Lissu arudi Ubelgiji akitokea ubalozi wa Ujerumani
Muktasari:
Tundu Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema alirejea Tanzania Julai 27, 2020 akitokea nchini Ubelgiji baada ya kuishi nchini humo kwa zaidi ya miaka miwili akipatiwa matibabu ya shambulio la risasi la Septemba 7, 2017 jijini Dodoma.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuomba hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu amesema leo Jumanne Novemba 10, 2020 ameondoka kwenda Ubeligiji alikokuwa akiishi tangu Januari 2018.
Lissu aliyeomba hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani tangu Novemba 2, 2020 akidai kutishiwa maisha yake, ameieleza Mwananchi Digital leo Jumanne Novemba 10, 2020 kuwa amesafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia itakayopitia Addis Ababa, kisha Vienna Austria na kituo cha mwisho kitakuwa Brussels, Ubeligiji.
“Ninaelekea Ulaya sasa hivi,” alisema Lissu kupitia ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa WhatsApp saa 9:29 alasiri.
Amesema anakwenda nchi hiyo kwa sababu tayari anayo ruhusa ya kuishi huko tangu alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Nakwenda Ubelgiji. Sio political asylum (hifadhi ya kisasa), mimi nina ruhusa ya kukaa Ubelgiji tangu nilipokwenda kwa matibabu Januari 2018. Kwa hiyo sihitaji kuomba political asylum,” amesema.
Lissu alirejea Tanzania Julai 27, 2020 akitokea nchini Ubelgiji na kushiriki mchakato wa kugombea urais kupitia Chadema ambapo chama hicho kilimpitisha. Katika uchaguzi huo Lissu alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais John Magufuli.