Wabunifu mavazi wazingatie rika zote

Ubunifu

Muktasari:

Hili siyo jambo baya hata kidogo, maana hata duniani inasemekana kila mtu amekuja kwa njia yake, lakini linapokuja suala la jamii, kuna kila haja ya kufikiri jinsi ya kushirikisha jamii iliyokuzunguka katika mawazo yako, ili iweze kufurahia matunda au kushiriki kwa uchache kile ulicholeta.

Moja ya mambo yaliyotawala ubongo wa binadamu ni ubinafsi. Binadamu yeyote

kabla ya kuangalia jinsi anavyoweza kuchangia katika maisha ya mwenzake, hujiangalia kwanza yeye kama amejitosheleza.

Hili siyo jambo baya hata kidogo, maana hata duniani inasemekana kila mtu amekuja kwa njia yake, lakini linapokuja suala la jamii, kuna kila haja ya kufikiri jinsi ya kushirikisha jamii iliyokuzunguka katika mawazo yako, ili iweze kufurahia matunda au kushiriki kwa uchache kile ulicholeta.

Sanaa ya Tanzania kwa sasa imetawaliwa na vijana kwa asilimia kubwa. Katika utafiti ambao gazeti hili imeufanya, imebainika kuwa asilimia kubwa ya wabunifu wa mitindo ya mavazi ni vijana na kila siku hubuni mitindo mipya ya mavazi, nadhifu na yenye mvuto wa hali ya juu.

Hata hivyo cha kushangaza, mavazi hayo kwa asilimia kubwa huwa ni kwa ajili yao wenyewe, huku wakisahau kwamba kuna wazee, hata watoto ambao pia wana uhitaji katika suala la unadhifu. Vijana wabunifu wamesahau watoto katika ubunifu wao, badala yake wamekuwa wakitengeneza kwa nguvu nguo za rika la kati.

Utafiti umeonesha pia vijana wanaotengenezea mitindo mipya kila uchao pia ni vijana wa kike kuliko vijana wa kiume ambao hawaendi na mitindo mara kwa mara, lakini mahodari katika kununua pia mavazi ya kike kwa wenza wao, hata kwa ajili ya marafiki. Swali kubwa gazeti hili linalojiuliza ni je, jukumu la kulipendezesha taifa, lililo mikononi mwa wabunifu limeshindikana?

Badala ya kutoa mitindo ya ushawishi kwa kutengeneza mavazi mazuri kwa watoto na wazee ili kilam mmoja aende na wakati, wenyewe wanaelekeza nguvu zao kwa vijana wakiamini ndiyo wanunuzi wazuri wa mavazi.

Hatujawahi kushawishika hata mara moja kuamini kwamba watu wenye rika la utu uzima hawahitaji unadhifu. Ni dhahiri kwamba hawajaona kitu chenye mvuto kilicho sokoni kwa ajili yao kutoka kwa wabunifu wetu.

Hata upande wa watoto, tuna imani kwamba wazazi hawajashawishiwa kwa mitindo nadhifu kwa ajili ya watoto wao.

Kuna haja ya wabunifu wetu kuwaza zaidi kuhusu unadhifu na kubuni mavazi kwa watoto na watu wazima badala ya vijana pekee mkikumbuka unadhifu ni suala la msingi kwa taifa zima na siyo kwa rika moja la vijana.

Hapa nakumbushia suala la Vazi la Taifa nikikumbuka mchakato wake ulioanza muda mrefu uliopita, lakini bado haujatoa majibu.

Juzi Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara aliwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake, pia hakuwa na jibu linaloonyesha kuwa kama taifa kuna vazi rasmi litakalowatambulisha Watanzania kwingineko.

Nasisitiza umuhimu wa wadau kukamilisha mchakato wa vazi la taifa ili hatimaye kuwe na vazi rasmi la Kitanzania litakalowafanya wananchi kutembea kifua mbele kwa kujivunia utaifa, utakaotambulishwa na vazi hilo.

Pia kwa wabunifu wa mavazi, kikubwa na jambo la msingi ni ushawishi katika ubunifu na suala la utaifa likiwekwa mbele. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuwa na taifa nadhifu.

Tunawatakia Jumamosi njema.