ukweli ni kwamba maofisa wa Idara ya Kazi na vyama vya wafanyakazi wamebweteka na hawasimamii sheria na taratibu za kazi kwa sababu wanazozielewa wenyewe.
Kilichokuwa wazi ni kwamba maofisa hawa inaonekana kazi yao kubwa ni wakati wote kungojea sherehe za kila mwaka za Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi na kufanya maandamano makuba na kubeba mabango yenye maneno matamu bila ya kujali kwamba wafanyakazi wanaodai kuwawakilisha wana matatizo.
Viongozi hawa wakati wa sherehe za Mei Mosi hotuba zao mara nyingi hazigusii matatizo yanayowakuta wafanyakazi katika sekta binafsi, kama vile kufanya kazi bila ya mikataba.
Hali hii imesababisha wafanyakazi wengi kutokuwa na imani na Idara ya Kazi na vyama vya wafanyakazi kwa kuwa inaonekana kama vile hakuna anayejali masilahi yao wala afya zao.
Mazingira ya kazi katika baadhi ya sehemu yanatisha na ni hatarishi na wafanyakazi wengine hulazimika kuzifanya kazi hizo bila ya kinga zinazohitajika.
Wafanyakazi hawa hawana bima, wengi wao wanapougua ni juu yao kujilipia matibabu.
Wakati mwingine watu hawa wanapolazimika kubaki nyumbani kusubiri wapate afueni, siku ambazo hawaendi kazini zinahesabika kuwa hazistahili kufanyiwa malipo.
Zanzibar inapaswa kulimulika suala hili na kuchukua hatua za kuhakikisha mwendo huu wa kudhalilisha na kunyanyasa wafanyakazi unakomeshwa.
Huu mtindo wa wamiliki wa kampuni na wafanyabiashara kujali kupata faida na kutojali masilahi na afya za wafanyakazi wao, hauwezi kukubalika katika jamii yoyote ile ya kistaarabu kwa sababu huu ndio huo nilioueleza kama utumwa mamboleo.
Sio haki kutumia hali ya umaskini na shida za kazi walizokuwa nazo vijana, hasa akina mama kama mtaji wa watu wachache kujitajirisha huku mamia ya watu wake wakiumia na kudhalilika.
Ni kweli tumefungua milango kwa sekta binafsi kuchangia kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii ya taifa letu, lakini si kufanya hivyo kwa kuwadhalilisha na kuwanyanyasa wafanyakazi. Tunachohitaji ni mazingira mazuri ya kazi kama yanavyoelezwa katika sheria za nchi yetu na sheria za kimataifa.
Mapumziko kwa wafanyakazi si upendeleo bali ni haki yao na anayefanya kazi saa za ziada au siku za sikukuu ni haki yake kupata malipo maalumu kwa kuwa kazini siku hiyo.
Kama tunafurahia kubembeleza, basi tufanye hivyo kwa watoto wetu wachanga na si wamiliki na viongozi wa kampuni ambazo zinawadhalilisha na kuwanyanyasa wafanyakazi wao.
Ni lazima pawepo mikataba ya kazi na sio kuruhusu waajiri kufanya watakavyo kwa sababu ni wamiliki wa kampuni au biashara. Vilevile yawepo maelezo ya wazi ya wajibu, haki na masilahi ya mfanyakazi.
Siku hizi duniani ukatili kwa wanyama haukubaliki seuze kwa binadamu. Kwa nini tuwavumilie watu wanaodhalilisha wafanyakazi? Tuseme kwa kupaza sauti na kuchukua hatua madhubuti kwamba tumeamua kuhakikisha udhalilishaji na unyanyasaji kwa wafanyakazi Zanzibar unafika mw