Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Tutapitia magumu, niko tayari’

Dar es Salaam. Sasa ni rasmi. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu anarejea nchini huku akisema; “nakuja kushiriki kuandika ukurasa wa kwanza mpya wa kitabu chenye kurasa 365 cha mwaka huu wa 2023.”

Ujio wa Lissu unatokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Januari 5, 2023 iliyopokea na kujadili taarifa ya mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano baina ya timu ya chama hicho na CCM.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kiliwataka makada wake walioko uhamishoni kurejea nchini.

Kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na viongozi wa vyama vya siasa Ikulu jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, alitangaza kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara iliyozuiliwa tangu mwaka 2016.

Mbali na Lissu, wengine waliokimbilia uhamishoni ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje.

Akizungumza jana na Watanzania kupitia mitandao ya kijamii, Lissu alitangaza kurejea Januari 25, mwaka huu akitokea nchini Ubelgiji alikokimbilia.

Alisema licha ya ahadi ya Rais Samia na utayari wake (Lissu) na chama chake wa kufanya siasa, siku zijazo hazitakuwa rahisi kwao.

“Ninajua tutakabiliwa na majaribu ya kila aina na tutapitishwa katika tanuru kubwa la matatizo na magumu mengi.

“Lakini licha ya mazingira hayo magumu na mbele ya changamoto kubwa na nyingi zitakazotukabili, ninaamini kwamba kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yeremia, Mwenyezi Mungu anatuwazia sisi Watanzania mawazo ya kutustawisha na wala sio ya kutuumiza, mawazo ya kutupa tumaini kwa siku zetu zijazo,” alisema Lissu.

Akitoa salamu zake za mwaka mpya wa 2023, Lissu, aliyesema amelazimika kuzichelewesha kutokana na kikao cha Rais Samia na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema 2023 ni wa kupambana kupata Katiba mpya.

“Ni mwaka ambao kama tukiamua kwa dhati ya mioyo yetu, tutapata Katiba mpya na ya kidemokrasia, yenye mfumo huru wa uchaguzi, inayojali na kulinda haki za wananchi na inayoweka misingi imara ya uwajibikaji wa viongozi wetu kwa wananchi na wawakilishi wao,” alisema.

Alisema kwa kuwa Rais Samia na chama na Serikali wameshaahidi hadharani kwamba wako tayari kuanza safari hiyo ndefu na ngumu, wako tayari kumjibu kwa vitendo kwamba wamejipanga kwa safari hiyo.

“Mimi binafsi na chama chetu tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo. Ninarudi kwa ajili ya kazi kubwa iliyoko mbele yetu, kazi ya Katiba mpya na mwanzo mpya kwa Taifa letu,” alisema Makamu Mwenyekiti huyo.

Alisema kutokana na mwelekeo uliotolewa na Rais Samia kuhusu mabadiliko makubwa ya kisheria na kikatiba yanayohitajika kufanyika kama sehemu ya maridhiano ya kisiasa nchini, bado kuna kazi kubwa ya maandalizi ya kitaalamu na timu za wataalamu wa Chadema, CCM na Serikali.


Kurejea

Lissu, ambaye aliondoka nchini Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma, alisema miaka mitano ya kuishi uhamishoni imekuwa ya mateso.

Lissu, aliyekwenda kutibiwa Nairobi nchini Kenya kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji, alirejea nchini Julai, mwaka 2020 kushiriki Uchaguzi Mkuu na aliondoka tena kurejea Ubelgiji Novemba 2020.

“Ukiondoa takriban miezi mitatu ya kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, nimeishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka mitano.

“Hiki kimekuwa kipindi kirefu na kigumu sana katika maisha yangu binafsi na yetu kama chama na kama Taifa. Hata hivyo, kama nilivyosema katika salamu zangu za mwaka mpya mwaka jana, “hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo,” alisema Lissu.

Alisema anatarajia kurejea nchini Januari 25 na atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Ethiopia akitokea Brussels, Ubelgiji, kupitia Addis Ababa, Ethiopia.

“Panapo majaliwa nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano ya tarehe 25 Januari, 2023, majira ya saa saba na dakika 35 mchana.

“Kwa vyovyote itakavyokuwa, mwaka huu utakuwa wa muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Tukiweka nia ya dhati na kuitekeleza kwa dhati, tutayashinda majaribu na magumu yaliyo mbele ya safari yetu,” alisema.

Alipoulizwa kwa simu jana Mkurugenzi wa Itifaki na Uhusiano wa Kimataifa wa Chadema, John Mrema kuhusiana na ujio huo wa Lissu alisema; “ngoja kwanza chama kitatoa kauli.”


Safari ya Lissu

Lissu aliondoka nchini Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana eneo la Area D, jijini Dodoma karibu na yalipokuwa makazi yake.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki, alipelekwa jijini Nairobi nchini Kenya kwa matibabu baada ya shambulio hilo.

Lissu alifanyiwa matibabu nchini Kenya hadi Januari 6, mwaka 2018 aliposafiri kwenda Ubelgiji kwa ajili ya matibabu zaidi, kadhalika makazi ya uhamishoni.

Nguli huyo wa sheria aliyewahi kukiongoza Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), aliishi Ubelgiji hadi Julai 27, 2020 aliporudi Tanzania kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Kurejea kwa Lissu nchini wakati huo kulitokana na chama chake kumpitisha kupeperusha bendera ya chama hicho kuwania urais ambao hata hivyo, hakushinda.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), katika uchaguzi huo, Lissu, aliyechuana na Rais John Magufuli wa CCM aliyekuwa akigombea kwa kipindi cha pili alishinda kwa kupata kura zaidi ya 12.51 milioni, huku Lissu akipata kura zaidi ya 1.93 milioni.

Baada ya uchaguzi huo, Lissu alidai kupata vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana, hivyo akakimbilia katika Ubalozi wa Ujerumani kuomba hifadhi na Novemba 10 aliondoka tena nchini na kurejea tena Ubelgiji.

Mara kadhaa alipoulizwa kuhusu mpango wa kurejea nchini, mwanasiasa huyo alijibu ni vigumu kutekeleza hilo hadi pale Serikali itakapotoa hakikisho la usalama wake.

Desemba 7, mwaka 2021 baada ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kumfutia kesi zilizokuwa zikimkabili, Lissu aliliambia Mwananchi kuwa hachukulii hatua hiyo kama hakikisho la usalama wake pindi atakapoamua kurejea nchini.

“Ni hatua nzuri, lakini jambo la pili wanatakiwa wanihakikishie usalama wangu. Hilo linahitaji kauli yao. Wakitoa kauli sina sababu ya kuendelea kuishi huku.

“Mimi sikukimbia nchi kwa sababu ya kesi za kubumba kama hizo walizonifungulia. Nilikimbia nchi kwa sababu ya jaribio la mauaji dhidi yangu. Serikali inatakiwa kunihakikishia usalama wangu ili niweze kurudi nyumbani nikijua nitakuwa salama. Hilo likifanyika nitarudi nyumbani,” alisema Lissu.

Juni 7, 2022, akijibu swali bungeni la Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega aliyetaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu viongozi wa Chadema walioko nje ya nchi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema hakuna sababu ya viongozi hao kutorejea nchini.

“Hakuna sababu yoyote kwa Mtanzania aliyeko popote pale, ikiwemo viongozi hao wa Chadema walioko nje ya nchi kutorejea nchini ili sio tu waweze kutumia fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi na kisiasa, lakini kushiriki kikamilifu katika kutoa michango yao kwa maendeleo ya nchi yao katika nyanja yoyote, kwani hapa ni nyumbani kwao,” alisema.

Baada ya hatua hiyo, Lissu aliahidi kurejea Tanzania kabla ya Septemba mwaka jana na hata hivyo hakurejea hadi baada ya Januari 3, Rais Samia kuzungumza na viongozi wa vyama zaidi ya 19 vya siasa na kuruhusu mikutano ya hadhara.

Baada ya ruhusa hiyo, Kamati Kuu ya Chadema iliketi Januari 5, mwaka huu na pamoja na mambo mengine iliwaita viongozi wake waliopo ughaibuni warejee kushiriki uzinduzi wa mikutano hiyo utakaofanyika Januari 21.

Katika mpango wa kurejea kwao, Lissu ndiye atakayetangulia, akifuatiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Lema kisha Wenje.

Kurejea kwa mwanasiasa huyo na wengine wa upinzani waliokuwa ughaibuni kunalenga kuziungurumisha siasa za majukwaani baada ya ruhusa ya mikutano ya hadhara, jambo ambalo lilikosekana kwa takribani miaka sita.