Lissu kurejea Tanzania Januari 25

Muktasari:
Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu amesema, anatarajiwa kurejea nchini Tanzania Januari 25, 2023 akitokea Ubelgiji alikorejea Novemba 10, 2020, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu amesema anatarajiwa kurejea nchini Tanzania Januari 25, 2023 akitokea Ubelgiji alikorejea Novemba 10, 2020, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Lissu amesema hayo leo Ijumaa, Januari 13, 2023 wakati akizungumza na Watanzania wa ndani na nje kupitia mtandao wa ‘Zoom.’
Lissu ametumia kile alichokiita salamu zake za mwaka mpya 2023 kueleza tarajio lake la kutua nchini Januari 25, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 7:35.
“Naomba kutumia salamu zangu za mwaka huu mpya wa 2023 kuwafahamisha kwamba, panapo majaliwa nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano Januari 25, 2023 majira ya saa saba na dakika 35 mchana,” amesema.
Lissu alirejea Ubelgiji akieleza kutishiwa usalama wake baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu alipogombea urais wa Tanzania kupitia Chadema. Alishindwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli.
Aliondoka kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 kwenda Nairobi Kenya kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi katika makazi yake eneo la Area D jijini Dodoma muda mchache baada ya kutoka bungeni.
Hata hivyo, Lissu alipatiwa matibabu nchini Kenya hadi Januari 6, 2018 aliposafiri kwenda Ubelgiji kwa ajili ya matibabu zaidi, kadhalika makazi ya uhamishoni.
Julai 27, 2020 alirudi Tanzania kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.