Zingatia haya unapovaa tai

Kuna mambo huhitajika kuzingatiwa ili kuvutia kila wakati, ikiwamo mpangilio wa mavazi.

Kwa kijana anayependa unadhifu na kutaka kupendeza katika kila aina ya tukio, hataweza kukosa kuwa na tai katika kabati lake.

Imezoeleka tai mara nyingi huvaliwa maofisini na katika sherehe na shughuli mbalimbali zilizo rasmi hasa na wanaume, lakini huvaliwa pia na wanafunzi wa shule, wavulana kwa wasichana.


Unapovaa tai unazingatia nini?

Msabaha Yaseen, mkazi wa Sinza Dar es Salaam anasema anapoamua kuvaa tai jambo ambalo huzingatia ni kuchagua ile itakayomfanya apendeze kulingana na aina ya mavazi anayovaa.

"Mimi ninazingatia zaidi kupendeza, hivyo ninavyochagua tai ninazingatia ile itakayonipa mwonekano nadhifu na maridadi," anasema Yaseen.

Mdau mwingine wa mavazi, Godfrey Gervas, anasema anapochagua aina ya tai anayovaa mara nyingi huzingatia rangi na aina ya suruali pamoja na shati alilovaa.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, muuzaji wa nguo za kiume jijini Dar es Salaam, Norbit Hassan anasema mtu anapoamua kuvaa tai anatakiwa kuzingatia aina ya umbo lake, kama ni mnene anapaswa kuvaa tai inayoendana na umbile lake.

Na kama wewe ni mwembamba basi unapaswa kuvaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Anasema ni muhimu kukadiria urefu sahihi na mlingano wa tai na koti au mkanda wa suruali.

Anasema tai inafanya muonekano wa mtu aliyevaa kuvutia zaidi endapo haitakuwa fupi sana wala ndefu sana.

“Tai inatakiwa isiwe ndefu mpaka kuvuka mkanda, inaweza kuwa juu kidogo ya mkanda au kukaribia juu ya mkanda," anasema Hassan.

Naye fundi wa nguo za kike na kiume, Abdul Kilumbi anaelezea ni vyema kuchagua tai ambayo rangi yake imekolea kuliko shati, rangi ya mkanda inapendeza zaidi ikifanana na ile ya viatu pamoja na kuzingatia ulingano wa upana wa tai na upana wa kola za koti.


Aina za tai

Kwa mujibu wa tovuti ya mitindo ya Afroswagga, zipo aina mbalimbali za tai, ikiwamo necktie ambazo ni ndefu zilizozoeleka kuvaliwa na wengi maofisini, shuleni au katika shughuli mbalimbali.

Pia kuna skinny necktie inayotaka kufanana na necktie, lakini yenyewe ni ndefu na nyembamba. Aina hii ya tai hupendelewa na vijana, maana zinafanya mtu uonekane unakwenda na wakati zaidi (more fashionable) na mwenye mwili mdogo.

"Pia, kuna Necker chief, hapa kitambaa (scarf) hutumika kuvaliwa shingoni kwa mitindo mbalimbali pamoja na bowtie (tai fupi) ambazo huvaliwa kwa kuangalia aina ya nguo," inaeleza Afroswagga.