Lissu aeleza sababu kuhamia ubalozini

Tundu Lissu

Muktasari:

Makamu mwenyekiti wa Chadema na aliyekuwa mgombea urais, Tundu Lissu yuko ubalozi wa Ujerumani, ambako ameomba hifadhi ya kisiasa kwa maelezo kuwa ametishiwa maisha.

Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa Chadema na aliyekuwa mgombea urais, Tundu Lissu yuko ubalozi wa Ujerumani, ambako ameomba hifadhi ya kisiasa kwa maelezo kuwa ametishiwa maisha.

Amesema hayo wakati kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akisema atatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Lissu alisema alikwenda ubalozi huo Jumatatu kwa sababu alipigiwa simu za kutishiwa maisha na kuwa anachofanya sasa ni kuendelea na mipango ili asafiri nje ya nchi.

“Nipo ubalozini kwa sababu ya vitisho vya maisha yangu. Nilianza kutishiwa Jumamosi, nilipigiwa simu na watu wakanitishia maisha, jioni ya siku hiyo pia nilipigiwa simu,” alisema Lissu ambaye ni mwanasheria.

“Jumapili niliondoka na kulala kwa marafiki, Jumatatu ndio nikaenda ubalozi wa Ujerumani.”

Lissu alisema hawezi kukaa katika ubalozi huo kwa muda mrefu.

“Tunafanya utaratibu ili niweze kuondoka nchini kwa ajili ya usalama wangu. Ninafanya utaratibu niweze kuondoka nchini kwa ajili ya usalama wangu. Nikiwa naendelea na utaratibu nitaendelea kukaa kwa balozi hapa.”

Alipoulizwa na Mwananchi kama polisi wana taarifa za madai ya Lissu kutishiwa usalama wake na kwamba amejisalimisha ubalozini, Kamanda Mambosasa alisema asingeweza kuzungumza lolote kwa sabbau hakuwa ofisini na kuahidi kuzungumzia suala hilo leo.

Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Christopher Kadio alisema ofisi yake haina taarifa Lissu kutishiwa usalama wake wala kujisalimisha ubalozi.

Lissu, ambaye amekuwa nje ya nchi kwa takriban miaka mitatu akitibiwa majeraha yaliyotokana na shambulizi la risasi 16, alikamatwa na polisi Novemba 2, akiwa nje ya jengo la Umoja zilipo ofisi za ubalozi za nchi za Ulaya na kupelekwa kituo kikuu cha polisi cha Dar es Salaam, lakini akaachiwa muda mfupi baadaye.