Wawili watupwa jela kwa wizi wa maudhui ya DStv

Muktasari:

  • Mahakama hiyo imewakuta washtakiwa hao na hatia ya uharamia wa maudhui; hatua ambayo inachukuliwa kuwa ushindi katika vita dhidi ya mitandao ya maharamia inayoathiri tasnia ya habari utangazaji na burudani kote duniani.

MultiChoice Group, mtoa huduma za burudani anayeoongoza barani Afrika, na Irdeto, kampuni inayoongoza katika huduma za usalama wa majukwaa ya kidijitali mtandaoni, hivi karibuni wamepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya uharamia barani Afrika baada ya mahakama ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, imewaadhibu watu wawili, David Peter Sembosi na Sebastian Justinian John kila mmoja faini ya Sh20 Milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya uharamia wa maudhui kinyume na Sheria ya Makosa ya Mitandaoni.

Mahakama hiyo imewakuta washtakiwa hao na hatia ya uharamia wa maudhui; hatua ambayo inachukuliwa kuwa ushindi katika vita dhidi ya mitandao ya maharamia inayoathiri tasnia ya habari utangazaji na burudani kote duniani.

Uchunguzi uliofanywa na kitengo cha makosa ya mtandao ulibaini kuwa moja ya tovuti inayoeendeshwa kinyume na sheria iliweza kutazamwa au kutembelewa na wastani wa watu 200,000 kila mwezi nchini na kwingineko.

Maudhui ya DStv, huduma ya setilaiti kwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara inayomilikiwa na MultiChoice, yalitolewa kupitia tovuti inayoendeshwa kinyume na sheria ili kuwawezesha wateja wao kulipia na kuyapata kwa urahisi maudhui hayo.

Tovuti hiyo haramu pia iliwapa wateja wake nywila zisizo halali ili kupata huduma za DStv na kutazama maudhui yake. Matokeo ya uchunguzi na uamuzi huo unachukuliwa kuwa hatua kubwa iliyopigwa katika vita dhidi ya uharamia wa maudhui ambayo inazidi kukua siku hadi siku nchini na kuathiri sana sekta ya utangazaji na burudani.

Ukiukaji wa hakimiliki nchini unaigharimu biashara ya urushaji wa matangazo ya video kwa kiasi kikubwa kwani wawekezaji wanashindwa kupata faida inayotarajiwa kwenye uwekezaji na kuiingizia hasara kubwa ya mapato ya Serikali. Kwa kuwa uharamia wa maudhui ni kinyume cha sheria, maharamia hao hawana leseni hivyo hawalipi ushuru wowote wa Serikali.

Akizungumzia matokeo ya kesi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso alisema ukiukwaji wa hakimiliki umekuwa tishio kubwa kwa biashara ya utangazaji nchini Tanzania huku ikidumaza sekta ya uzalishaji wa maudhui kama vile filamu na kazi nyingine za sanaa kwa kudhulumu haki za wasanii na pia kukwepa kulipa mapato kwa Serikali.

“Tumefurahishwa na uamuzi huo, na tunaamini kwamba vyombo vyetu vya sheria vitaendelea kuhakikisha kuwa sheria zinatekelezwa kwa faida sio tu ya waendeshaji, lakini pia Serikali na tasnia ya ubunifu ya Afrika kwa ujumla.”

Alisema uamuzi huo utakuwa onyo kwa wote wanaohusika na vitendo vya ukiukaji wa hakimiliki na kuzitaka pande zote kutekeleza jukumu lao katika vita dhidi ya uharamia wa maudhui.

“Tunahitaji kuongeza ushirikiano kwa pande zote ikiwa ni pamoja na waendeshaji maudhui na wadhibiti kwa sababu wahalifu wanaendelea kuboresha mbinu zao,” alisema na kuongeza kuwa adhabu kubwa ni muhimu ili kuzuia vitendo hivi haramu.

Shane McCarthy, Ofisa Mwendeashaji Mkuu wa Maudhui ya Burudani za Video wa kampuni ya Irdeto alitoa maoni yake kuwa, “Unapoangalia hasara katika kadhia hii ya uharamia wa maudhui, unahitaji kuzingatia kampuni zinazozalisha maudhui, wale wanaolipa kihalali ili kupata huduma, lakini muhimu zaidi, jinsi inavyoathiri moja kwa moja uchumi na wasanii.”

Aidha alivipongeza vyombo vya sheria nchini akisema kuwa mahakama zimetuma ujumbe wa wazi kuwa hazitavumilia ukiukwaji wa hakimiliki, na Irdeto itaendelea kusaidia katika uchunguzi

dhidi ya watengenezaji wa programu tumishi kinyume cha sheria na wasambazaji wa vifaa vya uharamia wa mitandaoni na magenge yanayosaidia uwepo wa vitendo kama hivyo. “Hakutakuwa na mahali salama kwa maharamia,” alisisitiza.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Said Yakubu hivi karibuni alinukuliwa akisema, “Tumepokea malalamiko kadhaa kuhusu ukiukwaji wa hakimiliki hasa uharamia wa maudhui katika urushaji wa matangazo.

Naiomba mamlaka husika hasa COSOTA kulichukulia suala hilo kwa uzito na kuhakikisha sheria inatekelezwa. Tumefahamishwa kuhusu uharamia mkubwa wa maudhui hasa michezo na maudhui ya filamu.

Tunaelewa kuwa kuna watoa huduma za matangazo walio na haki ya kipekee kwenye maudhui fulani. Ni muhimu haki hizo ziheshimiwe na wadau wote ili kuepusha misuguano sokoni.”
 

Alisema kuwa Serikali inatambua kuwa uharamia wa maudhui ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili sekta hiyo na katika kukabiliana na hilo Serikali imeunda kamati maalum ya kupitia upya hali ya usimamizi wa sheria ya hakimiliki nchini na kupendekeza njia bora ili kulinda wamiliki wa hakimiliki